NA Himid Choko, BLW
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imesema imefanikiwa kupata mafanikio makubwa baada ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa
mapato na matumizi yake.
Akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa
Maagizo ya Kamati ya Kuchunguza na kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika
(PAC) ya Mwaka 2019/2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amesema
miongoni mwa hatua zilizopelekea
mafanikio hayo ni pamoja na kudhibiti
uvujaji wa mapato kutokana na kuimarisha mifumo yake ya ukusanyaji kwa kutumia
njia za kibenki na mitandao ya simu za mikononi.
Balozi Ramia amezitaja njia nyengine
zilizopelekea mafanikio hayo ni kufanya utambuzi wa walipa kodi kwa kutumia
mfumo wa kielektroniki pamoja na kufuatilia kwa karibu malimbikizo ya madeni
kwa wenye madeni ya kodi.
Aidha Balozi Ramia ameliarifu Baraza
la Wawakilishi kuwa Serikali hivi sasa iko katika hatua za mwisho za
kufanikisha utumiaji wa risiti za kielektroniki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wa matumizi ya Serikali,
Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amesema Serikali inaendelea kutoa mafunzo
kwa watendaji wa ngazi tofauti juu ya
uwepo wa Sheria mpya ya zinazohusiana na matumizi ya fedha za umma ili kulinda
fedha zake na hatimae zitumike vizuri na kwa tija zaidi.
Aidha amesema serikali pia inaendelea
kufanya ukaguzi wa ndani wa mifumo yake ya malipo na kufuatilia taarifa wa
wakaguzi hao.
Akitoa maoni ya Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti
Hesabu za serikali na Mashirika, Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Mheshimiwa Shaibu Said Ali amevishauri vyombo vya uchunguzi ikiwemo Mamlaka ya
kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi kuchunguza kwa kina madai ya malipo ya Kampuni ya Hassan & Sons yanayokihusisha Chuo Cha Mafunzo ambapo kwa mujibu wa Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za serikali ya Mwaka 2016/2017 hati ya malipo, maelezo pamoja na
vielelezo vya malipo hayo havikupatikana wakati wa ukaguzi huo.
Amesema malipo hayo yanatokana na
deni la mkopo wa pikipiki na vespa ambazo Kampuni hiyo iliikopesha chuo cha
Mafunzo.
Mwisho.
Himid Choko, BLW
Alkhamis , April 16, 2020
No comments:
Post a Comment