Habari za Punde

AFRECO Kuipatia Basi Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma. *Basi Hilo ni Hospitali Kamili Itakayotoa Huduma Mkoani Dodoma na Mikoa Jirani.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa , Rais wa The Association of African  Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano (kushoto) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha, Profess  Donald Mpanduji (kulia) wakishikana mikono  ikiwa ni ishara ya makubaliano yanayolenga kuboresha hospitali ya Chuo Kuu cha Dodoma ya Benjamin Mkapa kati ya Chuo hicho na AFRECO baada ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan, Septemba 1, 2019.


Na,Khadija Mussa.OWM. 
TAASISI ya Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma basi ambalo ni hospitali kamili litakalotoa huduma za matibabu kwa Manispaa ya Dodoma, Mikoa na Wilaya zinazoizunguka Mkoa wa Dodoma.

Basi hilo litakapowasili nchini kutoka Japan linatarajiwa kuwa ni mkombozi kwa wananchi waishio vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali kwani kila litakakokwenda kutoa huduma litakuwa na madaktari waliobobea katika utaalamu wa tiba mbalimbali, vifaa tiba, maabara pamoja na dawa.

Hayo yamebainishwa leo (Jumapili, Septemba 1, 2019) na Rais wa   AFRECO, Bw. Tetsuro Yano katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.

Bw. Yano amesema wameamua kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini Tanzania baada ya kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Ameongeza kuwa anaamini siku moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika yote kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na vituo vingi vya Afya na hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama vile ya moyo na figo. Hata  hivyo tayari wagonjwa toka nchi jirani wameanza kuja kutibiwa nchini.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma za matibabu, pia taasisi hiyo ya AFRECO   itasaidia katika kupandisha hadhi hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa Shule kamili ya tiba.

Amesema hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma itapatiwa vifaa   mbalimbali vya tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni shule bobezi   kwa utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na Barani Afrika.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo maalum cha Uhandisi wa Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa tiba ili nchi yetu iwe na watalaamu wa  kukarabati vifaa tiba pindi vinapoharibika badala kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na watalaamu kutoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza.

“Hivi sasa yanafanyika makubaliano ya kuanzisha   kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba na kwa kuanzia wataanza kutengeneza maji ya drip ambayo huongezwa kwa wagonjwa kwa maeelekezo ya madaktari na baadae watengeneza dawa mbalimbali.”

Naye,Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma,  Mipango, Utawala na Fedha, Profesa Donald Mpanduji amesema wametia saini hati ya makubaliano kati ya  AFRECO na Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo yanalenga kuboresha hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Awali, Dkt. Omary Ubuguyu kutoka Wizara ya Afya amesema maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika huduma za tiba yameiwezesha Tanzania kupunguza wagonjwa wanaopelekwa nchi za nje kwa matibabu kutoka 800 hadi 42  ambalo ni punguzo la  asilimia inayotajwa kuwa 200.

Amesema hatua hiyo imeongeza nafasi kwa watalaamu wetu wa tiba kujifunza zaidi pamoja na kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi kutafuta tiba na pia imeipunguzia Serikali gharama ya fedha za kigeni ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,         
JUMAPILI, SEPTEMBA 01, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Rais wa The Association of African  Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano kabla ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Rais wa The Association of African  Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano kabla ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan September 1, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.