Habari za Punde

TASAF Yatowa Elimu ya "Mpango wa Kutengeneza Biashara Rahisi" Kwa Wananchi wa Kajengwa Makunduchi.

Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Kanda ya Unguja Makame Ali Haji alieleza hayo wakati akizungumza wa wananchi wanaofaidika na mpango wa kunusuru kaya maskini Shehia ya Kajengwa Makunduchi Mkoa Kusini Unaguja.
Baadhi ya Wananchi wa wanaofaidika na mpango wa kunusuru kaya maskini wa Shehia ya Kajengwa wakiendelea na Mafunzo yao katika Skuli ya Kajengwa Makunduchi.
Na.Kassim Suleiman OMPR.
Jamii nchini imeshauriwa kuziunga mkono Serikali zao zote mbili ile ya Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la kupambana dhidi ya umaskini kwa wananchi walio wengi kupitia mpango wa kunusuru kaya Maskani Tanzania.
Mratibu  wa TASAF  Unguja Makame Ali Haji alieleza hayo wakati akizungumza wa wananchi wanaofaidika na mpango wa kunusuru kaya maskini huko Kajengwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja katika mafunzo maalum yaliyopewa jina “Mpango wa kutengeneza biashara rahisi”.
Mratibu Makame alisema serikali zote mbili bado zina azma ya kuuendeleza mpango huo kwa wananchi wake ili kuwawezesha kubuni miradi mingi zaidi itakayowasaidia kuwaongezea kipato kitakachokidhi kuendesha maisha yao kwa kutatua changamoto zinazowakabili zikiwemo zile za kijamii.
Alieleza katika muendelezo wa kuwapatia huduma bora wananchi kwa ajili ya kujiletea maendeleo Rais wa Jamuhuri wa Mungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli anatarajia kuzindua rasmi mpango wa kipindi cha pili  wa TASAF jijini Dodoma.
Alifafanua kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini umekuwa na tija kwa wananchi na kupelekea mpango huo kutekelezwa katika vikundi vinavyofikia 1,147 kwa kisiwa cha Unguja na kati ya idadi hiyo jumla ya vikundi tisa (9) vipo Kajengwa  na kupelekea vikundi hivyo kukusanya jumla ya shillingi Bilioni 2.7 fedha ambazo zinaendelea kuzunguka katika jamii.
Kwa upande wao wanufaika wa mafunzo hayo kutoka Kajengwa Bi Mpunga Simai Mussa na Bi Salama Rajabu Juma walieleza kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kubuni, kutengeneza pamoja na kutambua gharama za kuendesha miradi yao waliyoidhinisha.
Walisema mpango huo wa kunusuru kaya maskini una faida kubwa kwa jamii hivyo wametoa wito kwa wananchi wenzao ambao wataingizwa katika mpango huo wajipange vyema kuitumia fursa hiyo kutokana na mpango  unatoa nafasi kwa wanachi kubuni miradi wanayoitaka ambapo miradi hiyo inasaidia kutatua changamoto ndogo ndogo ikiwemo kukidhi mahitaji ya kusomesha watoto.
Nae Sheha wa shehia ya Kajengwa Ali Nahoda Ali alisema mpango huu umesaidia kuleta mabadiliko kwa wanajamii wa Kajengwa yaliyopelekea kwa sasa kuweza kunaza miradi yao ikiwa kwa mtu mmoja mmoja au katika njia ya vikundi.
Akielezea kufanikiwa kwa mafunzo hayo Muewezashaji kutoka TASAF Mwanamosi Ali alieleza kuwa asilimia kubwa ya mafunzo hayo yamewawaezesha wananchi wa Kajengwa kuwa na biasha zao hivyo  na kupata wasaa wa kuziimarisha kwa  kubuni mawazo tofauti yenye kutoa tija kwao wenyewe.
Wakati huo huo Mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wananchi wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini yamendelezwa  kwa walengwa wa shehia za  mkoa wa Mjini Magharibi yaliyofanyika katika ofisi za TASAF zilizopo Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.