RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ameongoza hitma ya kumuombea Dk. Badriya
Abubakar Gurnal mke wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma
Sadala (Mabodi) iliyofanyika katika msikiti
Maamur Upanga jijini Dar-es-Salaam.
Katika hitma hiyo, iliyohitimishwa na Sheikh Zain Sharif
na dua yake kutolewa na Sheikh Ayoub Ali Seif wote wa msikiti Maamur, viongozi
mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali walihudhuria pamoja na wana familia
wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki.
Baada ya hitma hiyo, akitoa neno la shukurani kwa niaba
ya familia mjomba wa Marehemu alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein kwa ushiriki wake
na kuungana pamoja na wanafamilia hao katika kisomo hicho.
Aidha, alitoa shukurani kwa wote waliohudhuria hitma hiyo
na kutumia fursa hiyo kumuelezea Marehemu jinsi alvyokuwa mtu mwema, mwenye
hikma na hulka aliyekuwa akifuata maadili ya Kiislamu sambamba na maadili ya
kazi yake ya Udaktari.
Mapema Alhaj Dk. Shein akiwa na Mama Mwanamwema Shein
walifika nyumbani kwao Marehemu Mikocheni jijini Dar-es-Salaam kwa ajili ya
kutoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa watoto pamoja na mume wa Marehemu Dk. Badriya.
Akiwa nyumbani kwao Marehemu Rais Dk. Shein na Mama
Mwanamwema Shein walitia saini kitabu cha Maombolezi kufuatia kifo cha Marehemu
Badriya Gurnal.
Baada ya tukio hilo Rais Dk. Shein pamoja na Mama
Mwanamwema Shein walitoa mkono wao wa pole huku Rais Dk. Shein akiwaomba wana
familia wakiwemo ndugu, jamaa, watoto pamoja na mume wa marehemu kuwa na moyo
wa subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza jinsi
alivyomfahamu Dk. Badriya katika maisha yake yote pamoja na utendaji wake wa
kazi uliotukuka tokea Rais Dk. Shein akiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya
ambapo pia, aliwaomba wanafamilia kuzidi kuendelea kumuombea dua Marehemu.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma
Mabodi ambaye pia ni Mume wa Marehemu alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa
kuwa karibu na familia hiyo tokea uhai wa marehemu, ugonjwa wake pamoja na
hatua yake hiyo ya kwenda kuwafariji kwa kwuapa pole.
Dk. Mabodi alimshukuru Rais Dk. Shein kwa msaada wake
mkubwa kwa familia hiyo na jinsi alivyokuwa karibu na Marehemu katika kipindi
chake chote katika uhai wake na katika utendaji wake wa kazi.
Mara baada ya kutoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa,
watoto na mume wa Marehemu Mama Mwanamwema Shein aliungana pamoja na akina mama
wengine wakiwemo wakiwemo wanafamilia pamoja na viongozi mbali mbali katika
hitma ya wanawake ya kumuombea Marehemu Badriya.
Hitma hyo iliyoongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ilifanyika nyumbani kwao Marehemu
Badriya Mikocheni jijini Dar-es-Salaam.
Maziko ya Marehemu Dk. Badriya Abubakar Gurnal mke wa
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar yalifanyika Juni 23, 2019 huko katika
makaburi ya Kisutu jijini Dar-es-Salaam.
Marehemu Dk. Badriya alikuwa mfanyakazi wa Benki kuu ya
Tanzania (BOT) ambaye alifariki Jumaamosi Juni 22 2019 katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa
muda mfupi.
Marehemu Badriya Abubakar Gurnal ameacha mume na watoto
watatu, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amin.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment