Habari za Punde

Walimu wa Skuli za Msingi na Maandalizi Wapata Mafunzo ya Maandalizi ya Mawanda Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Eng.Idrisa Muslim Hija akizunguka katika hafla ya Ufunguzi wa Warsha ya uandaaji wa "Mawanda na Mtiririko wa Mihutasari ya Elimu ya Maandalizi na Msingi" iliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Jijini Zanzibar, iliowashirikisha Walimu wa Skuli za Msingi na Maandalizi .

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Idrisa Muslim Hija, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo mitaala katika Skuli ili kuwasaidia Wanafunzi kusoma kwa utaratibu na kufikia malengo ya kupata Elimu bora.

Akizungumza wakati alipofungua warsha ya uandaaji wa "Mawanda na Mtiririko wa mihutasari ya Elimu ya Maandalizi na Msingi" katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo, Dkt Idrisa  amesema ni vyema kuwa makini katika kazi hiyo ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Amesema warsha hiyo ya uandaaji wa mawanda (scope), inafanyika ikiwa Sera ya Elimu bado haijakamilika, lakini haitoathiri shughuli hiyo kutokana na kuwa ipo katika hatua ya mwisho.

Aidha Dkt Idrisa amewataka washiriki hao kujikubalisha kwa muda wote watakao kuwepo katika warsha hiyo kwa kuzingatia kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu, wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw Suleiman Yahya Ame amesema lengo la kufanya warsha hiyo ni kuandaa maudhui ya kumpa Mwanafunzi kwa kuzingatia umri wa mtoto ili kuwa na utaratibu bora wa Elimu  na kwenda sambamba na ukuaji wa Elimu nchini.

Amesisitiza kuwa katika kazi hiyo ni vyema kuzingatia sera ya Elimu iliopo, sheria, ilani ya Chama tawala, miongozo pamoja na kuangalia mtaala unaoendelea ili kupata mtaala uliobora zaidi.

Hata hivyo ametaka katika somo la historia kuweka maudhui yenye mantiki kwani ndio somo muhimu kwa  watoto katika kuzijua historia mbalimbali hasa ya nchi na kuwafanya kuwa wazalendo wa nchi yao.

Akiwasilisha mawazo ya wadau mbalimbali juu ya  mtaala uliopita, mfumo wa mtaala mpya pamoja na mawanda ya mtiririko wa mihutasari ya uandishi wa mtaala mpya wa Elimu ya Maandalizi na Msingi, Kaimu Meneja Idara ya Mitaala na Vifaa Wizara wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mwalimu Abdalla Mohd Mussa amesema imeonekana kuwepo mambo ya Msingi ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwemo wingi wa masomo katika Elimu ya Maandalizi na Msingi na pia kusomeshwa mwananfunzi somo lisilo na uwezo kwao.

Warsha hiyo ya siku kumi, imeandaliwa na Taasisi ya Elimu Zanzibar  na imewashirikisha baadhi ya Walimu wa Skuli za Maandalizi na Msingi kwa Skuli za Serikali na Binafsi kwa Unguja na Pemba.
Washiri wa Warsha ya mafunzo ya Maandalizi ya Mawanda wakimsikilia Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Eng. Idrisa Muslim Hija akifuingua mafunzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Jijini Zanzibar.
Muwezeshaji wa Mafunzo ya Mawanda akitowa mada kuhusiana na maandalizi ya Skuli za Msingi na Maandalizi kwa ajili ya muhtasari wa mtirieiko wa maandalizi ya Elimu Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.