SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuanzisha mfumo wa kielektroniki
ili kuvitambua vyombo vya moto vinavyotembea barabarani kwa lengo
la kuvifuatilia na kubaini madereva wanaokiuka sheria.
Akiwasilisha Ripoti ya utekelezaji wa
Maagizo ya Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi ya Mwaka
2019/2020 kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasilino na Usafirishaji, Waziri wa Wizara
hiyo Dkt. Sira Ubwa Mamboya amesema, katika kutekeleza suala hilo serikali imeanza
kutumia mfumo wa Kamera za CCTV zilizowekwa kwa matumizi ya mji salama ili
kubaini makosa ya usalama barabarani.
Aidha amesema Idara ya Usafiri na
Leseni inazipitia Kanuni mbali mbali za
usalama barabarani na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwachukulia hatua za kisheria madereva wote watakaobainika kufanya makosa
ya barabarani kwa lengo la kuwadhibiti
na kunusuru maisha ya wananchi na mali zao.
Wakati huo huo Mheshimiwa Dkt Sira
amesema, Serikali inaandaa utaratibu
wa faini za papo
kwa papo ili kuharakisha hukumu na
adhabu kwa madereva wazembe na
wanaokwenda kinyume na sheria za usalama
Barabarani.
“Serikali inaandaa utaratibu wa
kuwatoza faini watakaobainika kufanya makosa ya barabarani kwa njia za
kielektroniki ili kukusanya fedha hizo hapo hapo (barabarani) au kupitia kupitia Benki kwa kila atakaebainika kufanya
makosa” Alifafanua
mhe Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano na Usafirishaji.
Mheshimiwa Waziri amefahamisha kwamba
rasimu ya Kanuni hizo za adhabu ya papo
kwa papo imekamilika na kwa sasa ipo
wizarani kwa mapitio.
Akichangia hoja hiyo mjumbe wa Baraza
la Wawakilishi Jimbo la Magomeni Mhe Rashid Makame Shamsi ameishauri Wizara hiyo kuwashirikisha wadau wote wakati
wa utungaji wa Kanuni hizo ili kuondosha malalamiko wakati wa utekelezaji wake.
Divisheni ya Itifaki na Uhusiano
Baraza la Wawakilishi, Zanzibar.
Jumatano, Aprili 15, 2020
No comments:
Post a Comment