Habari za Punde

Ndege iliyotengenezwa na Wanafunzi yatua Zanzibar ikielekea Misri


Wanafunzi wa Afrika Kusini ambao wanaendesha ndege ndogo kutoka nchini Afrika Kusini kwenda Misri imetua Zanzibar.


Safari hiyo ya kutumia ndege aina ya Sling 4 inaendeshwa kwa zamu na marubani sita, na hakuna hata mmoja kati yao aliyefikisha miaka 20.

Walianza safari yao Juni 15 na wanapanga kusafiri kwa kilomita 12,000 kufika Misri ndani ya wiki sita.

Wazo la safari hiyo lilibuniwa na rubani msichana wa miaka 17 Megan Werner, ambaye baba yake pia ni rubani na anasimamia safari hiyo.

Mpaka sasa bwana Werner anasema changamoto kubwa walizokumbana nazo ni kutua na kupaa kutoka kwenye kiwanja cha ndege kidogo cha kisiwa cha Likoma nchini Malawi.


Kutengeza radio na mifumo ya rada ya ndege hiyo jijini Windhoek, Namibia pamoja na ukosefu wa mafuta na bidhaa nyengine muhimu kama mkate katika maduka kwenye eneo mashuhuri la Maporomoko ya Mto Zambezi (Victoria Falls) nchini Zimbabwe.

Bw Werner, anasafari ndani ya ndege nyengine ndogo ambayo ni ya huduma za msaada anasema timu ya marubani hao wanafunzi inaendelea vizuri na hali ya hewa ni nzuri kwao.

Kundi la wanafunzi 20 kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Kusini waliitengeneza ndege hiyo kwa muda wa wiki tatu baada ya kununua vifaa kutoka kampuni ya nchi hiyo.

Wakitoka Zanzibar, msafara huo utatua Arusha, Nairobi, mji wa Lalibela Ethiopia, kisha Asmara, Djibouti na hatimaye Misri.

Katika safari ya kurudi, watatumia njia tofauti na watasimama katika nchi za Uganda, Rwanda, Zambia na Botswana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.