Habari za Punde

Maonesho ya Kilimo Zanzibar Yafungwa leo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kat kati akiongozana na Waziri wake wa Nchi Mh. Mohamed Aboud Kulia na Naibu Waziri wa Kilimo Dr. Makame Ussi Shauri kutembelea Maonyesho ya Siku ya Nanane Nane huko Kizimbani yaliyoongezewa Siku Mbili ili kuwapa nafasi zaidi Wananchi,
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kasi ya kuendeleza Sekta ya Kilimo inatokana na utekelezaji wa Mipango ya Taifa ya Maendeleo iliyolenga kuifikisha Nchi kwenye Uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyolenga kwenye Dira ya Maendeleo ya Zanzibar  ya 2020.
Alisema kila Mwananchi anawajibika kwa nafasi aliyonayo kufanikisha malengo hayo ya Serikali katika kuimarisha Uchumi wa Taifa utakaomtoa katika wimbi la utegemezi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiyafunga Maonyesho ya Siku ya Wakulima Kitaifa Nane Nane yaliyokuwa yakifanyika Dole  Kizimbani Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema Mipango ya Maendeleo itazidi kuimarika hali itakayolifanya Taifa kuongeza Mapato yake kutoka asilimia 7.1% kwa Mwaka 2017/2018 hadi kufikia asilimia 7.8% kwa Mwaka 2019/2020.
Balozi Seif alisema Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi inatekeleza na kuhakikisha kwamba Elimu bora ya Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Matumizi ya kudumu ya Rasilmali inawafikia Wananchi kupitia Mabwana na Mabibi Shamba kwenye  Halmashauri kwa lengo la kuzalisha Chakula.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba Wizara hiyo kuendelea kufanya Utafiti ili kilimo chinachozalishwa Nchini kiendelee kukua na kuwa bora zaidi katika kasi  itakayosaidia kupunguza uagizaji wa chakula hasa mchele kutoka nje ya Nchi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa Maonyesho Kitaifa kwa lengo la kuhamasisha Jamii kuhusu umuhimu wa Sekta hiyo, kujua njia bora ya teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na namna ya usarifu  wa bidhaa za wazalishaji.
Balozi Seif alifahamisha kwamba nguvu za Vijana kwa sasa zimeelekezwa  katika ukuaji wa sekta ya Kilimo na uchumi wa Taifa baada ya kuundwa kwa Mabaraza yao yatayojengewa uwezo wa kupatiwa ajira kupitia Sekta hiyo zikiwemo nyengine.
Alisema maamuzi hayo ya kuundwa kwa Mabaraza ya Vijana kujielekeza kwenye miradi tofauti  hasa Kilimo itaweza kufutilia mbali ile dhana ya Kilimo ni kwa ajili ya Wazee kama ilivyozoeleka hapo nyuma.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba mafunzo waliyoyapata Wananchi hasa Vijana katika kujifunza mbinu mbali mbali ndani ya Maonyesho hayo yaelekezwe katika kujiajiri wenyewe kwenye uzalishaji wa Chakula.
Aidha alitoa wito kwa Wafanyabiashara kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuwapatia Wakulima, wafugaji na wavuvi masoko ya bidhaa zao ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa masoko na kuharibika kwa bidhaa baada ya mavuno.
Alisema Wananchi wengi wanaojishughulisha na Sekta ya Kilimo kipato chao kidogo jambo ambalo hata Taasisi za Kifedha zinawajibika kutoa mikopo nafuu kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa za Kilimo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa shukrani Maalum kwa Wizara ya Kilimo, Maliasini, Mifugo na Uvuvi, Washirika wa Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa, Taasisi za Serikali, Binafsi na Wafanyabiashara kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha Maonyesho hayo.
Aliwakumbusha Wananchi na Taasisi zilizopewa maeneo ya kujenga Majengo ya kudumu kwenye Maonyesho hayo liliopo Kizimbani Balozi Seif  wakamilishe Miundombinu hiyo ili kuleta m,abadiliko ya eneo hilo.
Alisema wale wenye ufinyu wa rasilmali ya Fedha wanaweza kujenga hoja Serikalini na kupatiwa Mikopo kwa ajili hiyo ili ifikie wakati Wananchi wanaweza kulitumia eneo hilo kupata huduma muhimu katika siku ya mapumziko ikiwa kama matembezi.
Mapema akitoa Taarifa ya Maonyesho hayo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Juma Saadala  alisema Maonyesho ya Mwaka huu yamefana sana kutoka na uongezeko la ushiriki wa Wananchi mbali mbali wakiwemo Wanafunzi.
Bibi Maryam alisema katika kutekeleza agizo la Serikali Kuu la kuyafanya Maonyesho hayo kuwa ya kudumu Wizara ya Kilimo tayari imeshatoa ploti kwa Taasisi, Mashirika na Watu Binafsi zipatazo 72 ndani ya eneo hilo la Hekta 7.4 ili kuliendeleza kuwa la kudumu.
Alisema Wizara imeshaziagiza Taasisi, Mashirika na Watu hao wajenge miundombinu ya kudumu ili kupunguza gharama za kila Mwaka zinazoweza kuepukwa.
Alisema maonyesho hayo yaliyofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein yalishirikisha Wadau 172 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alizishukuru Taasisi zilizounga Mkono maonyesho hayo ikiwemo Shirika la Chakula la Kimataifa  FAO, ZRB,PBZ, BIMA, ZSSF pamona na Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye ufungaji wa Maonyesho hayo Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dr. Makame Ussi Shauri alisema Wananchi pamoja na Wadau wa Maonyesho ndani na Nje ya Nchi watarajie Maonyesho mengine ya aina yake Mwaka huu ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Dr. Makame alisema Maonyesho hayo ya kuadhimisha Siku ya Kilimo Duniani      { World Food Day } yanatarajiwa kufanyika Kisiwani Pemba  katikia eneo la Chamanangwe yakiwa na Ujumbe mahsusi uitwao T. Saba {T7} .
Alisema T. Saba hizo  zinamaanisha Tulime, Tufuge, Tuvue, Tuendeleze Rasilmali zetu,Tule, Tushibe na Tusafirishe Bidhaa zetu nje ya Nchini kwa kuuza kupata kipato zaidi kitakachopunguza ukali wa maisha.
Katika ufungaji wa Maonyesho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitoa zawadi kwa washindi mbalimbali waliofanikiwa kuibuka washindi wa Mwaka huu.
Washindi hao Tisa waligawika katika Makundi Matatu ya Mafunzo ya Kilimo na Mifugo, Mashirika  ya Umma pamoja na Wajasiri Amali ambapo Mshindi wa Jumla wa Maonyesho  hayo ya Mwaka 2019 alikuwa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar |{JKU }.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliongeza Siku mbili za Maonmyesho hayo ya Siku ya Wakulima Nane Nane  ili kuwapatia fursa baadhi ya Wananchi waliokosa nafasi hiyo ndani ya siku Nane za Maonyesho hayo.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Maonyesho ya Siku ya Wakulima Kitaifa  Nane Nane yaliyogharimu jumla ya Shilingi Milioni  Mia Moja na Sita { 106,000,000/- } unaeleza :- Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ukuaji wa Uchumi wa Nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.