Habari za Punde

Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar Yafanyika Pemba na Kuongezeka Kwa Asilimia 50 Kwa Kampuni za Bima Visiwani Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika viwanja vya Gombani Chake chake Pemba kuhudhuria Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar akiwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliofanyika Kitaifa Kisiwani Pemba leo 30-6-2020.
Baadhi ya Wananchi na Wadau wa Sekta za Bima Nchini wakijivinjari kwenye moja ya burdani za Vikundi vya Utamaduni vilivyotumbuiza katika Maadhimisho ya Siku ya Bima Gombani Chake Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akipokea Tuzo Maalum aliyotunukiwa kutoka kwa Naibu Kamishna wa Malaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania {TIRA} Bibi Khadija Issa Said kutokana na mchango wake mkubwa kwa Taasisi za Bima.
Balozi Seif akikabidhi moja ya miongoni mwa Nishani Kumi na Moja zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania {TIRA} kwa wadau wa Bima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia kwenye Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Gombani Chake Chake Pemba.
Baadhi ya Viongozi wa Taasisi zinazotoa huduma ya Bima Zanzibar wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyofanyika katika Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar Hapo Gombani Kisiwani Pemba.

Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ongezeko kubwa  la makusanyo ya ada za Bima kutoka Shilingi Bilioni Tatu {3,000,000,000/-} kwa Mwaka 2015 hadi kufikia Shilingi Bilioni 13,000,000,000/- Mwaka 2019 limeonyesha dhahiri kwamba Sekta ya Bima ikishirikiana na wadau wake inaweza kusaidia kukuza Maendeleo hapa Nchini.
Alisema makusanyo hayo ya fedha za ada yameonyesha na kushuhudiwa kwa ongezeko kubwa la asilimia 50%  kwa Kampuni za Bima zilizofunguwa Matawi yake Visiwani Zanzibar.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Bima Zanzibar yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Michezo wa Gombani Chake Chake Kisiwani Pemba.
Alisema Sekta ya Bima imeliwezesha Taifa kupata mafanikio katika Nyanja za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii, jambo lililotoa mchango wa moja kwa moja katika kukuza pato la Taifa, Ajira, Uwekezaji na utopaji wa Elimu kwa Jamii juu ya majanga na athari zake.
Balozi Seif alieleza pamoja na kuwepo kwa ongezeko la ada za Bima, ulipaji wa fidia nao umeimarika kutoka shilingi Milioni 349 kwa Mwaka 2015 hadi shilingi Bilioni 2.8 kwa Mwaka 2019.
Alifahamisha kuwa hiyo inadhihirisha wazi kuwa Kampuni za Bima zinatekeleza wajibu wake kwa kumrejesha mnufaika wa Bima katika hali yake ya awali baada ya kukutwa na majanga.
Hata Hivyo Balozi Seif  aliwahimiza Watendaji wa Mamlaka na Mashirika ya Bima kutoa fidia zote stahiki kwa mlenga pale tu baada ya kukamilika kwa uhakiki na tathmini ya aina ya janga lililompata bila ya kuwepo viashiria vya rushwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Umma kuzingatia uaminifu na uwazi pale inapohitajika  huduma hizo ili kusaidia sekta ya Bima Nchini katika kukabiliana na majanga, na kutoa fidia stahiki kwa wahanga wa matukio mbali mbali ikiwemo ajali za aina zote.
Alisisitiza Mamlaka za Bima zina wajibu wa kutoa elimu kupitia vyombo vya Habari ili Wananchi wapate uelewa juu ya umuhimu wa Bima sambamba na kuhamasisha Wananchi wakate Bima kwa mali zao wanazomiliki zenye thamani kubwa.
Aliwakumbusha Watendaji wa masuala ya Bima wahakikishe Mwananchi aliyekata Bina hasumbuliwi kuhusu stahiki yake, Mamlaka ikiwa tayari kutekeleza wajibu wake  wa kusimamia sekta hii kwa haki na weledi huku kiwalinda Wananchi na mali zao kwa mujibu wadheria ilkiyowekwa.
Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha Viongozi wa Bima kuwa makini na watu wasio waaminifu ambao wakati mwengine huamua kuzichoma moto kwa makusudi mali wanazozimiki katika maeneo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa ombi kwa Taasisi za Serikali, Wananchi na Wafanyabiashara wa Zanzibar kuamini Kampuni zote za Bima zilizosajiliwa na Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania na kutumia huduma za Bima.
Aliyaagiza Makampuni na Wataalamu wa Bima kuendelea kutoa huduma na Elimu ya Bima kwa Wananchi kwa namna rahisi zaidi kupitia Mitando ya simu, Mabenki pamoja na Semina.
Balozi Seif alisisitiza juu ya utoaji wa huduma bora za Bima na salama kwa njia zisizo rahisi kwa lengo la kuwafikia Wananchi wengi pamoja na usimamizi madhubuti wa Mkampuni ya Bima yaliyosajiliwa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Watendaji wa Bima Kisiwani Pemba kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kukifanyia kazi kilio chao cha kupatia Ofisi ya Mamlaka ya Bima Kisiwani Pemba.
Alisema hii inatokana na Serikali kuthamini mchango wa jitihada zinazotolewa na Mamlaka ya Bima pamoja na Washirika wake katika kuendeleza harakati za Kiuchumi na Maendeleo ya Watanzania.
Balozi Seif ali Iddi  amewaagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa yote ya Zanzibar kuyahakiki Magari yote ya Taasisi za Serikali kama yamekatiwa Bima kwa Mujibu wa Sheria zilizopo zinazoelekeza magari hayo kukatiwa Bima.
Alisema Taasisi zote za Serikali zimekuwa na utamaduni wa kuomba na hatimae kupewa vifungu vya Fedha  ndani ya Bajeti za Mwaka kwa ajili ya vyombo vyake vya Moto vinavyotembea Bara barani, Majini na Baharini.
Balozi Seif alitanabahisha kwamba haipendezi kuona kwamba utaratibu huo hautekelezwi licha ya kuwemo ndani ya SDheria na Taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akitoa Taarifa kutokana na maadhimisho hayo Naibu Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania {TIRA} Bibi Khadija Issa Said alisema kila chombo cha Moto kinachotembea bara barani, Baharini pamoja na Angani lazima kikate Bima kwa mujibuwa Sheria iliyowekwa.
Bibi Khadija alisema wapo Watu wengi Nchini wanaotumia vyombo vya Moto  hasa vile vinavyotumia Bara bara mara nyingi huamua kuendesha vyombo hivyo bila ya kuzingatia ukataji wa Bima na matokeo kupata matatizo yenye utata kwenye ulipaji wa fidia.
Alisema Makampuni ya Bima kupitia Taasisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imechukuwa jihudi za kuwaelimisha Wananchi hasa Vijana umuhimu wa kukata Bima sambamba na kuendesha Vyombo kwa kuzingatia sheria za Bara barani ili kuepuka ajali.
Naibu Kamisha huyo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania alielezea matumaini yake kutokana na mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi na Makampuni ya Bima  katika kusaidia kukuza uchumi wa Taifa sambamba na kustawisha Mwananchi Mmoja Mmoja.
Bibi Khadija alisema zipo baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa shughuli za Bima akazitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa Wadau wa Bima unaokwenda sambamba na ukaidi wa wakata Bima hasa vyombo vya Magurudumu Mawili.
Katika kuimarisha Mapato ya Taifa, ongezeko la Ajira na ufanisi katika eneo la Bima Bibi Khadija aliiomba Serikali Kuu kutoa fursa kwa Makampuni yote ya Bima kwa vile yanayotoa huduma sawa.
Akitoa salamu za Mikoa Miwili ya Pemba pamoja na kumuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimkiwa Hemed Suleiman Abdullah kuwaomba Wananchi licha ya Serikali Kuu kuruhusu Shughuli za Kiserikali na zile za Kijamii kurudi katika uhalisia wake wanapaswa kuzingatia muongozo wa Wataalamu wa Afya.
Mh. Hemed alisema Kisiwa cha Pemba kimeonyesha kuwa Kituo maarufu cha Biashara kutokana na kuongezeka kwa harakati za Kibiashara baada ya uwepo wa Taasisi za Bima ambazo ni chachu ya Maendeleo kwa Mapato ya Taifa yanayoambatana na ustawi wa Mwananchi Mmoja Mmoja.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba alielezea faraja yake kutokana na kasi kubwa ya ongezekola Mashirika ya Bima Mawili kati ya Kumi yanayotoa huduma Zanzibar pamoja na Mawakala Watano ndani ya Kisiwa cha Pemba.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata wasaa wa kuangalia Maonyesho  mbali mbali ya harakati za Bima zinazotekelezwa kila siku na Taasisi 13 za Bima hapa Zanzibar.
Maonyesho hayo yalikwenda sambamba na kukabidhiwa  Nishani kwa Washindi waliofanya vyema katika utoaji wa huduma za Bima Nchini Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.