RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameongoza mazishi ya Marehemu Ali Ferej Tamim huko katika
Makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Unguja na
kuungana na ndugu, jamaa,marafiki pamoja na wanamichezo mbali mbali walioshiriki
mazishi hayo.
Marehemu Ali Fereji Tamim
ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa Chama Cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kwa zaidi ya
miaka 20 na kukiongoza chama hicho katika nyadhifa mbali mbali ikiwemo Urais wa
Chama hicho.
Aidha, Marehemu Ali
Ferej Tamim ambaye ni mmoja wa wanamichezo waliotoa mchango mkubwa katika mpira
wa miguu hususan Zanzibar pia, aliwahi kushika wadhifa wa kuwa Makamo wa Rais
wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa muda mrefu.
Sambamba na hayo,
Marehemu Ali Ferej Tamim alichukua juhudi kubwa katika uongozi wake katika
kuhakikisha Zanzibar inapatiwa uwanachama wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF)
pamoja na kuhakikisha ligi kuu ya Zanzibar inapata udhamini na kuvipa nafasi
vilabu vidogo vidogo.
Ali Ferej Tamim
amefariki dunia leo alfajiri katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar
baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu ambapo Marehemu Ali Ferej
ameacha kizuka mmoja na watoto wawili.
No comments:
Post a Comment