KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mjini katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha CCM Unguja.
Na.Is-haka Omar -,ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru,amewataka Viongozi na Watendaji wa CCM visiwani Zanzibar kuendelea kubuni miradi itakayoongeza mapato ndani ya Chama.
Rai hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara yake wakati akizungumza na Viongozi na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mjini Unguja huko Mkoa wa CCM Mjini.
Dkt.Bashiru. Bashiru,alifafanua kuwa uwepo wa miradi mbali mbali itasaidia Chama kujitegemea kiuchumi.
Alisema rasilimali za vyanzo vya mapato zinazomilikiwa na CCM katika maeneo mbali mbali nchini zikitumiwa vizuri zitasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa fedha katika maeneo mbali mbali nchini.
"Chama chetu kimejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo majengo, ardhi na vitu mbali mbali vilivyoasisiwa na Wazee wetu wa ASP na TANU,wajibu wetu kuvitunza na kuongeza vingineN ili na sisi tuache alama za uongozi kama walivyafanya viongozi waliopita.
Nasi tunaendelea kudhibiti rasilimali hizo zisihujumiwe na watu wachache kwani zipo kwa manufaa ya wanachama wote",alisema Dkt.Bashiru.
Kupitia Kikao hicho alihimiza wanachama kuendeleza utamaduni wa kuwa na mahusiano ya kijamii baina ya wanachama na wanachama pamoja na wananchi wengine.
Alisema mahusiano hayo ndio msingi wa Umoja na Mshikamano wa Chama Cha Mapinduzi unaowafanya watu wawe wamoja.
Aidha Dkt.Bashiru, alikemea siasa za ubaguzi kuwa zinatakiwa kupingwa na vyama vyote vya siasa kwani zinaharibu sifa ya nchi na kusababisha mipasuko isiyokuwa ya lazima kwa wananchi.
"Siasa za ubaguzi haziwezi kujenga umoja wa kitaifa hivyo tukiwa ni Chama kinachoongoza dola ni lazima tuwakumbushe vyama vingine vya siasa nchini waepuke dhambi hiyo kwani madhara yake ni makubwa juu ya ustawi wa maendeleo ya nchi.", alisema dokta Bashiru.
Alisema CCM sio chama cha wakati wa uchaguzi bali ni chama cha uongozi kinachoongoza wananchi wote, hivyo hakiwezi kushindwa kukemea juu ya masuala mbali mbali yanayolenga kuhatarisha Amani na Utulivu wa nchi.
Akizungumza kwa wakati tofauti wakati akipandisha bendera za chama katika mashina mbali mbali ya CCM,aliwataka Watendaji wa ngazi za wilaya kuhakikisha mabalozi wote wanapatiwa vitambulisho vitakavyowasaidia kuingiza katika ofisi za umma kuwasilisha changamoto za wananchi ili zitatuliwe.
akizungumza baada ya kukagua kazi za vikundi vya ujasiriamali katika Chuo Cha Ujasiriamali cha UWT Wilaya ya Mjini Kilichopo Miembeni,Dkt.Bashiru aliwapongeza viongozi wa CCM na kuwataka bidhaa zinazozalishwa katika Chuo hicho zitatuliwe soko la uhakika.
No comments:
Post a Comment