Habari za Punde

Mama Asha afungua Baraza la Jumuia ya Wazazi wa CCM Mfenesini

 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akisindikizwa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Zanzibar Nd. Othman Ali Maulid kuingia katika Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kufungua Baraza Kuu la Jumuiya hiyo Wilaya ya Mfenesini.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akilifungua baraza la Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mfenesini.
 Baadhi ya Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini na Mikoa wa Magharibi na Mjini wakifuatilia ufunguzi wa baraza la Jumuiya ya Wazazi wa CCM Wilaya ya Mfenesini.
 Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini Bibi Biubwa Jabiri akitoa Taarifa fupi ya utekelezaji wa kazi ndani ya kipindi cha Miezi Sita.
 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya Wazazi Zanzibar Nd. Othman Ali Maulid akitoa salamu wakati akimkaribisha Mgeni rasmi kuufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini.
Mama Asha akimkabidhi mchango wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini Bibi Biubwa Jabiri mara baada ya kuufungua Mkutano wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Bububu.
Picha na – OMPR – ZNZ.

NA Othman Khamis, OMPR
Wazazi wanapaswa kutambua kuwa bado wataendelea kuwa na jukumu la  kuzaa na kulea suala ambalo kwa wakati huu wengi kati yao hujisahau hasa katika ule mfumo wa asili wa malezi ya pamoja na badala yake kila Mzazi huamua kulea Mtoto wake pekee.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kauli hiyo wakati akilifungua Baraza la Wazazi  la Chama cha Mapinduzi la Wilaya ya Mfenesini linalofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere uliopo Bububu  nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mama Asha alisema hali ya ukosefu wa malezi ya pamoja kwa Watoto imepelekea kuporomoka kwa maadili ya Watoto walio wengi katika Jamii na matokeo yake wanashindwa kuwaheshimu Wazazi wa wenzao wakiona wa kwao  ndio wanaostahiki kupata Heshima hiyo.
Alisema Watoto wa sasa wameacha maisha mazuri yanayoongozwa na Utamaduni wa Taifa na kuamua kufuata mila na Tamaduni za Ughaibuni jambo ambalo limechangia kuporomoka kwa Maadili hasa wakiangaliwa Watoto wenyewe  vivazi  na mienendo yao tayari imeshapoteza hadhi ya Utamaduni wa asili.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea masikitiko yake  kutokana na vitendo vya udhalilishaji vilivyoshamiri katika mitaa mbali mbali Nchini ambavyo kwa mtazamo wa matukio hayo, maadili tayari yameshapoteza muelekeo kutokana na jamii ya sasa kukosea njia sahihi ya kuelekea.
Mama Asha alisema tabia ya kupigwa kwa Wanawake na Watoto hadi kuumizwa na wakati mwengine kuchomwa moto Watoto kwa makosa madogo madogo pamoja na kutelekezwa ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya udhalilishaji wa makundi hayo.
Alieleza kwamba ni ukweli usiofichika kwamba wanaoendeleza vitendo hivyo ambavyo ni vya kinyama na aibu kwa Jamii yenye kufuata mila, silka, desturi na Utamaduni wa Watu wastaarabu ni wale waliokosa malezi ingawa wanaelewa fika ubaya wanaoufanya.
Mama Asha aliwataka Wazazi na Viongozi wa ngazi na nyanja zote pamoja na Wananchi wote kuchukuwa tahadhari kwa kuwa karibu na familia zao ili kila mmoja kwa nafasi yake ailinde Jamii kwa kukemea vitendo hivyo viovu vyenye kutia aibu.
Aliwakumbusha Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kwamba bado wana jukumu kubwa la kutoa elimu, kusimamia malezi bora ya Watoto na kuhakikisha kwamba mazingira ya Mitaa yanaimarika ipasavyo ili kuwa na Jamii yenye ustawi na umakini mkubwa.
Akigusia janga la Dawa za kulevya Nchini ambalo huwakumba zaidi Vijana wanaotarajiwa kuwa Viongozi wa Taifa la kesho Mama Asha alisema jamii bado inapaswa kukemea utumiaji wa Dawa hizo ambazo ni janga linaloendelea kuikumba Dunia na hatimae kuathiri Mataifa mengi Ulimwenguni.
Mama Asha aliwanasihi Wananchi kwa kushirikiana na Viongozi wao ni vyema wakashiriki kikamilivu katika mapambano dhidi ya kupiga vita vitendo hivyo kwa kuwafichua wahalifu wanaoingiza, kusambaza na watumiaji kwa vile madhara yake huwagusa hata wale wasiohusika kwa kukumbwa na vitendo vya ajabu.
Alizikumbusha Taasisi zinazohusika na udhibiti wa Dawa za kulevya kuendelea kuimarisha mashirikiano na Serikali pamoja na wadau wengine wa Kitaifa na kimataifa ili kuona wimbi hili la Dawa za hatari linakomeshwa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Mama Asha alishauri katika kukabiliana na janga hilo ni budi kuanzishwa kwa vituo vya Maandalizi katika kila Tawi la Chama cha Mapinduzi, kuimarisha Vijana kuwa Chipukizi na kuendeleza madarasa ya Itikadi ya Jumuiya ili kulea, kusimamia na kuwafundisha Vijana Maadili mema ya Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake.
Akigusia masuala ya uchumi ndani ya Jumuiya Mama Asha aliutaka Uongozi wa Jumuiya hiyo ya Wazazi kuhakikisha kwamba Wawekezaji wanaoshirikiana nao wanazingatia Maadili, Heshima na Uzalendo wa Taifa.
Alisema wapo baadhi ya Viongozi hudiriki kuiua Miradi ya Uwekezaji kwa sababu ya kukoza asilimia Kumi ya Mradi jambo ambalo ni miongoni mwa vitendo vya Ruishwa vinavyodumaza maendeleo ya Jumuiya pamoja na Taifa kwa Ujumla.
Aliwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wazazi la Wilaya ya Mfenesini kwa umahiri wao wa kutekeleza Kanuni ya Jumuiya yao Kifungu cha 60{2} kinachotaka kufanyika Vikao kila miezi Sita ili Wajumbe wapate fursa ya kujadili masuala yao yenye mustakabal na Jumuiya pamoja na Chama chenyewe.
Alisema kwa vile Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi ni kongwe  iliyoasisiwa mnamo Mwaka 1955 tokea wakati wa enzi za Vyama vya TANU na ASP ikiwa ni miongoni mwa mihimili ya Ukombozi lazima ienziwe, itunzwe na kuthaminiwa ili iendelee kulea na kupata maendeleo mema yatakayokikidhi ustawi na maeneleo ya Jamii yote Nchini.
Akitoaa Taarifa fupi ya Utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini, Katibu wa Jumuiya Hiyo Bibi Biubwa Jabir alisema  yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kazi za Jumuiya hiyo ndani ya kipindi cha Miezi Sita iliyopita.
Bibi Biubwa alisema Viongozi wa Jumuiya hiyo bado wanaendelea kusimamia Jukumu lao la kuwajenga Vijana katika muelekeo wa kukua kimaadili wakizingatia kwamba Elimu ndio msingi imara wa kufanikisha majukumu hayo muhimu kwa Taifa.
Alisema kazi iliyopo mbele ya Viongozi hao ni kuunganisha nguvu katika kuhamasisha  Wazazi waelekeze juhudi zao kwenye Utekelezaji wa Sera na Malezi bora kwa Watoto ili kuwa na Jamii iliyostawi Kimaadili.
Hata hivyo Katibu huyo wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mfenesini alisema zipo changamoto zinazokwaza ufanisi wa kazi wa Jumuiya akizitaja baadhi kuwa ni pamoja na ukosefu wa Fotokopi, Mashine, Fedha kwa ajili ya kuanzisha Mradi wa Ufugaji Nyuki, ushakavu wa Mabweni wa Skuli ya Wazazi Dole inayokwenda sambamba na ukosefu wa Gari kwa ajili ya Wanafunzi.
Naye kwa upande wake akitoa salamu Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Zanzibar Nd. Othman Ali Maulid alisema kuanzia sasa Kiongozi au Mdau ye yote anayeamua kuchangia au kusaidia shughuli za Chama na Jumuia zake lazima kuwepo kumbu kumbu kamili.
Nd. Othman alisema hatua hii ina lenga kujiepusha na vitendo vya Rushwa wakati Taifa likikaribia kuelekea katika Chaguzi za Serikali za Mitaa kwa upnade wa Tanzania Bara na Uchaguzi Mkuu Mwaka ujao.
Alisema wapo Watu wakiwemo baadhi ya Viongozi  wanaoutumia udhaifu wa baadhi ya changamoto zinazokuwepo Kwenye Taasisi za Chama  kwa kutoa Misaada kwa muekeo wa kujinyooshea njia ya kupata madaraka na baadae kujinufaisha kibinafsi.
Mkutano huo wa Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi {CCM} Wilaya ya Mfenesini umejadili Utekelezaji wa Majukumu yake ndani ya Kipindi cha Miezi Sita iliyopita na kupanga Mikakati ya Utekelezaji kwa Kipindi chengine cha Miezi Sita Ijayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.