Habari za Punde

Serikali Haina Nia ya Kuwanyanganya Mashamba Wananchi Walioamua Kujitolea Kuyaendeleza.

Viongozi wa CCM Mikoa Miwili ya Pemba na Wilaya zake Nne wakimpokea Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba kuzungumza nao.
Balozi Seif  akisisitiza umuhimu wa Wana CCM kujiimarisha mapema katika maandalizi ya kuendeleza Ushindi wa Chamna hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi wa CCM Mikoa Miwili ya Pemba na Wilaya zake Nne.
                                                     Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi amewashauri Viongozi wa CCM wa Mikoa Miwili  na Wilaya Nne za Pemba kuisaidia Serikali katika Mkakati wake wa kuyatambua na baadae kuyahakiki Mashamba ya Serikali yaliyomo katika Maeneo yao.
Alisema Serikali kamwe haina nia ya kutaka kuwanyang’anya Mashamba Wananchi walioamua kujitokeza katika kuyaendeleza Mashamba ya Serikali kwa Kilimo ambayo kwa Muda mrefu yamekosa huduma za usafishaji na kupunguza uzalishaji.
Akizungumza na Viongozi wa CCM Mikoa Miwili na Wilaya zake  hapo Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi wa Kisiasa ni kiungo muhimu katika suala hilo kwa vile wana uzoefu wa muda mrefu wa masuala ya Takwimu katika maeneo yao.
Balozi Seif  alisema  Serikali Kuu iliamua kufanya Tathmini ya Mali zake yakiwemo Mashamba tofauti ndio ikaunda Kamati Maalum ya Kufuatilia kuyatambua na hatimae kuyahakiki Mashamba yake ambayo hayajaingia katika Takwimu za Mali za Serikali.
Akizungumzia uimarishaji wa Chama cha Mapinduzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif  alisema si busara kwa Viongozi na Wana CCM  kusubiri kufanya maandalizi ya Uchaguzi huo katika muda wa Miezi michache kabla ya Uchaguzi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Uongozi wa Chama kuanzia ngazi ya Shina, Tawi, Jimbo hadi Wilaya ndio wenye jukumu la kuwaongoza Wanachama na Wananchi kuelekea ushindi wa Uchaguzi unaoanzia  kwenye uandikishaji.
Alisema jambo hilo kwa Viongozi wa ngazi zote wanapaswa kulisimamia vyema ili kwenda sambamba na Katiba ya CCM inayoeleza wazi kwamba ukifika wakati wa Uchaguzi CCM lazima ishinde Tanzania Bara na Visiwani.
Balozi Seif  aliwatahadharisha Viongozi hao kuwa makini na Watu wanaotumia ujanja wa kujifanya waumini sahihi wa Chama cha Mapinduzi lakini unapofika wakati wa uchaguzi wanabadilika na kuwa madalali wa vyama vyengine vya Kisiasa.
Wakichangia kwenye Mkutano huo  baadhi ya Viongozi Chama cha Mapinduzi Mikoa Miwili ya Pemba pamoja na Wilaya zake  walisema CCM inaweza kudhoofika  iwapo Viongozi watafumbia macho tabia za baadhi ya Wanachama kuendeleza uvivu, fitna,migogoro na roho mbaya.
Walisema katika kuimarisha nguvu za Chama Kiuchumi Katika ngazi zote juhudi za makusudi zinapaswa kuongezwa katika kuwapatia vifaa vya Kazi Watendaji wa wa Chama yakiwemo kuyafanyia matengenezo Magari pamoja na upatikanaji wa vifaa vya Ofisi.
Viongozi hao wameendelea kukumbusha utakelezaji wa ahadi zilizotolewa na Wagombea  wa Ngazi mbali mbali za Uongozi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 – 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.