Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Shein Azungumza na Ujumbe wa Taasisi ya Utafiti ya Sheikh Saud Al Qasimi.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Ujumbe wa Taasisi ya Sera na Utafiti ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi wakizungumzia Masuala ya Elimu, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Waldorf Astoria Ras Al Khaimah.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Serikali ya Ras Al Khaimah katika kuanzisha programu ya mafunzo kwa walimu wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Sera na Utafiti ya Sheikh Saud Bin Saqri Al Qasimi huko katika ukumbi wa Hoteli ya Waldorf Astoria iliyopo mjini Ras Al Khaimah.

Ujumbe huo umekuja kufuatia agizo la Mtawala wa nchi hiyo alilolitoa kwa Msaidizi wake wa masuala ya elimu siku ambayo Mtawala huyo alikutana na kufanya mazungumzo na  Rais Dk. Shein katika ukumbi wa Kasri yake iliyopo Aldhait mjini Ras Al Khaimah.

Rais Dk. Shein alitoa shukurani zake kwa kiongozi wa Rais Al Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi kwa kulichukulia hatua ya haraka suala hilo na kupelekea kukutana na ujumbe wa viongozi wa Taasisi yake inayoshughulikia masuala hayo wakati bado yupo hapa hapa nchini Ras Al Khaimah.

Aidha, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi za kiongozi huyo anazozichukua katika kuiunga mkono Zanzibar na jinsi alivyolipa kipaumbe suala la kuimarisha sekta ya elimu kwa kuanzisha programu maalum ya mafunzo ya Walimu hatua itakayoimarisha ubora wa elimu kupitia mafunzo hayo ya Uwalimu kwa Walimu wa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein aliualika uongozi wa Taasisi hiyo kuja Zanzibar kwa lengo la kukutana na uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha  Zanzibar (SUZA) ili kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo itaiwezesha Wizara ya Elimu kutoa vipaumbele vya mahitaji waliyonayo ili iwe rahisi kutekeleza programu hiyo jambo ambalo litaisaidi Taasisi hiyo kutambua vipaumbe vya Zanzibar na hatimae kurahisisha utekelezaji wa programu hiyo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Sera na Utafiti ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi Natasha Ridge, alieleza kuwa Taasisi hiyo pia, inajishughulisha na utoaji wa mafunzo ya kitaalamu ya kuwajengea uwezo walimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni kwa lengo la kutoa mafunzo bora kwa wanafunzi ambayo yatawasaidia katika kumudu masomo yao ya ngazi za juu hususan katika Vyuo Vikuu popote watakapokwenda kusoma.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa Msingi na Sekondari ili waweze kuwatayarisha vizuri wanafunzi wao wanaopoingia katika ngazi za juu za masomo hasa Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya nchi yao.

Vile vile, Mkurugenzi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa katika programu zao wana mafunzo ya kufundisha njia bora za uongozi katika masuala ya elimu na kusisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya elimu Zanzibar.

Aidha, alisema kuwa katika utaratibu wao wa kutoa mafunzo huwa wanatoa mafunzo kwa Wakufunzi ambao na wao wataweza kuwafundisha walimu wengine ili ujuzi huo usambae kwa walimu wengi zaidi.

Sambamba na hayo, Mkurugenzi Mtendaji huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa wako uongozi wa Taasisi hiyo uko tayari kuja Zanzibar mnamo mwezi wa Novemba mwaka huu kwa ajili ya kukutana na uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kuangalia vipaumbelea ambavyo wao wataweza kuvifanyia kazi katika kutoa mafunzo hayo.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.