Habari za Punde

TANZANIA YAONGOZA AFRIKA MASHARIKI KWA KUFIKISHA MIUNDOMBINU YA UMEME VIJIJINI: SUBIRA MGALU


Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu, (kushoto) akipozi kwa picha na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Mhe. Jokate Mwegelo baada ya kupokea cheti cha shukrani kutoka kwa Mkuu huyo wa wilaya kwa ushiriki wake wa kuchangia kampeni ya "TOKOMEZA ZERO" inayolenga kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wilayani humo. Mhe. Mgalu alikuwa kwenye ziara ya kukagua upelekaji umeme kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji na majiji (periurban)  ambapo miongoni mwa maeneo yatakayofaidika na mradi huo ni taasisi za elimu.

NA  K-VIS BLOG, Khalfan Said, Kisarawe
NAIBU Waziri wa Nishati amesema Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kujenga miundombinu ya umeme vijijini.
Ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kukagua upelekaji wa umeme kwenye maeneo ya pembezoni mwa Miji na Majiji  (periurban) Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani Januari 23, 2020. Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendesha mradi wa periurban kwa majaribio katika baadhi ya maeneo ya Wilaya za Kisarawe,  Bagamoyo, Kibaha, Kigamboni na Ukonga jijini Dar es Salaam ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo kutumia umeme kwa bei nafuu ya shilingi elfu 27,000/= tu.
“Ilani ya uchaguzi 2015/2020 ilisema umeme usambazwe vijijini na jumla ya vijiji 8,500 kati ya 12,268 sawa na asilimia 67 ya vijiji vyote Tanzania vimefikiwa na miundombinu ya umeme.” Amefafanua Mhe. Mgalu ambaye katika ziara hiyo alifuatana na Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Hassan Said,  Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani Mhandisi Martin Madulu na viongozi wengine.
Mradi wa Periurban unapaswa kukamilika Juni mwaka huu 2020, na licha ya changamoto za hapa na pale, Mhe. Naibu Waziri amewahakikishia wakazi wa maeneo hayo kuwa miezi mitano kuanzia sasa wataanza kuwasha umeme kwenye maeneo hayo.
Katika Wilaya ya Kisarawe, jumla ya vijiji…………………..vitafaidika na mradi huo.
Amemtaka mkandarasi wa mradi huo kampuni ya Sengerema kuhakikisha kazi inakamilika katika kipindi cha miezi mitano kilichosalia na hakuna muda kuongezwa.
“Rai yangu kwa mkandarasi ni kufanya kazi usiku na mchana hakuna kulala, na wale suppliers wasambaza vifaa wa viwanda vya ndani vinavyozalisha nguzo, waya na transfoma, mita wapeni ushirikiano wakandarasi ili waweze kumaliza kazi zilizopo kwa wakati.”  Alisisitiza Mhe. Mgalu.
Mhe. Mgalu alisema katika mradi huu wa majaribio wa periurban unalenga kuwaunganishia umeme jumla ya wateja elfu 38,000 huku Wilaya ya Kisarawe na Ukonga maeneo 62 yatafaidika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Jokate Mwegelo ameipongeza TANESCO kwa kazi nzuri wanayoifanya Wilayani Kisarawe kuhakikisha huduma za upatikanaji wa umeme inakuwa bora na kwamba ongezeko la kiwango cha umeme wilayani humo litapelekea kuendelea kuing’arisha wilaya mbali na kuwafikishia umeme wananchi kwenye maeneo mengi ya vijijini lakini pia utasaidia kuweka taa za barabarani pia.
 Naibu Waziri akipokea cheti hicho kutoka kwa DC Mhe. Mwegelo.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu (kushoto), akijadiliana jambo na Meneja wa TANESCO Mkoani Pwani, Mhandisi Martin Madulu wakati wa ziara ya Mhe. Mgalu kukagua upelekaji umeme maeneo ya pembezoni mwa Miji na Majiji (periurban) wilayani Kisarawe Mkoani Pwani Januari 23, 2020.
 Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu, akipeana mikono na Meneja Mwandamizi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani Mhandisi Hassan Said mara baada ya kuzungumza na wananchi kwenye shule ya sekondari Christon iliyoko nje kidogo ya Mji wa Kisarawe Mkoani Pwani Januari 23, 2020 wakati akikagua upelekaji wa umeme kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji na majiji periurban
 Mhe. Subira Mgalu (katikati) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Mhe. Jokate Mwegelo na viongozi wengine akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua upelekaji umeme kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji na majiji (periurban) wilayani Kisarawe Januari 23, 2020.
Mhe. Mgalu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.