Habari za Punde

Ajali za Barabarani Zinaendelea Kutishia Maisha ya Wananchi Hasa Wakati huu Serikali ikiendelea na uimarishaji wa Miundombinu ya Bara bara pamoja na Mitaro ya Maji ya Mvua Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisoma Hotuba ya Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif ya Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani.
Baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif ya Kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi huko Chukwani.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ni jambo la kuhuzunisha kuona kwamba ajali za Barabarani zinaendelea kutishia Maisha ya Wananchi hasa wakati huu Serikali ikiendelea na uimarishaji wa Miundombinu ya Bara bara pamoja na Mitaro ya Maji ya Mvua Nchini.
Alisema Takwimu za hivi karibuni zimebainisha kwamba Watu wapatao 145 wamepoteza Maisha kutokana na ajali za Bara barani kuanzia Mwezi Januari  hadi Oktoba Mwaka huu ikionyesha uchambuzi wa kufariki kwa Watu 12 Kila Mwezi hali inayoleta wasi wasi mkubwa kwa Wananchi.
Akitoa Hoja ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi  Zanzibar  kwenye Majengo ya Baraza hilo Chukwani Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ajali hizo zimekuwa zikiripotiwa kika kukicha na hatma yake kuacha majonzi na simanzi.
Balozi Seif  Ali Iddi akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema hii ni hali ya kutisha na lazima umefika wakati wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kudhibiti ajali Bara barani ikiwemo kuhakikisha Mtu asiye na Leseni ya Udereva  haendeshi chombo cha Moto.
Ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia askari wake wa usalama Bara barani kuwadhibiti watu wanaoendesha Vyombo vya Moto wakiwa tayari wameshalewa sambamba na  kusimamia vilivyo matumizi ya alama za Bara barani na yule atakayekiuka taratibu hizo lamima aadhibiwe kwa mujibu wa Sheria.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema adhabu kama hizo kwa mujibu wa Sheria zinaapaswa pia kuwageukia Watu wanaojaribu kutaka kujiua wenyewe kwa njia tofauti ikiwemo kula dawa au sumu na wengine hujaribu kujinyonga kwa kutumia kamba au nguo.
Alisema hilo ni wimbi jipya la masuala ya udhalilishaji na unyanyasaji linaloendelea kuwa janga la Dunia ambalo kwa sasa linaonekana kuibuka na kuleta taharuki kwa upande wa Zanzibar .
Balozi Seif alitahadharisha na kuikumbusha Jamii kwamba Sheria za Nchi zinatambua kuwa tendo la kutaka kujiua ni kosa la jinai, hivyo ni busara wale wanaokumbwa na mchanganyiko wa mawazo wakaliepuka kwa kutafuta ushauri nasaha mapema utakaoleta amani ya roho kwao.
Akizungumzia  uadilifu wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Uwazi, Uwajibikaji, Maadili na Ukweli ni chachu ya mafanikio kwa Utumishi wa Umma na Taifa kwa jumla.
Balozi Seif aliwataka Watendaji wote wa Taasisi na Mashirika ya Umma Nchini kuzingatia na kufuata vyema uadilifu utakaowaongezea uchungu wa kuheshimua na kuthamini Rasilmali za Nchi na kuepuka kupanga mbinu za kuhujumu maeneo yao kwa kujibinafsisha kwa maslahi yao binafsi.
Aliwaomba Watendaji  wenye tabia hiyo  kuacha mara moja hulka hiyo na kuwataka wasimamizi wa Tume ya Maadili ya Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Utumishi wa Umma na Utawala Bora wajitahidi kufuatilia maadili ya Watendaji  na kuchukuwa hatua stahiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaomba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika Mpango wake Shirikishi wa Miakan 10 wa kupiga vita Maradhi thakili ya  Kipindupindu.
Alisema Mpango huo wenye lengo la kuondosha kabisa  usambazaji wa vimelea vinavyoeneza maradhi ya Kipindu pindu Zanzibar  umeipa fursa Wizara ya Afya Zanzibar kufanya Utafiti  wa Kitaalamu wa kubaini chanzo cha maradhi hayo.
Balozi Seif alisema Utafiti huo utasaidia kuelewa  maeneo hatarishi ya Kipindupindu Nchini na kupanga mipango ya kukabiliana na Ugonjwa huo utakaofanyika katika Wiloaya ya Mjini, Wilaya ya Magharibi “A”, Wilaya ya Magharibi “B”,  kwa upande wa Junguja na Wilaya ya Wete na  Micheweni kwa upande wa Kisiwa cha Pemba.
Katika Mkutano huo wa Kumi na Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar  Wajumbe wa Baraza hilo walipokea, kujadili hatimae  kupitisha Miswada Mitano ya Sheria ambayo ni pamoja na Mswada wa Sheria ya kuanzisha Ofisi ya Mufti, nambari 9 ya Mwaka 2001 pamoja na Mswada wa Sheria ya kuanzisha Wakala Serikali Mtandao, Kazi zake na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mengine ni Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake, Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usafiri Bara barani Nambari 7 ya Mwaka 2003 pamoja na Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Wakala wa Barabara Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Baraza la Wawakilishi limeahirishwa  hadi Jumatano ya Tarehe 5 Mwezi wa Pili Mwaka 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.