Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akitembelea jengo la Hoteli ya Kitalii inayojengwa katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Ndg. Hassan Mohammed Raza, alipofanya ziara kutembelea ujenzi huo ukiwa katika hatua za mwisho za ujenzi huo.
Meneja wa Operesheni wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar{AAKIA} Nd. Haji Haji akimpata maelezo Balozi Seif jinsi vitengo mbali mbali vitakavyotoa huduma kwa Wageni wasafiri watakaokuwemo kwenye Hoteli hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiupongeza Uongozi Mzima wa Makampuni ya Royal Group kwa uamuzi wake wa kujenga Hoteli ya Kimataifa itakayohuduma wasafiri wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Royal Group Ndugu Hassan Mohammed Raza Kushoto akimuonyesha Ramani ya Hoteli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alipofanya ziara fupi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifanya ziara fupi kukagua Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya Golden Tulip Airport Hoteli pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Royal Group Ndugu Hassan Mohamed Raza.
                                                        Picha na OMPR
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezishauri Kampuni za Uwekezaji katika Sekta ya Biashara kuangalia uwezekano wa Kujenga Hoteli ya Kitalii katika Uwanja wa Ndege wa Pemba kwa lengo la kutoa huduma kwa wasafiri na hata Wananchi wanaotumia Uwanja huo.
Alisema mfumo wa huduma za Mahoteli unaokuwepo katika Viwanja mbali mbali vya Ndege Duniani hulenga kuwaondoshea usumbufu Wasafiri wa  Anga kuzitafuta huduma hizo maeneo ya Mijini kwa vile baadhi ya Viwanja hivyo huwepo Ng’ambo ya Miji.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo alipofanya ziara fupi ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya  Golden Tulip Airport Hotel iliyopo pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ulio chini ya Kampuni ya Royal Group.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi zake za Uwekezaji ina nia ya kuona fursa ya ujenzi wa Hoteli ya Kitalii katika Uwanja wa Ndege wa Pemba inachangamkiwa na Wafanyabiashara wenye uwezo kwa kuanzisha Mradi huo muhimu unaoweza kutoa huduma sambamba na ajira kwa Vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi mzima wa Kampuni ya Royal Group kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mradi huo Mkubwa utakaosaidia kuongeza Pato la Taifa, huduma kwa Wasafiri na kwa upande mwengine Ajira kwa Wananchi Wazalendo.
Mapema akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika maeneo mbali mbali ya Jengo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Royal Group Ndugu Hassan Mohammed Raza alisema ujenzi huo unaotarajiwa kuchukuwa Miezi 16 utakamilika ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Ndugu Hassan alisema ujenzi wa jengo hilo litakalokuwa na Vyumba 62 vya kulala, eneo la kuegesha magari 150 kwa wakati Mmoja linatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 7.5 sawa na fedha za Kitanzania Zaidi ya shilingi Bilioni 17.1.
Mkurugenzi Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba pamoja na mambo mengine Uongozi wa Royal group umezingatia huduma za Michezo kwa kuweka Bwawa maalum la kuogelea pamoja na sehemu za mazoezi kwa wale wasafiri wanamichezo.
Alisema Mradi huo utakapokamilika utatoa huduma kwa Wasafiri wa Anga wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kwa kuzingatia umuhimu wa usalama wa Abiria unaokwenda sambamba na vile vigezo vya Viwanja vya Ndege vya Kimataifa.
Naye Meneja wa Operesheni wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar      {AAKIA} Nd. Haji Haji alisema vifaa Maalum vitawekwa katika Hoteli hiyo vitakavyosimamiwa na Watendaji wa Taasisi zote zinazohusika na masuala ya Uwanja wa Ndege katika kuona Msafiri anapata huduma zinazostahiki.
Nd. Haji alisema usafiri wa Mabasi utawekwa kwa ajili ya kuwahudumia abiria wanaokuwemo ndani ya Hoteli hiyo na kuwafikisha kwenye mlango na ndege wanazosafiria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.