Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Atuma Salamu Kufuatia Kifo Cha Mtoto wa Kiongozi wa Sharja, na Salamu za Pongezi Kwa Rais wa Comoro.Mhe.Azali, Rais wa Malawi Mhe.Arthur Kwa Kusherehekea Siku ya Uhuru wa Nchi Zao.


Rais Dk. Shein amemtumia salamu za rambirambi Mtawala wa  Sharjah Sheikh Sultan Bin Mohammad Al Qasimi pamoja na kuwatumia salamu za pongezi Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani na Rais  wa Malawi  Arthur Peter Mutharika kufuatia siku ya uhuru wa Mataifa hayo.

Rais Dk. Shein alituma salamu hizo kwa Mtawala wa Sharjah kufuatia kifo cha mwanawe Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi kilichotokea London, nchini Uingereza Julai 1, mwaka huu.

Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha mtoto wa kiongozi huyo na kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, wanatoa salamu zao za pole kwa familia, ndugu na wananchi wote wa Sharjah na Taifa zima za Umoja wa Falme nchi za Kiarabu kwa jumla.

Pamoja na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira familia ya Sheikh Al Qasimi wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Sheikh Khalid bin Sultan bin Mohammad Al Qasimi katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema peponi, Amin.

Aidha, Rais Dk. Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro, Azali Assoumani kwa kutimiza miaka 44 ya Uhuru wa Taifa hilo.

Kwa niaba yake binafsi, kwa niaba ya watu wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein  alitoa pongezi hizo kwa kiongozi huyo na wananchi wake wote katika Taifa hilo kwa kutimiza umri huo pamoja na kupongeza mafanikio ya kiuchumi na kijamii yanayondelea kupatikana.

Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake sambamba na kuimarisha uhusiano wa kihistoria ulipo baina ya pande mbili hizo na watu wake.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alimtakia mafanikio mema kiongozi huyo pamoja na wananchi wake na kuwatakia maendeleo katika kuimarisha amani, utulivu na umoja uliopo katika Muungano wa visiwa hivyo.

Pia, Rais Dk. Shein ametumia fursa hiyo kupongeza Rais wa Malawi Arthur Peter Mutharika kwa kutimiza miaka 55 ya Uhuru wa Taifa hilo na kumtakia sherehe njema yeye, familia yake pamoja na wananchi wote wa Malawi.

Kwa niaba yake binafsi, pamoja na  wananchi wote wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein  alitoa pongezi kwa kiongozi huyo na wananchi wake wote wa Malawi na kueleza kuwa hatua hiyo inatoa fursa ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya pande mbili hizo katika Nyanja mbali mbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii.

Rais Dk. Shein alimtakia kheri na mafanikio kiongozi huyo pamoja na wananchi wote wa Malawi sambamba na kuendeleza amani, utulivu na maendeleo ya kiuchumi kwa watu wa Malawi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.