Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Mratibu wa UN Tanzania Ikulu Zanzibar


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Mwakilishi Mkaazi na Mratibu wa Mashirikaka ya Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania Bwana.Alvaro Rodriguez,alipofika Ikulu Zanzibarv leo, kwa mazungumzo na kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi Tanzania.

UMOJA wa Mataifa (UN) umeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inayosimamiwa na Mashirikia yake inatekelezwa kikamilifu na kupata mafanikio kwa azma ya kuwasaidia walengwa ambao ni wananchi wa Zanzibar.

Mwakilishi Mkaazi na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) hapa Tanzania Alvaro Rodriguez alisema hayo leo wakati alipofika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Alieleza kuwa Mashirika yote ya Umoja wa Mataifa (UN) yanayofanya kazi zake hapa Tanzania yanapongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein na kuahidi kuendelea kuunga mkono kwani wanafarajika na juhudi hizo.

Alieleza kuwa Umoja wa Mataifa (UN) unapongeza sana juhudi hizo za Rais Dk. Shein na unaahidi kuendelea kushirikiana nae huku akieleza kuwa mashirika yote ya (UN) yana matumaini makubwa ya kuona matokeo endelevu yatakayotokana na juhudi hizo katika miaka ijayo.

Pia, kiongozi huyo alieleza azma ya Mashirika hayo ya UN katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa maji safi na salama, utawala bora, uimarishaji wa haki za binaadamu, uwezeshaji, mapambano ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto uhifadhi wa mazingira pamoja na mambo mengineyo.

Mratibu huyo alieleza mafanikio yanayopatikana ambayo yamepewa kipaumbele katika  utekelezaji wa ‘Programu ya pamoja ya Zanzibar ya mwaka 2018-2021’ iliyozinduliwa Agosti mwaka jana  yakiwemo kupunguza vifo vya uzazi, ukatili dhidi ya wanawake na watoto, uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake kupitia zao la mwani pamoja na uratibu wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Mratibu huyo alieleza kuwa licha ya yeye kupangiwa majukumu mengine ya kikazi lakini anaamini kwamba kiongozi atakaye chukua nafasi yake ataendeleza uhusiano na mashirikiano mema yaliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na UN.

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Umoja huo chini ya Mratibu wake hapa Tanzania Alvaro Rodrigues ambaye amemaliza muda wake wa kazi hapa nchini kwa kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake wanampongeza Mratibu huyo kwa kuonesha moyo na juhudi kubwa za kuisaidia Zanzibar na kuiunga mkono katika miradi yake ya maendeleo wakati wa uongozi wote wa Rodrigues alipokuwepo nchini.

Aidha, Rais Dk. Shein alimtakia safari njema Mratibu huyo na kumtaka akaendelee kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa kama alivyofanya wakati akiwa hapa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.