Habari za Punde

Benki ya Afrika Tawi la Zanzibar Yafutarisha Wananchi na Wateja Wao Katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Afria Bwana Wasia Mushi kushoto yake kuelekea kwenye futari ya pamoja iliyoandalia na Benki hiyo katika Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni.
Balozi Seif akisalimiana na Naibu Waziri Kiongozi Mstaafu wa SMZ MH. Omar Ramadhan Mapuri ambae ni Mteja wa Benki ya Afrika kabla ya kuanza kwa Futari ya pamoja.
Balozi Seif akijumika na Watu mbali mbali katika Futari ya pamoja pamoja iliyoandalia na Benki hiyo katika Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akijumuika na Watu mbali mbali katika Futari ya pamoja pamoja iliyoandalia na Benki hiyo katika Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni.
Washiriki wa Futari ya pamoja kutoka maeneo mbali mbali waliojumuishwa na Uongozi wa Benki ya Afrika iliyofanyika katika Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni.
Meneja wa Benki ya Afrika Tawi la Zanzibar Bwana Juma Burhan akitoa maelezo ya ufanisi wa majukumu ya  Taasisi hiyo ya Fedha.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Afrika { BOA} Bwana Wasia Mushi akiipongeza SMZ na Wananchi wa Zanzibar kwa kuipokea vyema Benki hiyo tokea ilipoanza kutoka huduma Visiwani Miaka Mitatu iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Afrika { BOA} Bwana Wasia Mushi wakiteta wakati wa Futari ya pamoja hapo Hoteli ya Madinatul Bahr Mbweni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha ya watedaji wa Taasisi za huduma za Fedha kuzingatia uadilifu katika majukumu yao ya kila siku.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema umainifu mkubwa unaowajibika kutekelezwa na Watendaji wa Taasisi zote zinazosimamia  masuala ya Fedha mahali popote pale ndio jambo la msingi linaloshajiisha Jamii kujenga imani ya kuwekeza mitaji yao kwenye Taasisi hizo.
Alisema udokoaji wa mitaji ya wateja ambayo wakati mwengine hufanywa na watendaji wasio waaminifu hupelekea baadhi ya Taasisi hizo kulazimika kufungwa na Mamlaka za Serikali zinazosimamia taasisi hizo baada ya kufilisika.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo mara baada ya Futari ya pamoja iliyoandaliwa na Uongozi wa Benki ya Afrika {BOA} iliyowashirikisha Wateja, Viongozi na Wananchi tofauti na kufanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Madinatul Bahr iliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema uaminifu ni silaha kubwa na ya msingi inayoleta msukumo wa kujenga Imani thabiti baina ya Wateja na Taasisi zinayosimamia na kutunza Mitaji yao jambo linalopaswa kuzingatiwa kwa uadilifu uliotukuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi na Watendaji wa Benki ya Afrika {BOA} kwa kufanyakazi kwa uadilifu uliopelekea Tawi la Benki hiyo liliopo Zanzibar kuongoza katika utoaji wa huduma za Kibenki ikilinganishwa na Matawi mengine ya Benki hiyo yaliyopo Tanzania.
Alisema uadilifu huo umemtia moyo na kushawishika kuwa tayari kufungua Akaunti ndani ya Benki hiyo na kuwashawishi Wananchi pamoja na Watumishi wa Taasisi za umma kuitumia fursa hiyo adhimu kwa maslahi yao ya sasa na hapo baadae.
Balozi Seif aliuhakikishia Uongozi wa Benki ya Afrika kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari muda wowote kutoa msaada katika kuona malengo ya Benki hiyo yanafanikiwa kama yalivyopangwa.
Akizungumzia ucha mungu uliokuwa ukitekelezwa na kuzingatiwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa kuendelezwa yale yote mazuri  katika Miezi ijayo ambayo  yalifanywa katika kipindi hicho.
Alisema haitapendeza hata kidogo na ni dhambi kwa Waumini hao kuwa na tabia yaWanyama wanaofungiwa kwenye zizi wanapoachiliwa ikawa balaa inayoenea mitaani na kuleta mtafaruku katika Jamii.
Mapema Meneja wa Benki ya Afrika Tawi la Zanzibar Bwana Juma Burhan alisema Taasisi hiyo ya Fedha imefanya mambo makubwa tokea kuanzishwa kwake Zanzibar Miaka Mitatu iliyopita kutokana na kuungwa mkono na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wananchi mbali mbali.
Bwana Juma alisema kipindi hicho cha miaka Mitatu kimeiwezesha Benki hiyo kusaini Mkataba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Watumishi wa Wizara 10 za SMZ.
Alisema mikopo hiyo iliyohusisha miradi tofauti ya kuwaongezea uwezo wa kipato cha kukimu Maisha Watumish hao pia ilizihusisha Taasisi Saba Binafsi zinazotoa huduma Visiwani Zanzibar.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Afrika { BOA} Bwana Wasia Mushi alieleza kwamba Zanzibar imejionyesha katika ramani ya Dunia kukua kwa haraka Uchumi wake jambo ambalo Taasisi za Kifedha zina kila sababu ya kuwekeza miradi yao katika kutoa huduma za haraka kwa wateja.
Bwana Mushi alisema ufanisi wa huduma za Fedha kama ulivyopatikana kwa Tawi la Benki yao hapa Zanzibar kuongoza kwa huduma zake ikilinganishwa na Matawi 16 yaliyopo Nchini Tanzania ni jambo la msingi katika Maendeleo ya Taifa na Wananchi wake.
Alisema Benki hiyo ya Kimataifa iliyopata mafanikio makubwa tokea kuasisiwa kwake Nchini Morocco hivi sasa imeshakuwa na Matawi 18 pekee ndani ya Bara la Afrika, Marekani, China wakati Nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki zikisheheni Matawi ya Benki hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.