Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Tax Ikulu Jijini Zanzibar leo.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na mgeni wake Katibu Mtendaji wa SADC Dkt.Stergomena Lawrence, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo. 
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akimsikiliza mgeni wake Katibu Mtendaji wa SADC Dkt.Stergomena Lawrence, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na mgeni wake Katibu Mtendaji  wa SADC Dkt. Stergomena Lawrence Tax, alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika leo 21-2-2020 , katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana ili kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokabili nchi za ukanda huo.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Katibu Mtendaji wa SADC Dkt. Stergomena Lawrence Tax aliefika kwa ajili ya kusalimiana nae.

Alisema nchi wanachama wa SADC zinakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazofanana, zikiwemo za majanga pamoja na za kiuchumi, hivyo ni vyema zikashirikiana katika  kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Akigusia suala la  suala la majanga, Dk. Shein alisema  ni changamoto inayoikabili dunia nzima, ambapo hutofautiana kulingana na mazingira ya kimaeneo.

Alisema kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Menejment ya Maafa kwa nchi wanachama wa  SADC ni mwanzo mzuri katika muelekeo wa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto hizo.

Alisema Zanzibar kwa upande wake imeanza kulitafutia ufumbuzi tatizo la kutuwama kwa maji ambalo husababisha majanga, (hususan katika maeneo ya ng’ambo) kwa kujenga mitaro mikubwa inayopeleka maji moja kwa moja baharini.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuna haja kwa nchi wanachama wa SADC kutafakari namna gani zitakavyoshirikiana na kusaidiana katika dhana ya kuimarisha uchumi wa nchi zao, kwa kubadilishana uzoefu pamoja na uapatikanaji wa mafunzo.

Alisema kuna umuhimu wa nchi hizo kubadilishana bidhaa hususan zitokanazo na kilimo kwa njia ya kuuziana, ikiwa ni hatua itakayopunguza gharama.

Akigusia matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa nchi wanachama, Dk. Shein alisistiza umuhimu wa nchi za SADC kuwa na utaratibu na mikakati ya kuanza matumizi ya lugha hiyo, na kuipongeza Burundi kwa mafanikio iliyofikia katika matumizi ya kiswahili.

“Ni vyema kila nchi ikajitayarisha kutumia Kiswahili, lazima ianze kwa maeneo”, alisema.

Aidha, Dk. Shein alibainisha dhamira ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia Demokrasia nchini kwa kuzingatia sheria na Katiba za nchi.

Mapema, Katibu Mtendaji wa SADC Dkt.  Stergomena Lawrence Tax, aliishukuru Serikali kwa kukubabali kuaanda mkutano huo muhimu, hatua aliyosema inatokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika maendeleo na mustakbali wa Jumuiya hiyo.

Alisema hali ya ulinzi na usalama kwa nchi wanachama wa SADC ni nzuri mbali na kuwepo kwa matukio mbali mbali yanayojiri kabla na baada ya chaguzi.

Alishauri kutiliwa mkazo suala la upatikana wa ajira kwa vijana katika nchi wanachama ili kuondokana na kadhia mbali mbali zinazojitokeza.

Aidha, Dkt Lawrence aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Uongozi wa Dkt Shein kwa maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii iliyofikia, hivyo akabainisha azma ya SADC ya kuunga mkono juhudi  hizo.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.