Habari za Punde

Serikali yapokea vifaa vya ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano

  Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustafa Aboud Jumbe kati kati aliyevaa Kanzu akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kujionea vifaa vya Ujenzi wa Bara bara vilivyonunuliwa na Serikali hapo Kibele Mkoa Kusini Unguja.
 Nd. Mustafa akimuonyesha Balozi Seif  Mtambo wa Kupikia Lami uliyoigharimu Serikali Dola za Kimarekani Laki 927,000 ukisubiri kufungwa kwa ajili ya majaribio la baadae kuanza kazi mara moja.


  Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Nd. Mustafa akimuonyesha Balozi Seif Gari la kuchanganyia Lami na Kokoto lililokwisha wasili Kibele Mkoa wa Kusini Unguja.

  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akiusisitiza Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuwa makini katika matumizi ya Vifaa vipya vilivyonunuliwa na Serikali kwa Gharama kubwa.
Muonekano halisi wa Mtambo wa kuchanganyia Lami uliotoka Nchini Brazil unavyoonekana kwa mbali.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kupokea Vifaa mbali mbali vya ujenzi wa Miundombinu ya Mawasiliano Nchini ilivyovinunua kutoka Nchini Brazil na Italy kwa ajili ya kuimarisha kazi ya utengenezaji wa Bara bara Nchini katika kiwango cha kitaalamu zaidi.
Asilimia kubwa ya vifaa hivyo vilivyoletwa Nchini karibu Mwezi Mmoja uliopita hivi sasa vimewekwa katika eneo la Kibele vikisubiri Mtaalamu wa kuvifunga ili vifanyiwe majario na kuanza kazi mara moja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na baadhi ya Mawaziri na Manaibu Mawaziri alifika katika eneo la Kibele kujionea mwenyewe Vifaa hivyo vitakavyoleta ukombozi Mkubwa kwa Idara ya Utunzaji na Utengenezaji Bara bara Zanzibar {UUB }.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Nd. Mustaha Aboud Jumbe alimueleza Balozi Seif kwamba awamu ya kwanza ya Vifaa hivyo ilitanguliwa na Mtambo wa kupikia lami ulionunuliwa na Serikali kwa gharama ya Dola za Kimarekani Laki 937,000.
Nd. Mustafa alisema vifaa vyengine ni Gari la kuchanganyia lami na kokoto, Gari ya kutandazia Lami ya moto pamoja na Gari ya kutandazia Lami wakati wa ujenzi wa Bara bara.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji alieleza kwamba Awamu ya pili ya vifaa hivyo itakayojumuisha pia magari  kumi pamoja na Grader vinatarajiwa kuwasili Nchini si zaidi ya Mwezi Juni Mwaka huu.
Nd. Mustafa aliishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada iliyochukuwa kuamua kununua vifaa hivyo vitakavyolea mabadiliko makubwa ya Uwajibikaji kwa watendaji wa UUB.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara Zanzibar Nd. Ali Tahir Fatawi alisema Mtambo huo ulionunuliwa kwa kuzingatia hali halisi ya Mazingira Nchini ni wa pili kununuliwa na Serikali ambao utasaidiana na ule unaotumika hivi sasa.
Nd. Tahir alisema wakati mtazamo wa Wizara ya Ujenzi kupitia Idara yake ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara umelenga kununua Lami Tani Elfu 1,000 mafunzo Maalum kwa Wafanyakazi kuweza kumudu kuviendesha vifaa hivyo vya kisasa yatatolewa.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wahandisi pamoja na Wafanyakazi wa Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara {  UUB } kwa sasa hawatakuwa na visingizio vya ukosefu wa vifaa vya kazi wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Balozi Seif  alitahadharisha kwamba wakati Serikali imejikita kununuwa vifaa hivyo kwa gharama kubwa mno Wahandisi na Wafanyakazi wa UUB wanapaswa kuwa makini na kuacha tabia ya kujaribu kubahatisha katika matumizi ya vifaa hivyo muhimu.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wake Dr. Ali Mohamed Shein imenunuwa vifaa hivyo vinavyokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni Tatu za Kitanzania ikilenga kuimarisha Sekta ya Mawasiliano hapa Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.