Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Amesisitiza Ahadi Aliyoitoa ya Ujenzi wa Barabara na Daraja la Kisasa Kisiwa Cha Uzi Wilaya ya Kati Unguja Iko Palepale.LAIpo zua I


MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kwamba ahadi aliyoitoa ya ujenzi wa barabara na daraja la kisasa la kuelekea kisiwa cha Uzi iko pale pale.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kulifungua jengo jipya la Tawi la CCM la Ng’ambwa, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambalo ni Tawi Kongwe miongoni mwa Matawi ya CCM hapa nchini lenye umri wa miaka 61 tokea kuanzishwa kwake.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kuwa Serikali tayari imo katika upembuzi yakinifu na imeshamkabidhi Mjenzi Muelekezi kufanya michoro ya njia hiyo pamoja na daraja ambapo awamu ya kwanza tayari imeshafanyika na hivi sasa iko katika awamu ya pili.
Rais Dk. Shein alisema kuwa lengo ni kujengwa daraja la kisasa litakalofanana na lile la daraja jipya la Kibonde mzungu jambo ambalo linawezekana kufanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa CCM.
“Serikali haishindwi kujenga daraja hilo kwani ikiamua inaweza na hilo linaweza kufanywa na litafanywa kwa nguvu za Allah, Serikali ya Awamu ya Saba itaanza na kama haikumaliza basi Serikali ya Awamu ya Nane italimaliza”, alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba juhudi za makusudi zinafanywa na Serikali katika kuhakikisha mradi huo unafanikishwa haraka iwezekanavyo na kwa umuhimu wake huwenda likapangwa katika Bajeti ijayo ili lianze kufanyiwa kazi.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alitoa pongezi kwa uongozi wa Jimbo la Tunguu, wanaCCM pamoja na wananchi wote Ng’ambwa sambamba na makaribisho makubwa na mapokezi aliyoyapata wakati akiwasili kisiwani humo.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na ahadi yake aliyoiahidi siku ya Februari 19, 2019 alipofanya ziara ya kikazi huko Ng’ambwa na kuahidi kuwa atakuja tena kushirikiana na WanaCCM wenziwe kujakulizindua Tawi hilo ambapo aliahidi kuwa Tawi hilo litajengwa na atakuja kulifungua na baadae wanaCCM Ng’ambwa watafurahi kwa kula kipila na kucheza rusha roho, ahadi ambayo leo ameitekeleza.
Alieleza kuwa pale panapofunguliwa Tawi la CCM ni vyema kukakumbushwa umuhimu wa wazee kwani ndio hazina kubwa ya chama hicho na ndio maana akafanya ziara ya kuzungumza na wazee wa CCM wa Wilaya zote 12 za Chama za Zanzibar pamoja na viongozi wa chama hicho.
Alisisitiza kwamba Katiba ya CCM, imeeleza utaratibu wa viongozi wa CCM namna gani wanatakiwa kufanya kazi katika Ngazi zake zote kuanzia Shina, Tawi, Wadi, Jimbo, Wilaya hadi Mkoa.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wanachama kupewa taarifa mapema juu ya chama chao na kusema kuwa Tawi hilo ndio utajiri wa siasa wa Wanang’ambwa wa CCM hivyo, ni vyema wakalitumia vizuri.
Aliongeza kuwa CCM ina hadhi yake na hadhi yake inakwenda sambamba na majengo yake yakiwemo Matawi ya chama hicho.
Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba Tawi hilo ni vyema likafanya kazi za Chama na kumtaka Mwenyekiti na Katibu wake kulisimamia vyema Tawi hilo kwa kuwapa taarifa wanachama wa chama hicho na kusema kwamba Tawi hilo ni vyema likawa na vuguvugu la kutafuta ushindi wa CCM.
Alieeleza jinsi alivyoridhishwa na kutiwa moyo na taarifa ya ujenzi wa Tawi hilo na kuwataka wananchi wa kisiwa hicho kufanya subira kwani Serikali imo katika kukamilisha mradi wa maji safi na salama.
Alitaka kufanyakazi za siasa kwa nguvu zote ili CCM iendelee kurudi madarakani na kuwataka wanaCCM kuhakikisha chama chao kinarudi madarakani kwani hiyo ni kazi ya wanaCCM na viongozi wake wote kupitia Jumuiya zao kwa mashirikiano na wazee.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza kwamba Matawi yake yanayojengwa yaendane na sifa ya chama hicho.
Alieleza kuwa Matawi mengi ya CCM yamefunguliwa lakini Tawi hilo liko vizuri na lina historia kubwa kisiasa hasa tokea wakati wa ASP pamoja na CCM.
Alieleza kuwa kuna nguvu kazi kubwa imefanywa na WanaCCM, kwani mchango mzuri umefanywa kwa nguvu kazi, viongozi pamoja na kutoa shukurani za pekee wka Rais Dk. Shein kwa mchango wake mkubwa wa ujenzi wa Tawi hilo.
Naibu Mabodi alisema kuwa Makamo Mwenyekiti huyo amekuwa na utamaduni wa kufanya alichokiahidi huku akieleza kuwa wananchi wa Ng’ambwa wamekuwa wakimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuweza kukaa pamoja na wananchi wa ngazi zote.
Alieleza kuwa CCM itaendelea kutoa ushirikiano wake kwani chama hicho kinaamini kwamba amani na utulivu ni jambo la pekee katika kuleta maendeleo, umoja na mshikamano.
Akisoma taarifa juu ya ujenzi wa Tawi la CCM Ng’ambwa Sharifa Maabadi Othman, kwa niaba ya Katibu wa Tawi la Ng’ambwa alisema kuwa Tawi hilo limeanzishwa mwaka 1957 chini ya Chama cha ASP na Mwenyekiti wake wa kwanza akiwa Marehemu Juma Hamadi Simai.
Alisema kuwa mara baada ya kuunganishwa ASP na TANU na kuundwa CCM uchaguzi wa mwanzo uliofanyika mwaka 1979 chini ya CCM na kupata Mwenyekiti wa CCM mpya ambaye ni Khatib Mussa Haji ambapo hivi sasa yupo Mwenyekiti Simai Ame Mkadam na kueleza kuwa chini ya uongozi wake Ng’ambwa itaendelea kuwa ngome ya CCM.
WanaCCM hao wa Uzi Ng’ambwa walimpongeza na kumshukuru Rais Dk. Shein kwa kusaidia ujenzi wa Tawi hilo kwa kuliezeka, kuweka madirisha na milango pamoja na umeme na hatimae kukamilisha ujenzi wa vyoo.
Sambamba na hayo, WanaCCM wa Ng’ambwa walitoa pongezi kwa wale wote waliowaunga mkono katika ujenzi wa Tawi hilo wakiwemo viongozi wa Jimbo hilo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Abdalla Juma Mabodi alitoa TZS Milioni moja zilizonunuliwa vifaa.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa wananchi wa Kisiwa cha Uzi Ng’ambwa wameridhika na uongozi wa Rais Dk. Shein hasa katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwani hatua aliyoifikia katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni zaidi ya asilimia 98.
Ilieleza kuwa yapo mambo ya maendeleo aliyoyasimamia Rais Dk. Shein katika utekelezaji wake ambayo hayakuwemo katika Ilani lakini kwa usimamizi wake mzuri wa kukuza uchumi wa Taifa ameweza kuyatekeleza bila ya msaada wa Taifa lolote.
Walieleza kuwa furaha kubwa ya wananchi wanaoishi Uzi na Ng’ambwa ni pale alipowaahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inawajengea daraja litakalorahisisha mawasiliano kati yao na wenzao walio nje ya kisiwa hicho.
Sambamba na hayo, wananchi hao wa kisiwa cha Uzi walieleza changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kumaliza tatizo hilo.   
Mara baada ya kumaliza uzinduzi huo wa Tawi la CCM Ng’ambwa wanaCCM na wakaazi wa kisiwa cha Uzi waliungana na Rais Dk. Shein kwa chakula maalum alichowaandalia  sambamba na burudani  murua ya Taarab kutoka kikundi cha Big Star vyote hivyo ikiwa ni shamrashamra ya sherehe za uzinduzi wa Tawi la CCM la Ng’ambwa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.