RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amekutana na Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Mtukufu Sheikh Saud
Bin Saqr Al Qasimi na kufanya nae mazungumzo yaliolenga kuendeleza uhusiano na
ushirikiano hasa katika sekta ya elimu.
Mazungumzo hayo yaliofanyika katika makaazi ya Sheikh Saud Bin
Saqr Al Qasimi mjini Ras-Al-Khaimah, ambapo kiongozi huyo wa Ras- al
Khaimah alimuhakikishia Rais Dk. Shein
kuwa yuko tayari kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu.
Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi alieleza kuwa Ras-al Khaimah imepiga hatua
nzuri katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya juu hivyo, ipo tayari kutoa
fursa kwa walimu wa Zanzibar kwenda nchini humo kujifunza katika vyuo vikuu
vilivyopo.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itasaidia zaidi kutoa nafasi kwa walimu wengi
waliopo Zanzibar kupata mafunzo ambayo watawasaidia na walimu wengine sambamba
na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hasa wale wanaosoma elimu juu.
Alieleza kuwa programu hiyo ya kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo walimu
kutoka Zanzibar itakuwa ya kila mwaka na itadhaminiwa na Serikali ya Ras Al
Khaimah.
Aidha, kiongozi huyo alieleza kuwa programu hiyo itajikita zaidi katika
masomo ya Sayansi hali ambayo itasaidia kuendeleza masomo hayo sambamba na
kuimarisha sekta ya elimu hasa katika karne hii iliyopo.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walieleza kuwa Zanzibar na Ras-al.
Khaimah zina mambo mengi yanayofanana kwa hivyo kuna haja kubwa ya kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo.
Pamoja na hayo, kiongozi huyo wa Ras Al Khaimah alimueleza Rais Dk. Shein
azma ya nchi yake kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta
mbali mbali za maendeleo zikiwemo za kiuchumi na kijamii.
Alieleza kuwa nchi yake inathamani uhusiano na ushirikiano huo uliopo na
kuahidi kuwa itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha mashirikianao
katika sekta za maendeleo yanadumishwa baina ya pande mbili hizo.
Kiongozi huyo wa Ras
Al Khaimah alizipongeza juhudi za Rais Dk. Shein na kuahidi kuziunga mkono
kwani anaona jinsi anavyofuatilia kwa karibu uimarishaji wa sekta za maendeleo kwa
manufaa ya Zanzibar na watu wake.
Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein, katika maelezo yake, alitoa shukrani kwa kiongozi huyo kutokana na juhudi
zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na kumpongeza kwa azma yake hiyo ya
kuiunga mkono sekta ya elimu Zanzibar.
Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar ina mengi ya
kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Ras Al Khaimah na iko tayari kupanua wigo wa
maendeleo kutoka nchini humo kwani inatambua mafanikio yaliopatikana kutokana
na mikakati iliyowekwa katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya
elimu.
Pamoja na hayo, viongozi hao kwa pamoja walizungumzia hatua zaidi
zinazohitajika katika kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Ras Al Khaimah
katika sekta za maendeleo ikiwa ni pamoja na kupanga mipango madhubuti katika
malengo yaliokusudiwa ya hapo baadae.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Sheikh Al Qasimi na kueleza
kuwa programu hiyo ambayo amekusudia kuiunga mkono itasaidia kuimarisha juhudi
za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazoendelea kuzichukua katika kukuza
sekta hiyo.
Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa tayari Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imepiga hatua katika kuimarisha elimu ya msingi na
Sekondari hivyo hatua hiyo ya Serikali ya Ras Al Khaimah itasaidia kuimarisha
elimu ya juu sambamba na kuongeza idadi ya wataalamu katika fani mbali mbali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment