Habari za Punde

Mbunge na Mwakilisho wa Jimbo la Mahonda Wakabidhi Vifaa Vya Michezo Kwa Timu 22 za Jimbo Hilo leo.

Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na Mbunge wa Jimbo hilo Bahati Abeid Nassir wakitoa Vifaa vya Michezo kwa Timu za Soka 22 za Jimbo la Mahonda hapo Tawi la CCM Kitope.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na Mbunge wa Jimbo hilo Bahati Abeid Nassir wakitoa Vifaa vya Michezo kwa Timu za Soka 22 za Jimbo la Mahonda hapo Tawi la CCM Kitope.
 Mbunge wa Jimbo la Mahonda Bahati Abeid Nassir akiwaasa Vijana kupenda michezo ili kujiepusha na ushawishi wa kujiingiza katika matendo maovu.
Mmoja miongoni mwa Viongozi wa Timu 22 za Jimbo la Mahonda Said maarufu Kocha John akitoa shukrani kwa Uongozi wa Jimbo la Mahonda mara baada ya kupokea Seti za Jezi na Mipira.
Picha na  - OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Jimbo la Mahonda umekabidhi vifaa vya Michezo kwa Timu 22 za Soka za Madaraja tofauti yaliyomo ndani ya Jimbo hilo pamoja na Timu Moja ya Mchezo wa Pete {Netball} katika azma ya kuimarisha Sekta ya Michezo Nchini kama Sera ya CCM inavyoeleza.
Vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na Seti za Jezi na Mipira Miwili kwa Timu iliyowakilisha Kiongozi wake vimetolewa hapo katika Tawi la Chama cha Mapinduzi Kitope vikigharimu jumla ya Shilingi Milioni 14,200,000/-.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi na Mbunge wa Jimbo hilo Bahati Abeid Nassir wakiambatana na Mke wa Balozi Seif  Mama Asha Suleiman Iddi walizikabidhi Timu za Aluta, Fujoni Star, Fujoni Boys na African Boys za Daraja la Pili.
Timu zilizokabidhiwa za Daraja la tatu ni Kiomba Mvua, Mbuyuni, Kichungwani United, Kinduni City, Simba Watatu, Kichungwani Star, Small Killer, Mtetema, Mnarani na Mandela.
Kwa upande wa Timu zilizo katika Daraja la Kati{ Central  } ni pamoja na  Timu za Mto Mchanga Kids, White Nacet, Spear Kids,  Kilima Baridi pamoja na Black Fighter.
Akizungumza na Viongozi na Wachezaji hao Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif alisema huo ni utararibu unaoendelea kutekelezwa na Uongozi wa Jimbo hilo katika kuwajenga Vijana kupenda Michezo ikiwa ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kuimarisha Sekta hiyo Nchini.
Balozi Seif  alisema Kijana anapoamua kushughulikia Fani ya Mchezo aelewe kwamba ni moja ya njia ya kumpatia ajira sambamba na  kujiweka tayari katika ulinzi wa Afya yake ya kila siku.
Alisema kwamba kwa Kijana Mchezo lazima uwepo ndani ya moyo wake ili uweze kumfaaa hapo baadae ambapo aliendelea kukumbusha kwamba mchezo ni faraja ya akili iwapo kama haikushughulishwa inakuwa Nyumba ya Shetani.
Alisema wakati Uongozi huo ukiandaa mazingira ya kuzipatia Viatu Timu hizo uko mbioni kutoa Vikombe vitakavyoshindaniwa na timu hizo katika muelekeo wa kupata Timu bora ya Kombaini ya Jimbo.
Naye Mke wa Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda Mama Asha Suleiman Iddi alisema Michezo itaendelea kubakiakuwa na gharama kubwa inayolazimika Wazee kwa kushirikiana na Viongozi waendelee kuwaunga mkono Vijana walioamua kujishughulisha na Sekta hiyo muhimu hivi sasa.
Mama Asha alisema Uongozi wa Jimbo hilo utajitahidi katika kuhakikisha Timu zote zilizosajiliwa na Chama cha Mapira wa Miguu ZFA zinapata Msukumo wa kusaidia vifaa.
Hata hivyo Mama Asha alitanabahisha kwamba ndani ya Jimbo la Mahonda zipo Timu zaidi ya 40 idadi ambayo Uongozi huo hautakuwa na nguvu za kuvihudumia vyote lakini kwa kuanzia wanaendelea kuvipa msukumo vile vilivyosajiliwa na kuingia katika mashindano.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Mahonda Bahati Abeid Nassir alisema Viongozi wanaoamuwa kuwasaidia Vijana wao kujihusisha na Michezo wanawasaidia kujiepusha na vitendo viovu kama matumizi ya dawa za kulevya na ubakaji.
Mbunge Bahati alisema Kijana anapoamua kuutumia muda wake mwingi katika shughuli za michezo humuondolea kirwa potovu zinazopelekea kumshawishi kujiingiza katika matendo hayo mabaya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.