Habari za Punde

TAMWA yawataka akinamama waliotelekezwa kutokata tamaa




Muhammed Khamis,TAMWA-Zanzibar

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-Zanzibar kimewataka baadhi ya akinamama ambao wametelekezwa na waume zao kutokata tamaa badala yake wajikite katika uzalishaji wa bidhaa mbali mbali ili waweze kujikwamua kimaisha.

Kauli hio imetolewa na Afisa masoko Muhidini Ramadhan wakati alipokua akizungumza na akinamama hao katika ofisi za Chama hicho zilizopo Tunguu Wilaya ya kati Unguja katika hafla maalumu ya kuwakabidhi vifaa ambavyo vitaumika kwa ajili ya uzalishaji wa sabuni. 

Aliwataka akinamama hao kutumia vyema fursa hio ya kupatiwa vifaa ili waweze kuzalisha bidhaa hizo za sabuni ambazo anaamini zitawaingizia kipato na kuweza kujikimu.

Alieleza kuwa kwa muda mrefu wapo baadhi ya akinamama kwenye familia mbali mbali wamekua wakikumbwa na hali ya utelekezwaji na kupelekea kuhangaika wao na watoto.

Awali Meneja miradi wa Chama hicho Asha Abdi Makame aliwataka akinamama hao kutumia vyema nyenzo hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Alisema ni wajibu wao kuhakikisha wanazalisha bidhaa bora ambazo zitauzika sokoni na hatimae kuweza kupendwa na walio wengi.

‘’Nendeni mkatumia vifaa hivi kwa uangalifu mkubwa na msiwe tayari kutumia kwa matumizi mengine yasiokusudiwa kwa kuwa vinaweza kuharibika mara moja’’aliongezea.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya wanaufaika wa msaada huo walisema umekuja wakati muafaka ambapo wanahitaji kuungwa mkono.

Walisema wao kama wanawake wanaojitegemea katika shughuli za kila siku wamekua wakikabiliwa na changamoto za hapa na mpale hivyo inapotokea taasisi kuwasaidia hufarijika sana.

Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na trea ya kutengezea sabuni pamoja na dawa maalumu ambazo hutumika katika utengenezaji wa bidhaa hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.