Habari za Punde

Upepo mpya, kivuli kilekile kivumbi cha urais Zanzibar 2020

LEO inatimia wiki moja tangu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitangaze kufungua pazia kwa wanachama wake kuchukua fomu ya kuwania urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Visiwani Zanzibar. 


Tayari Rais Dk. John Magufuli ambaye anawania muhula wa pili amekwishachukua fomu ndani ya chama hicho kuomba ridhaa kumpitisha kuwania urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kwa ujumla  na pengine kwa utamaduni wa CCM, anayewania muhula wa pili mara nyingi huwa hakutani na vigingi sana tofauti na inavyokuwa wakati wa kuwania mara ya kwanza na ndiyo hali inayoonekana kwa upande wa Zanzibar, baada ya Rais wake Dk. Mohamed Shein kumaliza muhula wa pili. 

Tayari idadi ya watia nia nafasi ya urais Zanzibar kupitia CCM,  imefikia 14. 

Baadhi ya makada waliojitokeza katika Ofisi Kuu za CCM zilizopo Kisiwandui mjini Unguja kuchukua fomu za  kuomba kupewa ridhaa ya CCM kugombea nafasi hiyo ni pamoja na aliyekuwa  Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha. 

Yumo pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk.  Hussein Mwinyi, ambaye amejitosa kwenye kinyang’anyiro  hicho kwa staili ile ile aliyoitumia Magufuli mwaka 2015. 

Hussein Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alijitokeza  kimyakimya katika ofisi za CCM,  Kisiwandui na kuchukua fomu kama alivyofanya Magufuli mwaka 2015 ambaye hakutaka kuzungumza na waandishi wa habari tofauti na wagombea wengine. 

Ukimwacha Mwinyi wengine waliochukua fomu ni Mbwana Bakari Juma, mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar,  Balozi Ali Karume, Mbwana Yahaya Mwinyi na Omari Sheha Mussa. 

Wengine ni Jenerali mstaafu Issa Suleiman Nassor, Mohamed Jaffar Jumanne na Balozi Mohamed Hijja Mohamed. 

Kwa idadi hiyo iliyojitokeza ndani ya wiki moja tu kwa upande wa Zanzibar, watu wanaofuatilia siasa wanasema  huenda wengi zaidi wakajitokeza katika siku zilizobaki. 

Itakumbukwa wakati Rais Jakaya Kikwete akielekea kumaliza muda wake, makada takribani 40 walijitokeza kuomba ridhaa ya CCM kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 

Japokuwa mchuano ulikuwa mkali kati ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe lakini jina la Magufuli ni kama lilipita katikati yao na hatimaye CCM ikampitisha kuwania nafasi hiyo. 

Pamoja na kwamba idadi hiyo ndiyo ilijitokeza hadi sasa visiwani Zanzibar, yapo majina mengine ambayo yamekuwa yakitajwatajwa kumrithi Dk. Shein. 

Miongoni mwao ni pamoja Waziri wa Maji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na Waziri wa Viwanda upande wa Zanzibar, Balozi Amina Ali ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alijitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuingia tano bora akichuana na Magufuli. 

Yumo pia  aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo Machi 3, mwaka huu baada ya kile kilichoelezwa kukaidi agizo la chama chake la kutoanza kampeni kabla ya wakati. 

Wengine  pia wanaotajwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Abood, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussi Gavu, na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan japo yeye mwenyewe aliishawahi kukanusha huko nyuma. 

Pengine kutokana na ubashiri huo, huenda wiki itakayoanza kesho na kuendelea yakashuhudiwa majina hayo au mengine mapya. 

RATIBA 

Ratiba inaonyesha mgombea urais wa Zanzibar zoezi la uchukuaji fomu kutafuta wadhamani na kurejesha inafanana na ile ya nafasi ya urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Juni 15 -30. 

Julai 1- 2  Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar itaketi kuchuja majina ya wale waliojitokeza kuwania nafasi ya kugombea urais visiwani humo. 

Julai 3- kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili Zanzibar kitaketi kwa ajili hiyo hiyo.

Julai 4- Kikao cha Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM kitatoa mapendekezo ya wanachama waliojitokeza kuomba kugombea urais wa Zanzibar. 

Julai 9-Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa kupendekeza majina matatu ya waliotia nia ya kuwania urais kupitia chama hicho. 

Julai 10- Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM kuchagua jina moja la mgombea wa chama hicho. 

Julai 11 – 12, Mkutano Mkuu wa CCM utathibitisha jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa urais Zanzibar. 

Atakayetangazwa na CCM kuwania nafasi hiyo atapambana na wagombea wengine wa upinzani. 

Ingawa bado haijajulikana ni kwa namna gani wapinzani wataamua kusimamisha mgombea wake lakini ni wazi uchaguzi wa sasa mgombea wa CCM atakabiliana na wagombea wa upinzani zaidi ya mmoja. 

Hilo linatokana na migawanyiko iliyojitokeza hasa ndani ya chama cha CUF ambacho kwa miaka mingi kimekuwa kikitikisa siasa za visiwa hivyo. 

Jabali la siasa za upinzani Visiwani Zanzibar aliyekuwa akikibeba CUF kwa mbeleko imara na hata kufanikiwa kukitikisa CCM kwa miaka yote, Maalim Seif Sharif Hamad sasa yupo chama kingine  cha ACT- Wazalendo baada ya mgogoro mkubwa na Mwenyekiti wake Prof. Ibrahim Lipumba unaonekana wazi kukisambaratisha chama hicho. 

Maalim Seif na timu yake iliyokuwa ikitikisa siasa za Zanzibar  wapo chama cha ACT- Wazalendo ambacho katika uchaguzi wa mwaka 2015 hakikuwemo kwenye ushirika wa muungano wa vyama vya upinzani ambao ulitikisa kura za urais na nafasi nyingine visiwani humo. 

Muungano huo ambayo ulibebwa na nguvu ya Maalim Seif  na timu yake, kama akina Babu Duni Haji, Ismail Jussa na wengine visiwani humo ulikuwa ni wa vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD. 

Ukiacha CUF, vyama vingine vilivyokuwa vimeingia katika muungano huo havikuwahi kuwa na nguvu ya kufurukuta visiwani humo kama ilivyo kuwa kwa CUF ya Maalim Seif. 

Wanaokumbuka kilichotokea mwaka 2015 na hata Tume ya Uchaguzi (ZEC) iliyokuwa chini ya Jecha Salum Jecha ikalazimika ama kupenda au kutopenda kuitisha uchaguzi wa marudio, hawatapinga kwamba mgombea atakayepatikana kwa upande wa CCM, atakuwa na kibarua cha kupambana safari hii kwa namna na staili nyingine na Maalim Seif Sharif Hamad. 

Ikitokea Maalim Seif atagombea au hatagombea tena urais kwa tiketi ya upinzani, kivuli chake bado kuna kila dalili ya kuendelea kutesa hata baada ya CUF kubaki vipande vipande. 

Vivyo hivyo, vyama vingine vya upinzani hususani CUF ambayo imebaki na makovu hakuna ubishi nacho kitasimamisha mgombea wake si tu kukabiliana na CCM bali pia kivuli au Maalim Seif mwenyewe. 

Chadema nacho kimeanzisha mchakato visiwani humo, lakini ni mapema kutabiri mwelekeo wake kutokana na mikakati  na staili ya siasa zake za kitafiti na matokeo ya kisayansi hasa nyakati za uchaguzi na zaidi jina la Maalim Seif ambaye ilishirikiana naye mwaka 2015 linapokuja mbele yake katika siasa za visiwani humo. 

CCM ITAKUBALI MAKOSA? 

CCM inaonekana kujipanga tena upya ikiwa na uzoefu mwingine baada ya Zanzibar kulazimika kufanya chaguzi mbili mwaka 2015 baada ya ule wa kwanza Maalim Seif kudai alishinda dhidi Dk. Mohammed Shein. 

Hatua hiyo ambayo ninaweza kusema kwamba ilitia doa, makosa ya namna hiyo itakuwa ni dhambi kubwa kwake safari hii. 

Tayari  huko nyuma kumekuwa na vikao vingi kati ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli na Makamu wake upande wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. 

Hivi karibuni siku chache kabla ya mchakato wa uchukuaji fomu kuanza walikutana na kufanya mazungumzo siri. 

Kukutana kwa nyakati tofauti kwa viongozi wao kulijenga hisia kwamba mazungumzo huenda yalikuwa ni ya nani anastahili na mwenye sifa za kurithi viatu vya Dk. Shein na kuwa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane. 

Hisia nyingine ya vikao hivyo vya viongozi hao ni kupatikana kwa mgombea ambaye atashindana na vyama vingine vya upinzani ili chama hicho kibaki salama bila mpasuko na zaidi kusababisha makosa ya nyuma. 

Kwa mara kadhaa viongozi hao wa juu wamekuwa wakikutana na kujadili masuala kadhaa kuhusu hatima ya CCM na majaliwa yake kuelekea Uchaguzi Mkuu. 

Juni 3, mwaka huu, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, Rais Magufuli alikutana na Rais Dk. Shein, katika kikao cha ndani kilichofanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma. 

Kikao hicho ilielezwa kuwa kilihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally, kuzungumzia masuala ya chama hicho. 

Majadiliano hayo yaligusia masuala kadhaa ikiwamo kufanyika kwa Mkutano Mkuu ambao utateua mgombea urais unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.