Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Ali Mohamed Shein, akijumuika na Wananchi wa Mkoa wa Kaskazi Pembe katika Futari Maalum aliyowaandalia katika Viwanja vya Ikulu Ndogo Micheweni Pemba kushoto Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi na kulia Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Omar Khamis Othman.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na kuwataka
kuendeleza ibada na kufanya mambo ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu.
Hafla hiyo ya futari iliandaliwa
na Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba ilifanyika katika
Ikulu ndogo Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali
mbali wa dini, vyama vya siasa, Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa huo.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya Rais, Mkuu wa Mkoa huo Omar Khamis Othman alieleza kuwa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani ni kipindi cha kufanya ibada sambamba na kufanya mambo
Mwenyezi Mungu ameamrisha ili kupata rehma za Ramadhani.
Alieleza kuwa wananchi
na waumini wote wa Dini ya Kiislamu wanapaswa kufanya vitendo vyema hasa
ikizingatiwa Zanzibar ni nchi yenye amani na utulivu mkubwa.
Alisistiza kuwa
maendeleo makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar yametokana na amani, utulivu na
upendo sambamba na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein.
Aliongeza kuwa kukutana
kwao katika hafla hiyo kumetokana na amani, utulivu na upendo mkubwa uliopo
hapa nchini na kusisitiza haja ya kuendeleza hata baada ya kumalizika kwa mwezi
wa Ramadhani ili Zanzibar iendelee kupata neema.
Aidha, aliwasisitiza
wananchi kuendelea kuzitumia vyema mvua za masika kwa kuimarisha na kuendeleza
sekta ya kilimo kwani ndio uti wa mgongo wa taifa hili.
Alieleza kuwa mvua
zinazoendelea ni vyema wakulima wakazidisha juhudi kwa kupanda miti ya kudumu
ili waweze kufaidika wao pamoja na vizazi vijavyo huku akisisitiza haja ya
kuimarisha kilimo cha mpunga kwani ndio chakula kinachopendwa zaidi hapa
nchini.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuridhishwa na juhudi kubwa zinazochukuliwa na wakulima
katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini na kueleza kuwa Serikali
itaendelea kuwaunga mkono ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.
Alhaj Dk. Shein
aliwatakia Ramadhani njema wananchi wa Mkoa huo na kuwataka kumaliza salama funga
yao ya mwezi mtukufu wa Ramadhan ili hatimae kusherehekea vyema Sikukuu ya Idd el
Fitri kwa salama na amani.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote waliohudhuria katika futari hiyo aliyowaandalia
na kupongeza jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwake kwa kukubali muwaliko wake
huo.
Mkuu wa Mkoa huo pia, litumia
fursa hiyo kutoa shukurani kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo na kutoa pongezi
zake kwa Alhaj Dk. Shein kwa kufutari pamoja na wananchi wa Mkoa huo katika
eneo hilo la Micheweni na kueleza jinsi wananchi hao walivyofurahi kuona jinsi
Rais wao alivyokuwa karibu nao.
Aidha, wananchi hao walitumia
fursa hiyo kumuombea dua Rais Dk. Shein kwa ukarimu na upendo wake mkubwa aliyowaonesha
pamoja na ukarimu anaoendelea kuwaonesha wananchi wote wa Zanzibar katika
kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na katika kipindi chote cha
uongozi wake.
Nae Ustadh Omar Hamad
alitumia fursa hiyo kusoma dua na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuleta neema
na baraka katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Wakati huohuo, nae Mama Mwanamwema
Shein kwa upande wake aliungana pamoja na viongozi wanawake wa kitaifa wa Mkoa
huo pamoja na wananchi katika futari hiyo maalum aliyoianda Rais Dk. Shein.
Leo Alhaj Dk. Shein
anatarajiwa kuungana pamoja katika futari maalum aliyowaandalia wananchi wa kijiji
cha Mkanyageni Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment