Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia UWT Jimbo la Magomeni Wafanya Usafi wa Mazingira Hospital ya Mental Kidongochekundu

Na  Mwashungi Tahir  Maelezo Zanzibar.
Jamii nchini imetakiwa kujitolea kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Magonjwa ya Akili Kidongo chekundu kila inapopata nafasi badala ya kusubiri siku maalum ya kumbukumbu za kitaifa kufanya usafi huo.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Kinamama UWT Jimbo la Magomeni huko Hospital ya Magonjwa ya akili Kidonge Chekundu walioshiriki zoezi la usafi katika maeneo hayo ikiwa ni shamra shamra ya maadhimisho ya juma la akinamama ambalo kilele chake ni kesho Machi 8, duniani kote.
Amesema kinamama hao wamefanya maamuzi mazuri ya kwenda kufanya usafi maeneo hayo kutokana wagonjwa hao wanahitaji mazingira yao kuwa masafi licha ya kuwa hali za akili zao haziko sawa.
Amesema hali hiyo haiwasababishii wao kuishi katika mazingira machafu na kwamba jukumu la mazingira hayo kuwa safi ni la jamii inayowazunguka.
Mwakilishi huyo amesema Wagonjwa hao wanahitaji faraja na utulivu wa hali ya juu hasa ikizingatiwa kuwa wenyewe hawawezi kusafisha.
“Shukurani pekee zije kwenu kwa maamuzi mliyoyatoa ya kuja hapa na kuwafanyia wenzetu wagonjwa usafi kwani usafi ni muhimu kwa kila mtu. Hata kama wana magonjwa ya akili lakini wanastahiki waishi katika mazingira mazuri”, alisema Mwakilishi Shamsi.
Aliwaasa wenye tabia ya kuwadharau watu wenye magonjwa ya akili kuacha tabia hiyo na kuwataka kuwa karibu nao katika kuwapa faraja.
Amefafanua kuwa hakuna Mgonjwa yeyote aliyetakuwa kuugua isipokuwa baadhi yao wamezaliwa nao na wengine wamepata kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo na madawa ya kulevya.
Hivyo alitoa wito kwa kinamama kufanya kulifanya zoezi la usafi katika maeneo hayo kuwa endelevu kila wanapopata nafasi na sio kusubiri siku maalum.
Mwakilishi huyo alitumia nafasi hiyo pia kuwataka kinamama wa Jimbo la Magomeni kuzidisha mashirikiano katika utendaji wao wa kazi ili kuleta maendeleo zaidi katika jimbo hilo.
Kwa upande wa Madiwani wa Jimbo hilo wamesema kuwa binaadamu yeyote  ni mgonjwa mtarajiwa hivyo anapaswa kuwa na huruma kwa wagonjwa wa maradhi hayo na kuzitaka jumuiya nyengine kujitokeza kila baada ya muda kuwawekea mazingira yao katika hali ya usafi.
Nae katibu wa Hospitali ya magonjwa ya akili Kidonge Chekundu Bhai Ibrahim Khamis ameishukuru Jumuiya ya Kinamama UWT Jimbo la Magomeni kwa uamuzi wao wa kwenda kufanya zoezi la usafi katika Hospital hiyo.
Aidha ameziomba taasisi na jumuiya nyingine kuiga jambo hilo kwa kujitokeza kufanya usafi na kuleta misada mbali mbali ikiwemo Vifaa vya kufanyia usafi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.