Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Metuma Salamu za Rambirambi Kwa Familia na Ndugu wa Dr. Mengi.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa IPP Media kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Abraham Mengi.

Kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Abraham Mengi kilitokea alfajiri ya kuamkia Alhamis ya Mei 2, 2019 akiwa mjini Dubai Falme za Kiarabu (UAE).

Rais Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Dk. Mengi na kueleza kuwa yeye binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla wamejawa na simanzi nzito kufuatia msiba huo mkubwa wa kitaifa.

“Kwa hakika msiba huu umetugusa Watanzania sote, ni msiba wetu kwa sababu aliefariki ni ndugu yetu, mwenzetu, mfanyabiashara, mwekezaji mzalendo na aliyekuwa akiwajali wanyonge wakiwemo wananchi wa rika zote pamoja na watu wenye ulemavu, wanamichezo na wapenda mazingira”,ilieleza sehemu ya salamu za rambirambi alizozituma Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa vile kifo ndio mwisho wa uhai wa mwanaadamu alimuomba Mwenyezi Mungu aijaalie roho ya marehemu Dk. Reginald Mengi alilaze mahala salama.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu, jamaa, wafanyakazi wa IPP Media na marafiki wa marehemu katika msiba huo mzito.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimuomba Mwenyezi Mungu awape Watanzania wote na wanafamilia nyoyo za subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Katika salamu hizo za rambi rambi Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatomsahau Marehemu Dk. Reginald Abraham Mengi kwa juhudi zake kubwa katika suala zima la uhifadhi wa mazingira ambaye aliweza kushirikiana nae kwa kiasi kikubwa wakati  Rais Dk. Shein akiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Dk. Mengi akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC).

Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu Dk. Reginald Abraham Mengi ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kuanzia mwaka 2008 hadi 2009 alihamasisha Maendeleo ya Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuchangia ukuaji wa sekta binafsi kuendana na soko la pamoja kwa nchi wanachama.

Marehemu Dk. Mengi pia, atakumbukwa kwa juhudi zake kubwa katika kuiimarisha tasnia ya Habari katika nchi za Afrika Mashariki ambapo vile vile aliweza kuanzisha tunzo za waandishi wa habari katika nchi za (EAC) kwa ajili ya kuhamasisha ari ya uandishi wa kujenga uhusiano mwema wa (EAC).

Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu Dk. Mengi atakumbukwa kwa uzalendo wake wa kuipenda nchi yake pamoja na wananchi wake hasa katika kuimarisha michezo ambapo hadi mauti yanamfika alikuwa  Mlezi wa Timu ya Taifa ya Vijana U17 “Serengeti Boys”.

Dk. Reginald Abraham Mengi alizaliwa katika kijiji cha Nkuu huko Machame, Kilimanjaro, Tanzania mnamo mwaka 1942 ambaye amefariki alfajiri ya kuamkia Alhamis ya tarehe 2, Mei 2019 akiwa mjini Dubai Falme za Kiarabu (UAE).

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.