Habari za Punde

Mama Asha Balozi: Watoto yatima wanastahiki kupendwa zaidi


Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza katika Dua Maalum ya kuwaombea ambayo ilihudhuriwa na Watoto yatima wa Wilaya ya ya Kaskazini  “B” iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi ya CCM Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Mahonda.
Baadhi ya Watoto Yatima waliohudhuria Dua Maalum ya kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki iliyoandaliwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya Kusaidia Jamii na Maendeleo na Hayat Foundation ya Nchini Uturuki.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar {Zardefo} Sheikh Sleyum Jumbe akijiandaa kumkaribisha mgeni rasmi kuzunguza wa washiriki wa Dua maalum ya Wazazi waliotangulia mbele ya Haki.
Watoto Yatima wakifuatilia hotuba za Viongozi mbali mbali kwenye Dua maalum ya Wazazi waliotangulia mbele ya Haki iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi ya CCM Mkoa Kaskazini Unguja uliyopo Mahonda.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar {Zardefo} Sheikh Ali Haji Mohamed akiongoza Dua Maalum ya kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki hapo Mahonda na kushirikisha Watoto Yatima wa Wilaya ya Kaskazini B.
Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Jamii na Elimu ya Hayrat Foundation Sheikh Adnan Kushoto akimkabidhi zawadi Maalum Mama Asha Suleiman Iddi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyekuwa Mgeni Rasmi katika Dua Maalum ya Kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki.

Baadhi ya Watoto Yatima waliohudhuria  Dua Maalum ya Kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuioya ya kusaidia Jamii na Maendeleo { Zardefo} na ile ya Hayrat Foundation ya Uturuki.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Mke wa Makamu wa Makamu wa Pili wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi amewakumbusha wanajamii kuelewa kwamba Watoto yatima wanastahiki kupendwa zaidi ndani ya Familia ili kuwapa moyo na nguvu za kuondokana na mawazo ya kufikiria kupoteza Wazazi wao waliotangulia mbele ya haki.

Mama Asha alitoa kumbusho hilo wakati wa Dua Maalum ya kuwaombea Wazazi waliotangulia mbele ya Haki ambayo ilihudhuriwa na Watoto yatima wa Wilaya ya ya Kaskazini  “B” iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi ya CCM Mkoa Kaskazini Unguja iliyopo Mahonda.

Dua hiyo iliyoambatana na Chakula cha Mchana imeandaliwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar { ZARDEFO} kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo na Elimu ya Hayrat Foundation kutoka Nchini Uturuki.

Mama Asha Suleiman Iddi alisema zipo changamoto kadhaa zinazowakumba Watoto Yatima ikiwemo manyanyaso na udhalilishaji wa kupindukia mipaka unaofanywa na baadhi ya Wazazi na hatimae hupelekea kuzitia doa Familia zinazowalea Watoto hao wanaohitaji uangalifu Maalum wa kiimani.

Alisema Waumini na Wanaadamu lazima wakumbuke kwamba kumtesa Mtoto Yatima ni sawa na kukanyaga kaa la moto lisilofahamika ukali wake. Hivyo  wahusika wa vitendo hivyo lazima wajiandae na adhabu kali iumizayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo hata akitaka kutubu haitamsaidia lolote wakati unapowadia.

Mama Asha Suleiman Iddi ameishukuru Jumuiya ya Kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar {Zardefo} na ile ya Hayrat Foundation ya Nchini Uturuki kwa jitihada zinazochukuwa katika kusaidia ustawi wa Wana Jamii katika maendeo mbali mbali Nchini.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya kusaidia Jamii na Maendeleo Zanzibar {Zardefo} Sheikh Sleyum Jumbe alisema Taasisi ya Maendeleo ya Elimu na Jamii ya Nchini Uturuki imefanya kazi kubwa katika kuunga mkono Jumuiya yao kwenye masuala mbali mbali ya Kijamii.

Sheikh Sleyum alisema jitihada za Hayrat Foundation  zimeongeza nguvu zilizopelekea kuimarika kwa miradi ya Maendeleo, Uchumi na Kijamii katika maeneo mbali mbali na hatimae kuleta ustawi mkubwa  wa Wananchi hasa wale wa maisha ya kawaida Vijijini.

Akitoa salamu katika Dua hiyo Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Jamii na Elimu ya Hayrat Foundation Sheikh Adnan alisema Sekta ya Elimu inayotiliwa mkazo na Taasisi yao hulenga  kutanua wigo  wa Elimu inayomfungulia Mwanaadamu mwanga wa mafanikio katika maisha yake ya Dunia  na milele.

Sheikh Adnan alisema Taasisi yake itaendelea kuunga mkono harakati za kijamii za Wananchi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba Jamii za Watu wa Uturuki na Zanzibar zinalingana kabisa Kiutamaduni, Mila na hata tabia.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za Maendeleo Sheikh Adnan aliahidi kwamba Hayrat Foundation imejitolea kujenga Skuli Moja kubwa hapa Zanzibar ili kutoa elimu kwa Vijana endapo watapaka eneo  kwa ajili ya kutoa sadaka kwenye mradi huo muihimu wa Kielimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.