Na Mwashungi Tahir Maelezo 22-112019.
Jamii imetakiwa kuwathamini watoto wenye mahitaji maalum kwa kuwasaidia katika kuwapatia misaada mbali mbali ili waweze kujikwamua kimaisha .
Hayo ameyasema Katibu wa kamati maalum ya NEC ya Idara maalum ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar.Bi.Catherine Peter Nao huko Kituo cha Upendo (Viziwi) kilioko Mwanakwerekwe wakati alipokuwa akikabidhi vifaa vilivyotolewa na Mwakilishi wa viti maalum kupitia watu wenye ulemavu Mwantatu Mbaraka Khamis kwa walimu wa kituo hicho.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiwa katika Utekelezaji wa Ilani imeweka sehemu maalum ya watu wenye mahitaji maalum kwa kutambua umuhimu wa watu hao na kuweka kipaumbele kwa kuwapatia mahitaji yao ili wapate faraja ya kuthaminiwa.
Pia amewaomba wazazi na walezi kushirikiana na walimu wanaowafundisha watoto hao walio katika mazingira hayo kwa kuwa nao karibu kwani sote ni walemavu watarajiwa.
Hivyo amewataka wawe na subira na kuwapa malezi yaliyo mazuri watoto hao kwa kuwa nao karibu na kuepuka kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji ambavyo huwaathiri kisaikolojia.
”Hivi sasa kadhia ya udhalilishaji imelikumba Taifa hasa watoto wenye ulemavu tuwe karibu nao ili tuweze kuwalinda na vitendo hivi, “ alisema Catherine..
Vile vile amewataka wazazi na walezi kutoa michango ya watoto hao kwa walimu ili waweze kukidhi mahitaji yanayotakiwa kituo hapo ikiwemo sabuni chakula na mahitaji maalum mengine wanayohitajika kwa walimu hao wanajitolea kuwafundisha na kuwatunza .
Hata hivyo ameiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kukitembelea kituo hicho ili kujua changamoto zinazowakabili na kuona vipi wataweza kuwasaidia.
Nae Mwakilishi wa vitu maalum vya watu wenye ulemavu Mwantatu Mbaraka Khamis akikabidhi vifaa katika kituo hicho amesema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuunga mkono baada ya kuona wanapatiwa mafunzo ya kujiendeleza katika kituo hicho .
Amewapongeza walimu wa kituo hicho kwa juhudi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia watoto hao katika mambo mengi ikiwemo kufuma , kushona na pia kutengeza madomet na vitu vyengine kadha na kuweza kujipatia fedha za kujikimu kimaisha.
Kwa upande wa msoma risala Msaidizi Mkuu wa kituo hicho cha Upendo Sada Hamadi Ali amesema kituo kinatoa mafunzo mbali mbali yakiwemo ya lugha za alama kwa watoto wadogo wa maandalizi na wa skuli za misingi za Serikali ikiwemo kazi za amali kwa vijana viziwi .
Pia wanatoa mafunzo ya uzoefu wa tabia za watoto viziwi na wanafunzi wakubwa kufundishwa lugha za alama ili waweze kupatiwa fursa ya ajira kwa kutumia lugha hiyo katika sehemu za kazi.
Amesema mafanikio waliyoyapata watoto kujua kuelewa lugha za alama, kituo kutambulika katika sehemu mbali mbali, pamoja na mashirikiano na viongozi wa jimbo hilo .
Kwa upande wa changamoto amesema wanakabiliwa na ukosefu wa mashirikiano na baadhi ya wazazi, ulipaji wa ada, kukosa sehemu ya kuuzia bidhaa zao na ukosefu wa mtaji wa kuendeleza bidhaa hizo .
Jumla ya sh Millioni Moja zimetumika kwa kununuliwa vifaa hivyo ikiwemo sare za skuli , mabuku, vitamba vya kufumia mashuka , charahani ya kushonea na ya kufumia .
No comments:
Post a Comment