Habari za Punde

MAJALIWA: BANDARI YA KAREMA IJENGWE USIKU NA MCHANA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili katika eneo la  Karema  wilayani Tanganyika kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Bandari
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipoweka jiwe la msinngi la ujenzi wa  bandari ya Karema wilayani Tanganyika Julai 4, 2020. Wengine kutoka kushoto ni  Mbunge wa Mpanda  Vijijini,Moshi Kakoso, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Juma Homela, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandii Isack Kamwelwe, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzani, Masanja Kadogosa  na  kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa bandari ya Kasanga wilayani Tanganyika kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi  wa bandari hiyo, Julai 4, 2020. Kushoto kwake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Karema wilayani Tanganyika, Julai 4, 2020. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Xiamen Ongoing Construction Group inayojenga  Bandari ya Karema kwa gharama za zaidi ya sh. bilioni 47 ifanye kazi usiku na mchana na  kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Congo.

Pia, Waziri Mkuu ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Wizara ya Madini na wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la Ikola ili kuhudumia wageni wanaotoka Congo.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumamosi, Julai 04, 2020) baada ya kuweka jiwe la msingi la  ujenzi wa Bandari ya Karema inayojengwa kwenye ziwa Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika, Katavi. Alisema mkandarasi anatakiwa ahakikishe mradi huo unakamilika haraka.

Waziri Mkuu alisema mradi huo unalenga kuongeza tija katika shughuli za kibandari kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ndani na nje ya nchi na kwamba utaongeza fursa za kibiashara nchini na pia utakuwa chachu ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

“Tumeamua kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na kushusha abiria na mizigo kwa wakati mmoja. Hii ni Serikali ya kuahidi na kutekeleza na ni Serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi ya falsafa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Dkt. Baraka Mdima alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa gati kubwa la kufungia meli lenye urefu wa mita 150 pamoja na kingo ya kuzuia mawimbi makali, uchimbaji wa kuongeza kina cha lango la kuingilia bandarini na sehemu ya kugeuzia meli.

Alisema eneo jinguine ni ujenzi wa miundombinu ya bandari ikiwemo mgahawa, jengo la kupumzikia abiria, majengo ya ofisi, eneo la sakafu ngumu kwa ajili ya kuhifadhia makasha pamoja na miundombinu ya Zimamoto na Tehama. Mradi huo utazingatia ujumuishi wa Reli ya Kisasa (SGR).

“Mradi unajengwa kwa miezi 24 na kukamilika kwa bandari ya kisasa ya Karema, kutaboresha shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Katavi na Tanzania kama kusafirisha watu na bidhaa katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi jirani za Congo, Burundi na Zambia.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera aendelee na operesheni ya kuwasaka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.“Watu wote wanaomiliki silaha bila ya kuwa na vibali watafuwe popote walipo na wachukuliwe hatua za kisheria.”

Awali, Waziri Mkuu alizungumzia upatikanaji wa umeme katika wilaya ya Tanganyika, alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote nchini, hivyo waendelee kuwa na subira.

“Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme na amepunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000 ili kila mwananchi aweze kumudu gharama hizo.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa licha ya gharama za kuunganishiwa umeme kupunguzwa, pia wananchi hatolazimika kulipia gharama za nguzo pamoja na gharama za fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari zimeshalipiwa na Serikali.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 05, 2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.