Habari za Punde

KAMPENI YA CHANJO KITAIFA MWEZI ULIOPITA IMEFIKIA ASILIMIA 97.9

Katibu wa Kamati ya Kampeni ya Chanjo Kitaifa  ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya  Halima Maulid akiwaeleza wajumbe wa kamati hiyo changamoto zilijitokeza katika mkutano wa tathmini uliofanyika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi Mmoja .  
Na Kijakazi Abdalla  Maelezo  8/10/2019
Wizara ya Afya Zanzibar imeweza kufikia asilimia 97.9 kwenye Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua, rubella na polio iliyoanza tarehe 26 na kumalizika tarehe 30 mwezi uliopita Unguja na Pemba.
Hayo ameyasema Mratibu wa kampeni ya chanjo Zanzibar Abdulhamid Ameir katika mkutano wa tathmini ya Kampeni hiyo uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Amesema zoezi la chanjo hiyo lilienda vizuri na Wilaya zote zilionyesha ushirikiano na kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa kwa Unguja na Pemba.
Aliitaja mikoa iliofanya vizuri zaidi katika Kampeni hiyo kwa Unguja ni Kusini na Pemba ni Mkoa wa Kaskazini.
Alisema wananchi wengi walijitokeza kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo hizo bila ya kujali kuwa walipatiwa katika chanjo za aina hiyo siku za nyuma.
Alieleza kuwa kuchelewa kuanza kazi na kufungwa mapema kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma ya chanjo ilisababisha usumbufu kwa baadhi ya wazee kutowapeleka watoto.
Wajumbe wa mkutno huo waliiomba Wizara ya Afya kutumia njia za asili kuhamasisha wananchi ikiwemo kupiga upatu mtaa kwa mtaa hususani vijijini ili wananchi waweze kuhamasika.
Aidha wameshauri kutumia zaidi vituo ambavyo wananchi wamevizoea badala ya kutumia vituo vya dharura ili kuwa rahisi kwenda kupata huduma ya chanjo.
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman amewashukuru wananchi wote waliojikeza katika zoezi la Kampeni ya chanjo  na kuwahakikishia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa mapendekezo waliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Aidha aliwaomba wananchi wasichoke na inapotokea Kampeni  nyengine ya kuwakinga watoto na maradhi wajitokeze kwa wingi kama walivyofanya kampeni iliyomalizika ili kuwa na wananchi wenye afya bora zaidi hapo baadae .
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.