Habari za Punde

Waumini wa Dini ya Kiislam Watakiwa Kudumisha Upendo Mshikamano Ili Kuimarisha Dini.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Issa Haji Gavu. akizungumza na kutowa shukrani kwa Wananchi waliohudhuria hafla ya futari ilioandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu nchini kuendeleza upendo na mshikamano, ili kuimarisha dini hiyo pamoja na kupata fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Dk. Shein amesema hayo katika viwanja vya Ikulu mjini hapa baada ya kukamilika hafla ya futari, aliyoiandaa kwa wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba yake, Waziri wa Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu alisema mshikamano na upendo miongoni mwa waumini huleta maelewano na kuwa chachu katika uimarishaji wa dini hiyo.

Alisema hatua hiyo hufanikisha dhamira ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, na hivyo waumini kupata fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Alisema utaratibu  wa kila mwaka wa Rais Dk. Shein wa kujumuika pamoja na wananchi katika  futari una mnasaba na dhamira hiyo, hivyo akabainisha matumaini yake ya  utamaduni huo kuendelelea mwakani.

Aidha, alitowa shukurani kwa wananchi wote walioshiriki katika hafla hiyo, na kusema hatua waliyoionyesha ya kuwacha familia zao inaonyesha heshima na mapenzi  makubwa waliyonayo kwa kiongozi huyo.

Waziri Gavu aliwatakia kheri wananchi hao katika kukamilisha mfungo wa mwezi wa Ramadhani sambamba na maandalizi mema ya sikukuu ya Idd el Fitri.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.