Habari za Punde

Ameahidi Nafasi Nyingi za Uteuzi Watapewa Kapaumbele Wanawake.


Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi akizungumza wakati wa hafla ya Kongamano la UWT 2Umoja Wetu Wanawake Ndio Nguvu Yate" lililofanyika katika ukumbi wa Afisi ya CCM Mkoa wa Mjini Kichama Amaniu Jijini Zanzibar. 

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi ameahidi kuwa nafasi nyingi za uteuzi katika Serikali atakayoiunda ya Mapinduzi ya Zanzibar wanawake watapewa kipaumbele kwani ndio nguzo ya chama hicho.

Dk. Hussein aliyasema hayo leo wakati akitoa salamu katika Kongamano maalum la Wanawake lililofanyika katika ukumbi wa Amani CCM Mkoa, ambapo Mgeni Maalum katika Kongamano hilo alikuwa Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein na Mgeni Rasmi alikuwa Mwenyekiti wa (UWT) Gaudentia Mugosi Kabaka.

Katika salamu zake hizo, Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa anauhakika mkubwa kwamba CCM itashinda kutokana na wagombea wake wa uongozi kuungwa mkono na makundi yote ndani ya chama hicho wakiwemo wanawake ambao ndio jeshi kubwa la CCM.

Alisema kuwa wanawake wamekuwa wakifanya vizuri pale wanapopewa nafasi ya uongozi kwani wamekuwa wakionesha uadilifu wao mkubwa.

Dk. Hussein alieleza kuwa katika kampeni zote za CCM wahamasishaji wakubwa ni wanawake ambao mara zote wamekuwa kitu kimoja katika kukiunga mkono na kukitetea chama chao cha CCM.

Aliongeza kuwa umefika wakati wagombea wote wanawake wa  CCM waliogombea nafasi mbali mbali zikiwemo za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kuwa kitu kimoja ili kuhakikisha chama chao kinaendelea kuongoza dola na kupata ushindi wa kishindo.

Katika salamu zake hizo Dk. Hussein Mwinyi alitoa wito kwa wanawake kuendelea kukitetea chama hicho na kuhakikisha kinapata ushindi na kuweza kuongoza Serikali.

Aidha, Dk. Hussein alieleza kuwa kampeni kubwa za chama hicho zitafanywa majukwani lakini zaidi zitafanywa katika mikutano ya ndani.

Sambamba na hayo, Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza haja ya kuendelea kuitunza amani kwani bila ya amani hakuna maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.