Habari za Punde

MNEC Ndg.Amin Salimin Afunga Mafunzo ya Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu.

Na.Is-haka Omar - Zanzibar.
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Amin Salmin Amour, amewataka Vijana wa CCM wanaosoma Vyuo Vikuu Nchini kutokubali kutumiwa kisiasa na baadhi ya Viongozi wanaoweka mbele maslahi binafsi kuliko Maslahi ya Chama Cha Mapinduzi.

Rai hiyo ameitoa Wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi kwa Vijana wa Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu ya UVCCM Zanzibar, huko katika Ukumbi wa Jimbo la Jang'ombe Matarumbeta Unguja.

Alisema kuna baadhi ya Viongozi wamekuwa na tabia ya kuwatumia Vijana katika mambo yao binafsi yanayohatarisha uhai wa Chama, hivyo Vijana hao linatakiwa kuepuka kuingizwa katika makundi yasiyofaa.

Alieleza kuwa Vijana vijana endapo Watafuata miongozo na Kanuni za UVCCM na CCM wataendelea kuwa msaada mkubwa wa kuivusha CCM katika masuala mbali mbali ya Kisiasa,Kiuchumi na Kijamii.

Alisema maendeleo ya Taifa lolote Duniani yanaletwa na Vijana Wasomi na Wenye ujuzi wa Fani mbali mbali zinazochochea kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Nchi husika.

Katika maelezo yake MNEC Amin,aliwasihi Vijana hao kuwa wanatakiwa kuhamasisha Vijana wenzao waliopo Mitaani na wa Vyama vya Upinzani wajiunge na CCM ili kuongeza Jeshi la kufanikisha Ushindi wa 2020.

Ndugu Amin, akizungumzia Hafla hiyo aliwapongeza Vijana hao kwa kukubali kupewa Mafunzo hayo ya Uongozi na Itikadi kwani wamejifunza mambo mbali mbali yenye Tija yanayowajengea kujiamini katika Safari yao ya Kielimu.

"Chama Cha Mapinduzi na Serikali zake wamewaamini Vijana kwa kuwapatia fursa za Uongozi na Utendaji hivyo nanyi mnatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu ili kulinda heshima hiyo.",alisema Amin.

Aliongeza kwamba Vijana wanapopewa dhamana ya Uongozi wajitahidi kuliwakilisha Vyema kundi hilo ili kujenga Matumaini kwa Jamii.

Naye Mwenyekiti wa Idara hiyo Ndugu Masoud Shibli, amesema Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu kwa upande wa Zanzibar imekuwa ni kitovu cha kutoa Mafunzo mbali mbali kwa Vijana wake ili wawe na uthubutu wa kujiamini kwa kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa Uadilifu zaidi.

Awali awali akitoa Taarifa ya Mafunzo hayo Katibu wa Idara ya Vyuo na Vyuo vikuu William Dikson,alisema zaidi ya Vijana 300 wamepatiwa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo juu ya masuala ya Uongozi.

Kupitia hafla hiyo Vijana  wa Idara hiyo kutoka Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu mbali mbali wametunukiwa  Vyeti vya Mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.