Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Pemba, kulia Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar.Mhe. Mmanga Mjengo Mjawiri.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali imejidhatiti
kuendeleza kwa vitendo Mapinduzi ya Kilimo kwa kuwapa taaluma ya kilimo bora
wakulima, wafugaji na wavuvi, pamoja na kuendeleza huduma za ugani.
Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa Maonesho ya siku ya chakula Duniani, yaliofanyika katika viwanja vya Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Alisema katika kutekeleza azma hiyo, Serikali itaendelea kutowa
huduma za matrekta na pembejeo mbali mbali za kilimo, kwa kutoa ruzuku ya
asilimia 75 kama ilivyoahidi .
Alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya
kibiasharaili kuwawezesha wafanyabiashara kuingiza na kuuza zana, vifaa na
pembejeo za kisasa kwa wakulima kwa urahisi.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya wakulima kulima kwa
kuzingatia matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo pamoja na kufuata maelekezo ya
wataalamu.
Alitaka kuwepo matumizi bora ya pembejeo
za kilimo, mbolea pamoja na kuwataka wakulima kuondokana na kilimo cha mazowea,
akibainisha hatua hiyo italiwezeshaTaifa kuongeza mavuno ya mazao ya chakula na
biashara na kutoa uhakika wa chakula na lishe bora.
Rais Dk. Shein aliitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi kuhakikisha inakuwa na mipango na mikakati madhubuti katika kuwaelimisha,
kuwahamasisha na kuwasaidia wananchi ili kuwa na mwamko wa kutumia teknoljia
bora za kilimo katika mazao mbalimbali.
“Maarifa watakayopata wananchi kupitia maonyesho haya
yatawasidia kupata mbinu mpya za
kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuongeza tija”, alisema.
Aidha, alisema kupitia maonyesho hayo, wananchi watapata fursa
ya kuzijua taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa wakulima, wavuvi na wafugaji
pamoja na wajasiriamali na hatimae
kuweza kusaidiwa.
Alisema wananchi wataweza kujifunza na kuitumia elimu watakayoipata
ili kuongeza uzalishaji katika shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji na hivyo
kukuza uchumi pamoja na kujiongezea kipato cha kujikimu.
Akigusia changamoto za ajira zinazowakabili vijana, Dk.
Shein aliisistiza umuhimu wakutembelea
maonesho hayo ili kuona fursa za kujiajiri zilizopo.
Alisema serikali itaendelea na juhudi za kuwasaidia vijana
kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao kupitia mfuko maalum ulioanzisha hivi
karibuni pamoja na Mfuko wa Khalifa Fund wenye gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 10.
Sambamba na hilo, Dk. Shein alisema katika kipindi cha miaka
mitano serikali imetenga Dola Milioni 10 (sawa na shilingi Bilioni 46) kwa
lengo hilo hilo la kuwawezesha vijana kujiajiri na kupunguza kutegemea ajira
kutoka serikalini.
Katika hatua nyengine, Dk.Shein alisema Serikali imeanzisha
taasisi ya utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi ili kuziwezesha shughuli hizo kufanyika
kisasa zaidi pamoja na kubaini changamoto zilizopo, hatua iliyokwenda sambamba na
kukiunganisha Chuo cha Kilimo Kizimbani na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA).
Alitowa wito kwa vijana wenye sifa za kujiunga na masomo ya utaalamu wa kilimo, mifugo na
uvuvi kujiunga na na masomo hayo ili Taifa lipate wataalamu inaowahitaji.
“Naiagiza Wizara ya Kilimo, maliasili. Mifugo na Uvuvi
iendelee kuwaajiri vijana waliokwisha maliza masomo yao ya kitaalamu
wakumbushwe kazi zao sio kukaaa ofisini, bali wawafuate wakulima huko waliko,
kwani ndio namna bora ya kuwatumikia”, alisema.
Akigusia uendelezaji wa kilimo cha mpunga, Dk. Shein alisema
kuna mafanikio ya kuongezeka kwa mavuno yalioanza kupatikana na kusema hivi
sasa Serikali imejielekeza katika mradi mkubwa wa ujenzi wamiundombinu ya
uwagiliaji maji kupitia mkopo wa Dola Milioni 50 kutoka Benki ya Exim ya
Jamuhuri ya Korea.
Alisema mradi huo utatekelezwa katika mabonde matano
yanayolimwa mpunga, ikiwemo Cheju, Kilombero, Bumbwisudi, Mkwararani na
Mlemele, hatua itkayopanuwa wigo wakilimo cha mpunga wa umwagiliaji kutoka
ekari 810 hivi sasa na kufikia ekari 2,397.
Alisema kutokana naongezeko hilo, kuna matarajio makubwa ya
kuongezeka kwa mavuno ya mpunga nchini kutoka wastani watani 31,000 za mchele
hadi kufikia tani 70,365, hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika
kuagiza bidhaa hiyo.
“Takwimu zinaonyesha Zanzibar kwa mwaka tunatumia wastani wa
shilingi Bilioni 40.5 kununua mchele peke yake, kiwango hiki kitapungua kwakiasi
kikubwa na hatimaeckuondoka kabisa”, alisema.
Aidha, aliwataka Wakuu wa Wilaya kote nchini kuongeza kasi ya mashirkkiano na Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, sambamba na kusimamaia ipasavyo maendeleo
ya kilimo katika Wilaya zao.
Alieleza kuwa mafanikio haliofikiwa na kuongezeka uzalishaji
katika sekta ya kilimo, kunatowa matumaini makubwa katika miaka michache ijayo
Zanzibar itajitosheleza kwa chakula, kuwa na lishe bora na usalama wa chakula.
Alisema lishe borana usalama wa chakula ni muhimu katika
kuleta ustawi wa jamii na hasa watoto wenye mahitaji maalum pamoja na wagonjwa.
Dk. Shein aliipongeza Wizara ya kilimo, Maliasili,Mifugo na
Uvuvi pamoja na Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali kwa kuendeleza mpango wa
kutoe elimu ya lishe bora kupitia maskulini, akibainisha kuwa ni uamuzi waserikali
katika kuimarisha afya za watoto pamoja na kukabiliana na utapiamlo.
“Natoa wito kwa wananchi kuzingatia haja ya kula chakula
chenye lishe bora kitakachosaidia kuimarisha afya zetu, tuone umuhimu wa kula
vyakula vya asili vinavypapatikana kwawingi hapa nchini,ikiwemo matunda na mboga
mboga ili tupate lishe bora”, alisema.
Mapema, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga
Mjengo Mjawiri, alisema muelekeo wasekta ya kilimo ni kuongeza uzalishaji na
usarifu wa mazao ili kuongeza tija kama ilivyoainishwa katika MKUZA pamoja na Ilani
ya Chama cha Mapinduzi ya 2015-2020.
Aliipongeza serikali kwa juhudi za kutoa kipaumbele katika
sekta ya kilimo, ili kuona uzalishaji wachakula onaongezeka na kuleta tija kwa
jamii.
Alisema uamuzi wa Serikali wa kuanzisha Idara ya uhakiki wa
chakula pamoja an ghala la Akiba la chakula ni muhimu , kwani pamoja na mambo
mengine utapunguza mfumko wa bei na kuondokana na hatari ya kuibuka kwa njaa.
Alisema Wizara hiyo kwamashirikiano na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali imejidhatiti kuendelea
kutoa elimu kwa wananchi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi juu ya lishe
bora pamoja na matumizi endelevu ya
rasilimali zilizopo, sambamba na kuwataka wananchi, hususan vijana kutumia
maonesho hayo kupata ujuzi.
Nae, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo. Maliasili, Mifugo na
Uvuvi, Maryam Juma Abdalla alisema maonyesho hayo ni ya pili kufanyika katika
eneo hilo la Chamanangwe, yakiwa na lengo la kuhamisha wananchi na wadau
kutekeleza sera za kuimarisha kilimo nchini.
Alisema sekta ya kilimo imekuwa na mchango mkubwa katika
kukuza uchumi na mandeleo ya Taifa na kubainisha katika mwaka uliopita wa 2018,
sekta hiyo ilichangia wastani wa asilimia 21.3 ya pato la Taifa.
Alisema maonesho ya mwaka huu yameshirikisha wadau 207 kutoka
taasisi za serikali na binafsi, wafanyabiashara pamoja na watoa huduma kutoka
serikalini na sekta binafsi.
Maryam aliyapongeza mashirika ya ndani na yale ya Kimataifa
kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kuimarisha kilimo pamoja na kufanikisha
vyema maonesho hayo.
Katika hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alikabidhi zawadi kwa vikundi mbali mbali
vilivyofanya vizuri pamoja na kutembelea mabanda ya maonesho kuona uzalishaji
wa bidhaa mbali mbali.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment