Habari za Punde

TANZANIA KUTUMIA ZOEZI LA KUPIMA UTAYARI WA KUKABILI MAGONJWA YA MLIPUKO MIPAKANI, KUCHAGIZA UTEKELEZAJI WA DHANA YA AFYA MOJA NCHINI.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza umuhimu wa Sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya moja, wakati  akifungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani,  leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga.
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akitoa hotuba wakati wa  mkutano wa kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (Watu wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa, akitoa hotuba wakati wa  mkutano wa kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto wakifuatilia mkutano wa kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani,  leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga,

 

Mratibu wa  Dawati la Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka (wa kwanza kulia) akiwa katika chumba maalum cha Menejimenti ya Taarifa za zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani,  leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga. 
Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri  Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, akisalimiana na baadhi ya wafugaji walioshiriki katika mkutano wa  kufungua  zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani,  leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Kufuatia nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, Tanzania kwa kushirikiana na Kenya wameanza kutekeleza zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, lilofunguliwa leo  mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu.

Zoezi hilo, linazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla ya washiriki 150 ambao wanatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.

Akiongea leo tarehe 11 Juni, 2019, wakati wa Kufungua rasmi zoezi hilo  la siku nne, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga,  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amefafanua kuwa, serikali kupitia Wizara hiyo inatumia zoezi  hilo kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya magonjwa ya mlipuko.

“Hapa nchini Tanzania tunalo Dawati la Kuratibu masuala ya Afya Moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Dawati hilo sisi kama wizara ya Afya tunasubiri tu ripoti ya zoezi hili na tutaitekeleza mara moja. Utekelezaji wa ripoti hiyo tutahakikisha unakuwa wa ufanisi na tija kwa nchi ili tuweze kusaidia kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya hapa nchini  kwa kuzingatia dhana ya  Afya moja.” Amesisitiza Waziri  Ummy.

Aidha, Waziri Ummy, ameongeza kuwa zoezi hilo linalenga kutathmini utaratibu wa kutumia kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini pia  kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika, kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana  na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi hiyo, itaendelea kuratibu sekta zote za Afya nchini kwa kutumia Dhana ya Afya moja,  ili kuhakikisha Afya za wananchi zinakuwa imara na salama kwa kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababisha maafa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina, amebainisha kuwa,  kwa kutambua umuhimu wa Dhana ya Afya moja, Wizara inafahamu kuwa mifugo huwa ni chanzo cha  vimelea  vya magonjwa ambayo huambukizwa binadamu, hivyo serikali imeendelea kuboresha maabara za Mifugo nchini ili kuweza kutambua vimelea kwa haraka na wakati ili visisababishe magonjwa ya mlipuko kwa  binadamu.

Naye, Waziri wa Afya wa Kenya, Mhe. Sicily Kariuki, amebainisha kuwa zoezi hilo ambalo linahusisha  mlipuko wa virusi vinavyo shabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya, kwa kuwa  washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwakuzingatia Dhana ya  Afya Moja.

Zoezi hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga. 

Zoezi hilo ambalo linafanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, linaratibiwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.


IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILINO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.