Habari za Punde

Ujenzi wa majengo mapya kwa ajili ya skuli za Sekondari utasaidia kuondosha uhaba wa madarasa

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiukagua ukumbi wa Mitihani wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda uliojengwa kwa nguvu za Wananchi na Walimu.
 Balozi Seif  akiwahakikishia Walimu, Wanafunzi na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Mahonda kukamilishiwa jengo lao la Ukumbi wa Mikutano lilisimama kwa kipindi kirefu sasa.
  Balozi Seif kizungumza na Uongozi wa Kamati, Walimu na Wananchi wa Mahonda mara baada ya kulikagua jengo linalotarajiwa kuwa Ukumbi wa Mitihani wa Skuli ya Sekondari ya Mahonda.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Rajab Ali Rajab.
 Jengo linalotarajiwa kuwa Ukumbi wa Mitihani la Skuli ya Sekondari ya Fujoni lililosimama ujenzi wake kwa kipindi kirefu sasa.
 Baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Skuli ya Fujoni, Wazazi na Maafisa wa Tasaf wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati alipotembelea Maendeleo ya Skuli hiyo.
Mkurugenzi Uratibu Shughuli za Serikali SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amrani akiwaahidi Wananchi wa Shehia ya Fujoni kukamilishwa ujenzi wa Ukumbi wao wa Mitihani kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf katika Mkutano wao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mradi wa Ujenzi wa Majengo Mpya ya Skuli za Sekondari za Ghorofa unaofanywa na Serikali katika maeneo tofauti Nchini utakapokamilika utasaidia kuondosha changamoyo za uhaba wa Madarasa.
Alisema Mradi huo uliopangwa kutekelezwa kwa Skuli zipatazo 20 kila Wilaya pamoja na yale maeneo yenye idadi kubwa ya Wanafunzi wa Sekondari italeta faraja kubwa mbali ya Wanafunzi lakini pia kwa Wazazi.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa Kamati za Skuli za Sekondari za Mahonda na Fujoni pamona na Walimu alipofanya ziara ya kukagua Kumbi mbili za kufanyia Mitihani za Skuli hizo zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi na Walimu.
Alisema Serikali Kuu kupitia Sera ya Elimu ililazimika kujizatiti katika kuongeza Majengo ya Skuli kwa lengo la kukidhi mahitaji halisi ya ongezeko kubwa la Idadi ya Watu Nchini ambayo asilimia kubwa ni Wanafunzi.
Balozi Seif  alisema wakati Serikali ikiendelea na harakati zake za kujenga miundombinu katika Sekta ya Elimu, Uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf } unaoratibiwa na Ofisi yake kwa upande wa Zanzibar umeahidi kuongezea nguvu Miradi iliyoanzishwa na Wananchi.
Alisema Tasaf Awamu ya Tatu katika mkupuo wa Pili imejipanga kukamilisha ujenzi wa Kumbi Mbili za Mitihani za Skuli ya Mahonda na Fujoni ambazo zimesita ujenzi wake kwa muda mrefu sasa.
“ Nakuthibitishieni Uongozi wa Skuli ya Sekondari Mahonda na Fujoni kukamilishwaujenzi wa Majengo hayo ili kuunga mkono nguvu za Wananchi zinazoonekana kutaka kupotea”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi, Viongozi na Walimu hao katika Mikutano Miwili tofauti kwamba Mradi wa Tasaf umeendelea kufanya kazi kubwa ya kuwajengea uwezo Wananchi wake hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Balozi Seif  alieleza kwamba yapo mafanikio mengi kupitia Mradi huo na kupelekea Zanzibar kupaa katika Nyanja za Kimataifa iliyopelekea Mataifa mbali mbali Duniani kuleta watendaji wao kuja kujifunza kutokana na hatua iliyofikiwa na Zanzibar.
Aliwashauri Wananchi na Viongozi hao pamoja na wale wa Majimbo mengine kuendelea kubuni Miradi ya Ujenzi na kuianzisha kwa hatua ya msingi na Viongozi pamoja na Serikali itakuwa tayari kuunga mkono Miradi hiyo kwa maendeleo ya Jamii.
Akitoa maelezo kuhusiana na utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf } Mkurugenzi Uratibu Shughuli za Serikali SMT na SMZ Nd. Khalid Bakar Amrani alisema kupitia mradi huo Zanzibar tayari imeshapunguza ukali wa Umaskini kwa asilimia 12%.
Nd. Khalid aliwaomba Wananchi kutoa Taarifa sahihi kupitia kwa Masheha wao pale wanapopelekewa Mipango inayobuniwa na kuanzishwa kwa Miradi Mipya katika maeneo yao.
Alisema wapo baadhi ya Wananchi pamoja na Shehia zilizochelewa kupelekewa miradi ya Mfuko wa Tasaf kutokana na sababu mbali mbali za Kimaisha, Uchumi na hata kipato ikiwemo ushirikiano mdogo baina ya Wananchi na baadhi ya Maafisa wa Mfuko huo.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Nd. Rajab Ali Rajab alisema Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mahonda imebeba Wanafunzi wengi kuliko Skuli nyengine yoyote ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.
Nd. Rajab alisema upo umuhimu wa kujengewa mazingira bora zaidi ya kuongezewa huduma za Madarasa Wanafunzi wake kwa lengo la kupunguza  uhaba wa madarasa.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” aliishukuru Serikali Kuu kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa uamuzi wake wa Kujenga Skuli Mbili za Ghorofa ndani ya Wilaya hiyo katika Skuli za Mahonda na Kitope na kuifanya Wilaya hiyo kuwa na Skuli 3 za Ghorofa ikitanguliwa na ile ya Donge.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.