WANANCHI wameipongeza hotuba ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyotoa kwa wananchi kupitia
vyombo vya habari ikiwa ni salamu zake za sikukuu ya Idd El Fitr hivi karibuni.
Wananchi hao walieleza
kufarajika na salamu hizo alizozitoa Rais Dk. Shein katika hotuba yake hiyo na kusisitiza kuwa
wamezipokea mikono miwili na watazifanyia kazi hasa wito alioutoa juu ya
kuendeleza mafunzo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Walieleza kuwa Rais
Dk. Shein ameonesha kuwajali kwani licha ya kuwepo kwa janga la COVID-19 lakini amefanya juhudi za makusudi
za kuhakikisha anazifikisha salamu zake kwa wananchi wake anaowaongoza kupitia
vyombo vya habari.
“Kwa jambo hili lazima
tumpongeze Alhaj Dk. Shein kwa kutupa
salamu za Idd el Fitr wananchi wake kwa kweli tumefarajika sana hasa pale
alipotutaka tuendeleze vazi la uchamungu, Allah atamlipa kwa hili”,alisema
Nwagili mkaazi wa Ubago Cheche.
Wananchi hao waliongeza
kuwa hatua zake hizo zimeonesha kuwa Rais Dk. Shein ni kiongozi anaewajali
wananchi anaowaongoza pamoja na kuwa na kiu ya kutaka wananchi wake waishi kwa
upendo, amani, utulivu na maelewano zaidi.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti wananchi hao walimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa wataendelea
kumuunga mkono yeye na Serikali anayoiongoza na wale wote ambao hawapendi
maendeleo ya Zanzibar pamoja na kukebehi juhudi zinazochukuliwa ni vyema wakapuzwa na badala yake wamemtaka
Rais Dk. Shein endelee kuchapa kazi.
Walieleza kuwa tokea
kuanza kwa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona duniani na hadi kuingia
visiwani Zanzibar, Rais Dk. Shein amekuwa mstari wa mbele katika kuwapa
maelekezo mazuri wananchi wake pamoja na matumaini makubwa katika kupambana na
janga hilo sambamba na kuwatoa hofu.
Wakiwa katika maeneo
mbali mbali kwa nyakati tofauti wananchi hao wameipongeza hotuba ya Rais Dk.
Shein na kumpongeza yeye mwenyewe binafsi kwa yale yote aliyoyasema katika
hotuba hiyo ambayo wamesema wamepata matumaini makubwa hasa baada ya kusikia
kuwa Serikali inakusudia kuregeza masharti iliyoyaweka.
Katika pongezi hizo
pia, wananchi hao wameipongeza misimamo yao thabiti ya Rais Dk. Shein pamoja na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ya kutozifunga
nyumba za ibada kwa hofu ya ugonjwa wa COVID-19 ambapo waumini wameweza kufanya
ibada zao vyema ikiwemo sala ya Idd el Fitr.
Kwa upande wake
Sheikh Fadhil Suleiman Soraga aliisifu na kuipongeza hotuba ya Rais Dk. Shein na
juhudi anazozichukua na kueleza kuwa hotuba hiyo imekusanya mambo yote muhimu na
kusisitiza kuwa kitendo cha Rais kuwatakia heri ya Idd el Fitr wananchi wake ni
kitendo cha kiungwana ambacho kinafaa kupongezwa.
Wananchi hao pia,
walieleza azma yao ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuimarisha uchumi, kudhibiti mapato na kuzilinda rasilimali
mbali mbali ikiwa ni njia moja ya
uaminifu na kufanya uadilifu.
“Hapa Rais Dk. Shein
amepigilia msumari aliposema wananchi ni lazima tuepuke kufanya vitendo viovu
kama vile vya uonevu na hujuma ambavyo vinaweza kutupeleka katika mustakabali
mbaya ambayo yote hayo ni mafunzo ya saumu, nampongeza kwa kusisitiza hili
katika hotuba yake”, alisema Khamis Ame mkaazi wa Donge Pwani.
Aisha Ahmada Ali
mwalimu wa skuli ya Migombani alipongeza hotuba ya Rais Dk. Shein hasa pale
aliposema kuwa Serikali kwa upande wake itahakikisha kwamba inaendelea
kuwapatia wafanyakazi fursa za kujiendeleza kwa elimu na ujuzi zaidi ili
kuwajengea uwezo.
Nae Mkufufunzi kutoka Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba kutoka
(SUZA) Mohammed Sharksy aliipongeza
hotuba ya Rais Dk. Shein hasa shukurani alizozitoa kwa madaktari na wataalamu
wa afya ambao tangu yalipoanza maradhi ya COVID-19 wamekuwa wakifanya juhudi
kubwa za kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuwapa huduma walioathirika au wale
walioonesha dalili.
Nao baadhi ya wananchi mbali mbali Kisiwani Pemba
wametoa pongezi zao kutokana na hotuba ya Idd el Fitr aliyoitoa Dk. Shein
kupitia vyombo vya habari na kusema kwamba iliojaa hekima na busara kubwa ikiwa
ni pamoja na kuendeleza hatua za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Wamesema hotuba hiyo imewaondoshea hofu wananchi
wa Zanzibar juu ya janga hilo na kueleza
kuwa tamko la kuangalia uwezekano wa kupunguza masharti linaonesha jinsi
anavyowajali wananchi wake.
Walieleza kuwa kila siku Dk, Shein, amekuwa
akihimiza Wananchi kuchukuwa tahadhari juu ya maambukizo hayo kwani anaelewa athari
za kuwepo kwa wagonjwa wengi nchini.
Hata hivyo, walisema ni wajibu wa kila mwananchi
kuona umuhimu wa kuchukuwa tahadhari zilizoelezwa na Rais Shein katika
kujikinga na maradhi hayo na sio kupuuza kwani mgonjwa mmoja anaweza kuwaambukiza
watu wengi na kwa wakati mmoja.
Bwana Juma Salum kutoka Wete Pemba, alisema
kiongozi mzuri ni yule anaewahimiza wafuasi wake kutenda mambo mema kwa maana
hiyo kitendo cha Rais Dk. Shein, cha kuwataka wananchi kuendelea kufanya mema
waliojifunza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kuonesha mapenzi kwa
anaowaongoza.
“Ni wazi kwamba Rais wetu amekuwa mstari wa mbele
kila mara katika kutuhimiza sisi wananchi wake kufanya mema na kitendo cha
kutuhimiza tuendeleze mafunzo ya mwezi wa Ramadhani ni kuonesha uadilifu wake
kwa sisi anaotuongoza,”alisema Juma.
Akizungumzia kwa namna Rais Shein, alivyosikitika
kutokana na wananchi wake kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakiwa
wamekabiliwa na mitihani ya janga la COVID-19 sambamba na mafuriko kutokana na
mvua kubwa ilionyesha inaonesha wazi juu ya kiongozi huyu anavyowajali wananchi
wake.
“Tumepokea salamu zake za pole alizozitowa katika
hotuba yake hiyo na hii inatupa moyo kuwa Serikali inayoongozwa na Dk, Shein
iko pamoja na wananchi wake kwa hali yoyote inayowatokea kwa kweli tunampongeza
kwa kutufariji,”alieleza.
Nae Mohammed Khamis Ali, mkaazi wa Chake Chake
alisema kuwa hotuba ya Rais Dk. Shein ilikuwa na kila aina ya ujumbe kwa wananchi
wa Zanzibar na Tanzania nzima kwani ilijaa nasaha ambazo hata kwenye dini ya
Kiislamu zimo na hii inaonesha jinsi Dk. Shein alivyokuwa Mcha Mungu na
alivyobobea katika elimu ya dini ya Kiislamu.
“Mimi kwa nafsi
yangu nampongeza Dk, Shein kwa namna anavyoonesha kuguswa na mambo mbali mbali
yanayowapata wananchi wake yakiwemo maradhi, mafuriko, ukosefu wa huduma muhimu
kama maji safi na salama ” alieleza Mohammed Khamis.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment