MAKAMO
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameiunga mkono kauli ya Wazee wa CCM wa
Wilaya ya Kusini Unguja ya kuwa Wilaya hiyo itaendelea kuwa ngome ya CCM.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Skuli ya
Kizimkazi Mkunguni, Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja wakati
alipofanya mazungumzo na Wazee wa Wilaya ya hiyo.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa Wilaya
ya Kusini Unguja ina historia kubwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo,
anaamini kuwa Wilaya hiyo ina uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa ngome ya chama
hicho.
Alieleza kuwa ushindi wa CCM katika chaguzi zake zote ni
jambo ambalo halina mbadala kwani hilo ni agizo la Katiba ya Chama hicho
kutokana na malengo iliyojiwekea.
Alisema kuwa malengo ya CCM yako wazi kwamba chama hicho
kimeundwa kwa lengo la kushinda uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, aliwataka viongozi wote wale ambao wako madarakani
na wale wasiokuwepo madarakani bado wana nafasi ya kukipigania Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kama wanavyofanya Wazee na Mabaraza yao pamoja na Jumuiya za
Chama hicho.
Aliwataka viongozi na wanachama wa CCM kufanya kazi na
wazee sambamba na kuwasaidia ili waendelee kukiimarisha chama.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa
wazee kuwaeleza vijana juu ya heshima ya wazee na vipi wazee wanatakiwa
kuenziwa na kutunzwa sambamba na kupewa heshima yao kutokana na mambo makubwa
waliyoyafanya.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inathamini na inazijali juhudi za wazee walizozichukua hadi kupelekea
kupatikana uhuru wa Tanganyika na uhuru wa Zanzibar kupitia vyama vya ASP na
TANU.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM
pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee
ndio walioijenga Zanzibar na kuleta ukombozi na hatimae kuwakomboa wanyonge.
Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa ipo haja ya kupokea
mawazo ya wazee sambamba na kuwaheshimu
na kuwalinda wazee kwani kuna kila sababu ya kufanya hivyo hasa ikizingatiwa
historia ya wazee katika kupigania uhuru wa nchi hii.
Rais Dk. Shein alipongeza kwa mapokezi makubwa aliyoyapata
katika Wilaya hiyo na kuipongeza risala iliyotolewa ambayo imetoa pongezi kwake
na kwa Serikali pamoja na wananchi kwa kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya
CCM kwa vitendo.
Makamu mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza umuhimu wa
wazee umo kwenye Katiba na Ilani ya CCM kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliongeza kuwa wakati huu uliopo ndio wakati mzuri wa kushikamana
na kuwa kitu kimoja sambamba na kuongeza nguvu katika kukiimarisha na
kukiendeleza Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisisitiza kuwa ushindi kwa CCM ni lazima ili Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964 yaendelee kulindwa yadumishwe na yaendelezwe
sambamba na kudumishwa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi
alieleza kuwa utamaduni wa Rais Dk. Shein wa kukutana na wazee ameuanza muda
mrefu na kusisitiza haja kwa viongozi wengine wa chama kuiga utamaduni na
utaratibu huo.
Naibu Mabodi alieleza kuwa mbali ya juhudi alizozichukua
katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo nchini pia, amefanya juhudi
katika kukiimarisha chama kwa kujenga Matawi, kuimarisha Mashina pamoja na
Ofisi za chama.
Nao Wazee wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja walieleza kuwa
wanaamini kuwa ujio wa Rais Dk. Shein katika Wilaya hiyo watapata baraka,
nasaha, busara pamoja na hekima zake za kuijenga CCM hususan kwa kipindi hichi cha
kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Aidha, walieleza jinsi wanavyoridhika na utekekelezaji wa
Rais Dk. Shein wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa
vitendo pamoja na ahadi zake alizozitamka kipinndi cha Kampeni zilizopita
kuzitimiza.
Wazee hao walimpongeza kwa mengi aliyoyafanya ndani ya
Zanzibar kwani yapo ambayo yamewagusa moja kwa moja ikiwa ni pamoja na malipo
ya Pencheji Jamii ya TZS 20,000 ambapo walianza wazee 1,421 mnamo mwaka 2016 na
hivi sasa wapo wazee 1,348 ambao wote wanapata Pencheni hiyo.
Pia, wazee hao walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kwa
jitihada na huruma zake kubwa aliyowaonesha wazee kwa kuwaongeza kima cha chini
cha penscheni ya wastaafu.
Walieleza kuwa uungwana wa uchapakazi wa Rais Dk. Shein uliotukuka wao wazee wanauona zaidi pale alipolisimamia
kidete suala la upatikanaji wa maji safi na salama katika Wilaya yao na kutolea
mfano wa kutatua tatizo la maji Makunduchi eneo la Mnywambiji.
Aidha, ahadi aliyoitoa Shehia ya Mtende ameitimiza kabla ya
muda wake aliouahidi kufika sambamba na kero ya muda mrefu Shehia ya Michamvi
nayo ameshaipatia muarobaini wake na sasa kazi ya kuzika mabomba inaendelea
kutokea katika visima vya Ras el Khaimah Bwejuu kuelekea Michamvi.
Walieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inatarajia kugharamia zaidi ya Bilioni 1.8 katika mradi huo.
Pia, wazee hao walieleza kuridhika na juhudi anazozichukua
na Serikali anayoiongoza katika suala zima la kipaumbele cha elimu kwa Zanzibar
nzima, kuanzia ujenzi wa skuli za ghorofa, mipango imara ya kuendesha elimu,
ufaulu wa wanafunzi umeongezeka na utoro wa skuli umepungua.
Sambamba na hayo, wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa
kuwajengea Chuo Cha Amali killichopo Kisongoni Makunduchi na Skuli Sekondari ya
kisasa iliyopo Kibuteni, kuwepo kwa majengo hayo wanaamini itatoa viongozi bora
wa hapo baadae.
Kwa upande wa sekta ya afya wazee hao walimpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuifanya Wilaya yao ya Kusini kuwa na huduma za kisasa na
zinazokwenda na wakati kwa kuipandisha
hadhi hospitali yao ya Makunduchi kuwa Hospiyali ya Wilaya.
Walieleza kwamba kiufanya hivyo kunasaidia kwa kiasi
kikubwa sana baadhi ya huduma ambazo walilazimika kwenda katika hospitali ya
rufaa na sasa zimesogea Hospitalini hapo.
“Tunashukuru sana wazee wako kwa hakika wewe ni mja mwema unaejali wazee wako bila ya
ubaguzi wa rangi, kabila wala itikadi ya siasa tunasema ahsante sana”,
walieleza wazee hao kwenye taarifa yao hiyo.
Sambamba na hayo, wazee hao walimuaahidi Rais Dk. Shein
kuwa Wilaya yao ya Kusini itaendelea kubaki kuwa ngome ya CCM.
Wazee hao pia, walishukuru
sana kwa kuansihwa utaratibu mpya
wa kuwakumbuka na kuwaombea dua Waasisi na viongozi mbalaimmbali ambao
wamelitumikia Taifa hili kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Nae Mwenyeviti wa
CCM Wilaya ya Kusini Unguja Abdulaziz Hamad Ibrahim alipongeza ukusanyaji wa
mapato na ukuaji wa uchumi jinsi ulivyoimarika hapa Zanzibar hatua ambayo
imepelekea kuimarika kwa huduma mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na ununuaji
meli mpya ya mafuta na meli ya abiria.
Alimpongeza Makamo huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Rais Dk.
Shein pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli kwa hatua walizochukuwa
katika kuhakikisha ada kwa wanachama wa CCM inahifadhiwa katika akauti maalum hatua
ambayo imepelekea kupatikana fedha nyingi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment