Habari za Punde

Uongozi wa CCM Mkoa wa Mjini Yakabidhi Vifaa Kupambana na Maradhi ya Corona Zanzibar.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizundua rasmi mpango wa ugawaji wa Vifaa vya kujikinga na Viirusi vya Corona vilivyotolewa na Uongozi wa CCM Mkoa wa Mjini.
Balozi Seif  akiwanasihi Wanachama wa CCM na Wananchi watakaobahatika kupata vifaa vya kujikinga na Virusi vya Corona ni vyema wakavitumia vizuri.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mjini Nd. Talib Ali Talib na Ujumbe wake akitoa maelezo mbele ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif kabla ya kuzinduliwa rasmi mpango wa ugawaji wa vifaa vya kujikinga na Corona.

Balozi Seif Ali Iddi akiupongeza Uongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Mjini kwa wazo lao la kuanzisha mpango wa ugawaji wa vifaa vya Corona kwa ajili ya Matawi yote ya Mkoa huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mjini Nd. Talib Ali Talib akimshukuru Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kwa kukubali kuungana pamoja na Uongozi wa Mkoa huo kwenye uzinduzi wa Mpango wa ugawaji vifaa vya kukabiliana na Virusi vya Corona.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Taifa litasalimika kupita katika wimbi la maambukizi ya Homa Kali ya Mapafu, Kikohozi, kupumua kwa shida kunakosababishwa na Virusi vya Corona endapo kila Mwananchi atakuwa makini katika kujilinda binafsi na janga hilo.
Alitanabahisha kwamba wapo baadhi ya Watu Nchini wameanza kujisahau na kuendelea na harakati zao za Kimaisha bila ya kuchukuwa tahadhari zozote za Wataalamu wa Afya pamoja na Viongozi ya kujiepusha na maambukizi ya Maradhi hayo ambayo bado yanazunguuka katika Jamii.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alisema hayo wakati akizindua Rasmi Kampeni ya Ugawaji wa Vifaa vya kujilinda na Maambukizi ya Virusi vya Corona vilivyotolewa na Uongozi wa CCM Mkoa wa Mjini kwa ajili ya kuvigawa ndani ya Matawi 59 yaliyono ndani ya Mkoa huo.
Alisema Virusi vya Corona licha ya kwa sasa kuzunguuka ndani ya Jamii  bila ya maambukizi ya nje lakini vinaweza kuondoka na kuwa Historia katika Visiwa vya Zanzibar kama kila Kiongozi, Mtendaji wa Taasisi ya Umma pamoja na Mwananchi atatimiza wajibu wake kwenye mapambano dhidi ya Virusi hivyo.
“ Corona hivi sasa haitafutwi bali inazunguuka na kupatikana ndani ya Jamii ambayo inapaswa kuwa na tahadhari katika kujikinga nayo” Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Balozi Seif  alibainisha kwamba Shirika la Afya Duniani {WHO} katika tafiti zake mbali mbali limeshabaini kwamba Ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona utaendelea kuwepo kama yalivyo maradhi mengine mfano Ukimwi licha ya jitihada zinazoendelea kuchukuliwa.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliupongeza Uongozi wa CCM Mkoa Mjini kwa jitihada ulizochukuwa wa kushirikiana na Serikali katika kusaidia mapambano dhidi ya Virusi hivyo thakili.
Aliwasihi Viongozi wa Matawi yatakayobahatika kupata msaada huo kuwaelekeza Wanachama wao kuvitumia vifaa hivyo na pale baadhi ya vifaa vidogo vidogo vitakapokwisha si vyema wakasubiriwa Viongozi wa Mkoa kutoa vyengine kazi itakayowajibika sasa kufanywa na Viongozi wenyewe wa Matawi.
Akitoa maelezo ya wazo la kubuni mpango huo wa ugawaaji wa Vifaa kwa ajili ya mapambano dhidi ya kupiga vita maambukizi ya Virusi vya Corona, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mjini Nd. Talib Ali Talib alisema Vifaa hivyo ambavyo ni ndoo pamoja na Sabuni vitatolewa kwa Matawi yote 59 yaliyomo ndani ya Mkoa wa Mjini,
Nd. Talib alisema Uongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini umeelewa na kufahamu umuhimu wa kupiga vita Virusi hivyo na ndipo ulipokuja na wazo la  kutafutwa vifaa vitakavyosaidia Wanachama wao ndani ya Matawi ili viwasaidie kujilinda na Corona.
Alisema Mwanachama  au Mwananchi ye yote atakayekwenda Ofisi na Majengo ya Chama kufuata huduma atalazimika kunawa mikono kabla ya kuingia kwenye Majengo hayo ili iwe kinga ya kujieousha na virusi vya Corona vinavyozunguuka ndani ya Mitaa kwa wakati huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.