Katibu Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Hassan Abbasi (kushoto) akisitiza kwa viongozi wa menejimenti (hawapo pichani)kuwa
amedhamiria kufanya mageuzi ya kiutendaji alipofanya kikao na viongozi hao,baada
ya kuwasili katika ofisi ya wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba,Jijini Dodoma
baada ya kuapishwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt.John Pombe
Magufuli,kulia ni Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo Dkt.Ally Possi.
Katibu Mkuu Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Hassan Abbasi (kushoto) akipokea nyaraka
mbalimbali zinahusu ofisi ya Katibu Mkuu kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara
hiyo Dkt.Ally Possi ikiwa ni sehemu ya makabidhiano ya ofisi mara baada ya kikao na viongozi wa menejimenti
aliporipoti leo Jijini Dodoma.
Katibu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo Dkt.Hassan Abbasi (kushoto) akisalimiana kwa furaha na wafanyakazi wa wizara alipowasili katika ofisi ya wizara hiyo
iliyopo Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma,mara baada ya kuapishwa kwake jana
na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt.John Pombe Magufuli
Na
Anitha Jonas – WHUSM Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dkt.Hassan Abbasi amewataka viongozi wa
menejimenti wa Wizara hiyo kufanya mageuzi kwa kuwa sekta za wizara hiyo zimebeba ushawishi mkubwa kwa nchi na dunia.
Dkt.Abbasi ametoa
kauli hiyo Jijini Dodoma baada kuwasili katika ofisi ya wizara hiyo iliyopo Mji
wa Serikali Mtumba na kufanya mazungumzo na viongozi wa Menejimenti kwa lengo
la kupata taarifa fupi ya kisekta na makabidhiano ya ofisi.
“Wizara hii imebeba
sekta muhimu sana katika nchi ambazo ni soft
power na smart power mfano sekta ya Sanaa na Michezo ni burudani na sekta
hizi zikisimamiwa vizuri taifa hili litazidi kuwa la amani na furaha pamoja na uchumi
utaongezeka,tutaandaa matamasha ya kitaifa ya burudani kama JAMAFEST ambayo
yatashirikisha wasanii na wachezaji sisi ni watumishi wa umma lazima tuoneshe
wananchi utendaji wetu na ningependa tuache kufanya kazi kwa mazoea,”alisema
Dkt.Abbasi.
Akiendelea kuzungumza katika kikao hicho, Dkt.
Abbasi alisema kuwa anatarajia kuona utendaji wa pamoja (team work) na utendaji
wa kujituma pasipo kuchoka,pia alisisitiza anategemea kutumia vipaji na ubunifu.
Naye Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Dkt. Ally Possi alipokuwa
akifanya makabidhiano alimweleza Dkt. Abbasi changamoto mbalimbali za wizara
ikiwemo ya uhaba wa fedha katika uendeshaji wa Uwanja wa Taifa na pamoja na
Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuwa na changamoto katika
uendeshaji, umuhimu wa programu hiyo
sababu kuwa ni ya kimataifa na faida zake utakaposimamiwa vyema na kukamilika.
“Nakupongeza kwa mapinduzi
makubwa unayoyafanya katika Idara ya Habari hakika kazi ni nzuri haswa katika
kuisemea Serikali ningeomba kwa upande wa usimamizi wa taaluma ya habari na Vitengo
vya Mawasiliano Serikalini huko nako nguvu inahitajika ili kuwa na utendaji
wenye usawa katika uwajibikaji wenye tija,’’alisema Dkt.Possi.
Aidha, Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu, Bw.Marceline Patrick alimpongeza Katibu Mkuu huyo
na kumweleza kuwa watumishi wote wamefurahia uteuzi wake na wana imani nae
katika kusimamia mabadiliko ya sekta za wizara na wapo tayari kumpa ushirikiano
ili kufanikisha hilo.
Halikadhalika mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo kutoka
Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Bibi Hadija Kisubi alisema anamshukuru
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt.John Pombe Magufuli kwa kumteua
Dkt.Abbasi kuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo sababu ni mchapakazi na anaamini
kuwa atafanya mabadiliko makubwa katika wizara katika maeneo yote yenye
changamoto.
No comments:
Post a Comment