Habari za Punde

Serikali ya CCM Ikitekeleza Vyema Ilani ya Uchaguzi Kwa Asilimia Kubwa.

Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh.  Mihayo Juma N’hunga akifungua Semina maalum kwa Wenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya pamoja na maafisa wa CCM kutoka Afisi Kuu iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar Rais Vuga Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani Nd. Hussein Mjema Kimti akichangia kwenye Semina maalum kwa Wenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya pamoja na maafisa wa CCM kutoka Afisi Kuu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Nd. Abdulazizi Hamad Ibrahim akichangia kwenye Semina maalum kwa Wenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya pamoja na maafisa wa CCM kutoka Afisi Kuu.(Picha na Kassim Abdi Salum.OMPR.)
Na. Rashida Abdi Khalfan. OMPR. 
Naibu Waziri Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga amesema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wana Wajibu wa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020 inayotekelezwa na Serikali Kuu.
Mhe.Mihayo amesema kufanya hivyo kutasaidia kuwaeleza na kuwafahamisha wananchi juu ya mambo mazuri yanayoendelea kutekelezwa na Serikali yao ikiwemo kuimarika kwa uchumi.
Mh.  Mihayo Juma N’hunga ameeleza hayo wakati akifungua Semina maalum kwa Wenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya pamoja na maafisa wa CCM kutoka Afisi Kuu iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Zanzibar Rais Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali inayoongozwa na Dr.Ali Mohamed Shein imekuwa ikitekeleza vyema ilani ya uchaguzi kwa asilimia kubwa,sambamba na kutekeleza ahadi ambazo nyengine hazijatajwa ndani ya  ilani akitolea mfano Utekelezaji wa Ujenzi wa Daraja la Kibonde Mzungu na Mwanakwerekwe sehemu ambazo zilikuwa na Changamoto hasa katika msimu wa Mvua kubwa.
Alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kama msimamizi na utekelezaji wa Shughuli za Serikali itaendelea kutoa taarifa zinazohusiana na mambo mbali mbali yaliotekelezwa na Serikali kama yalivyoahidiwa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alisema  lengo ni kuwafahamisha viongozi wa Chama ili na wao waweze kuyawasilisha kwa wananchi wa kawaida katika azma ya kuwajengea mazuri yanayofanywa na Serikali yao.
Mhe .Mihayo alisema kuwa kutokana na usimamizi mzuri wa Serikali unaofanywa na Mhe.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hakuna budi kila Kiongozi wa CCM kwa mujibu wa nafasi alionayo kuunga mkono jitihada hizo.
Akiwasilisha mada kupitia kikao hicho Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali Ndugu Khalid Bakari Hamrani,alisema Ofisi ya Makamu wa Pili imekua ikijitahidi kutoa taarifa kwa viongozi na watendaji wa Chama kwa lengo la kuyaweka bayana mambo mema na mazuri yaliyofanywa na Serikali.
Mkurugenzi Khalid alisema hali ya Uchumi wa Zanzibar imekua ikiimarika kwa Kasi kwa Wastani wa asilimia 7%, ambapo kipato cha Mwananchi kimeongezeka ukilinganishwa na miaka ya nyuma.
Pamoja na mambo mengine Mkurugenzi Khalid alisema kutokana na kuimarishwa kwa suala zima la Ulinzi kwa kufungwa kwa CCTV Kamera katika Mji wa Zanzibar hali ya Amani na Utulivu inaendelea kuwepo jambo ambalo limepelekea kuimarika kwa Sekta ya Utalii inayoiingizia Serikali mapato na kutatua Changamoto za Wananchi wake.
Akizungumzia Sekta ya Kilimo alisema kupitia mradi wa TASAF ambao umetoa fursa kwa wananchi kubuni mambo mbali mbali  yenye tija na mafanikio makubwa yamepatikana kwa  Wakulima kutokana na Wakulima hao kulima kwa kutumia njia bora zinazowawezesha kulima katika eneo dogo lakini hupata mazao mengi.
Alisema kupitia Sekta hiyo hiyo ya Kilimo Serikali imejitahidi kuimarisha Miundombinu ya Kilimo kwa Kurahisishia kwa kutumia vifaa vya Kisasa, sambamba na Sekta ya Uvuvi.
Aidha, Mkurugenzi Khalid amesema Zanzibar imepiga Hatua katika suala la ukuaji wa Demokrasia na Utawala Bora akitolea mfano Kitengo Cha Rais wa Zanzibar kutia Saini Mkataba wa Utafutaji na Uchimbaji wa Gesi na Mafuta, kitendo  ambacho dunia nzima kimeshuhudia kikifanywa kwa Uwazi na Kushuhudiwa na kila mmoja.
Kwa upande wa Washiriki wa Semina hiyo wameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa jitihada zake nzuri za Kukusanya pamoja utekelezaji wa ahadi zilizoahidiwa na Chama kupitia Ilani ya Uchaguzi 2015-2020.
Wajumbe wa Semina hiyo wameiomba Serikali Kuimarisha Mtaala wa Elimu kupitia Utalii,ili uweze kutoa fursa zaid za ajira kwa vijana wake,nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Abdul-azizi Hamad Ibrahim,amesema anasikitishwa na vitendo vya baadhi ya viongozi na watendaji walipewa dhamana mbalimbali kumuangusha Mhe.Rais kwa Kutowajibika vyema katika Majukumu yao.
Akifunga Semina Hiyo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Raisi ndugu Abdalla Hassan Mitawi,kwa kuwapongeza washiriki wa semina hiyo na kuwataarifu kuwa Serikali bado inaendelea kuipatia ufumbuzi Miradi iliyokwama ikiwemo mradi wa Viwanja vya Ndege Taminal 2,na ujenzi wa bandari ya Mpiga Duri.
Semina hiyo ya Siku moja imewakutanisha viongozi wa Chama wa Wilaya na Jumuiya na jumla ya mada tatu zimewasilishwa nazo ni Kiongozi Bora ,Serikali imetekeleza nini katika taarifa ya Ilani ya Utekelezaji kwa miaka 3(2015-2018), na Taarifa fupi ya Mradi wa Tasaf.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.