RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi la Skuli ya Biashara
Mombasa Zanzibar (kushoto kwa Rais) Mfadhili Mkuu wa Ujenzi wa Skuli hiyo kwa
kushirikiana na Serikali Mfanyabiashara na Mwakilishi wa Kuteuliwa Mhe. Ahmada Yahya
Abdulwakil na( kulia kwa Rais) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar.Mhe. Riziki Pembe Juma
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Sekta binafsi, ikiwemo
biashara zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mataifa mbali mbali
Duniani.
Dk. Shein amesema hayo katika ufunguzi wa jengo jipya la skuli
ya Sekondari ya Biashara iliopo Mombasa mjini hapa, ikiwa ni shamra shamra za
maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema mnamo mwaka 1980, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
iliondokana na mfumo wa kuhodhi biashara
na badala yake kujikita katika usimamizi wa sera na sheria, ili kutoa
fursa kwa wadau wa sekta hiyo kufanya shughuli hizo kwa mapana.
“Watu wa sekta binfasi ikiwemo biashara ndio wanaoimarisha
nchi zao duniani kote, serikali haiwezi ikafanya kila kitu”, alisema.
Alisema hatua ya wafanyabiashara kurejesha faida kwa wananchi,
hususan wanyonge, huleta baraka kubwa, akinasibisha kauli hiyo na hatua ya Mfanyabiashara Ahmada Yahya Abdulwakil aliefadhaili ujenzi wa jengo la skuli hiyo na
kusema ni miongoni mwa wafanyabiashara
weledi na wanaofanya vyema.
Alisema anawaheshimu wafanyabiashara ikiwemo wale wanaofanya
vyema shughuli zao kw auadilifu na hatimae kurejesha faida kwa jamii,
akibainisha kuwa biashara ni amali yenye
heshima kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kuwaendeleza vyema wanafunzi
wa skuli hiyo juu ya namna bora ya kufanya biashara ili waweze kulisaidia Taifa
na kueleza kuwa Taifa linahitaji wataalamu wa kutosha katika masuala ya uchumi.
“Uzinduzi wa skuli hii ulete tija kubwa baadae kwa kutoa
wataalamu wengi zaidi wa uchumi”, alisema.
Aidha, alisema mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya elimu hapa
nchini, kuanzia mwaka 1964 hadi sasa, yanalenga kuifikisha Zanzibar katika
maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye
mfumo wa kutoa elimu bure, huku ikilenga kupanua wigo wa hatua hiyo hadi
kufikia ngazi za Chuo Kikuu pale uchumi wake utakapoimarika.
“Kuna umuhimu wa kutafakari kwa kina vipi Serikali itaweza
kufikia malengo hayo”, alisema.
Alisema kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, elimu
ilihodhiwa na wakoloni, ambapo ni wazalendo wachache wenye uwezo ndio waliopata
fursa ya kusoma na kuliacha kundi kubwa la wazalendo bila ya kupata fursa hiyo.
Aidha, alisema elimu ilitolewa kwa ubaguzi kuambatana na makabila
ya watu, hivyo Waafrika waliikosa fursa hiyo, hadi mwaka 1935 pale skuli ya
mwanzo ilipoanzishwa kijiji cha Dole.
Rais Dk. Shein, alisema mara baada ya Mapinduzi ya 1964,
Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kupitia manifesto ya ASP, alitangaza elimu
bure nchini kote, hatua iliyotowa fursa kwa wananachi wote kusoma hadi kikomo
cha uwezo wao.
Katika hatua nyengine Dk. Shein alimpongeza mfadhili wa ujenzi
huo Ahmada Yahya Abdulwakil na kusema ni mfanyabiashara mzalendo, mkweli na muadilifu ambae amekuwa
akitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar, hususan kupitia sekta ya
elimu.
Mapema, Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma,
alimpongeza mfanyabiashara huyo kwa uzalendo na juhudi kubwa anazochukuwa
kuimarisha sekta ya elimu na kuwawekea mazingira bora ya masomo wanafunzi.
Aidha, alimpongeza Rais, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kufungua
milango ya uwekezaji kwa wazalendo na kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.
Nae, Mfanyabiashara.Mhe.Ahmada Yahya Abdulwakili ambae pia ni
Mwakilishi wa kuteuliwa, alisema kwa kushirikiana na Serikali amefanikisha
dhamira ya ujenzi wa jengo hilo ili kusaidia
juhudi za Serikali katika kuondokana na uhaba wa madarasa unaozikabili skuli
mbali mbali na kuwafanya wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
Aliipongeza Serikali, ikiwemo viongozi na watendaji wa Wizara
za Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Fedha kwa mashirikiano makubwa yaliofanikisha
kukamilika kwa ujenzi huo.
Aidha, alimshukuru Dk. Shein kwa kubainisha umuhimu wa
wananchi, ikiwemo wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa lao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dkt.
Idriss Muslim Hijja alisema ujenzi wa jengo hilo linalohusisha ghorofa mbili,
likiwa na madarasa tisa na ofisi mbali mbali za huduma za kitaaluma umegharimu
zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 hadi kukamilika kwake.
Alisema katika ujenzi huo Familia ya Mfanyabiashara Ahmada
Yahya Abdulwakil imechangia shilingi Milioni 900, wakati ambapo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imechangia zaidi ya shilingi Milioni 263.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaondoa
mrundikano wa wanafunzi katika madarasa, kutoka wanafunzi 49 kwa darasa hadi
kufikia 36 kupitia mkondo mmoja wa masomo.
Dk. Idriss aliwataka wadau wa elimu kote nchini kushirikiana
ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo,
sambamba na kuitaka jamii kuitunza skuli hiyo.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment