Habari za Punde

MAADHIMISHO YA SIKU YA MAAFA DUNIANI

Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar                  13/10/2020.

MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Hassan Khatib Hassan, ameitaka jamii kufuata utaratibu wa mipango miji wakati wa ujenzi wa nyumba za makaazi, ili kuepukana na athari za maafa zinazochangiwa na ujenzi holela.

 

Aliyasema hayo   wakati alipokuwa  akizungumza katika Siku ya maafa duniani ambayo hufanyika kila ifikapo Oktoba 13 ya kila mwaka ghafla hiyo imefanyika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil  Kikwajuni Mjini Zanzibar.

 

Alisema kuwepo kwa matukio mengi ya maafa visiwani humu mara nyingi huchangiwa na ujenzi holela, ambao husababisha njia za kupitia maji kipindi cha mvua kuziba na kupelekea maafa.

 

Alisema umefika wakati kwa wananchi kutambua kuwa tatizo la maafa si suala dogo, kwani athari zake ni kubwa kwa jamii na serikali kwa ujumla, hivyo kuna kila sababu ya wananchi kujiepusha kufanya makosa.

 

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa alisema mbali ya wananchi kutakiwa kuchukua tahadhari, lakini taasisi zinazosimamia masuala ya majenzi ikiwemo Halmashauri, Manispaa na Taasisi nyengine kutekeleza vyema majukumu yao ili kuepuka tatizo hilo.

 

 

Alisema umefika wakati kwa watendaji hao  kuacha tabia ya kukaa ofisini bila ya kufanya ukaguzi, akiweka wazi kwamba kufanya hivyo ni kuondoshea jamii kuepukana na athari na kupunguza gharama zinazoweza kuepukika zinazotolewa na Serikali kwa wahanga wa maafa.

 

Hata hivyo alisema  bado mashirikiano ya pamoja yanahitajika kwa wadau wa Kamisheni ya kukabiliana na maafa ili kutekeleza muongozo wa utoaji wa elimu kwa wananchi ikiwemo  taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa.

 

Nae Mkurugenzi  Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatib Makame alisema Kamisheni hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo mbali mbali pamoja na.kuandaa vipeperushi na makala.

 

Aidha alisema Kamisheni hiyo imefanya ukaguzi katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kuangalia mipango na utaratibu wa kukabiliana na maafa katika maeneo yao .

 

Aliyataja baadhi ya maeneo yaliokaguliwa ni pamoja na vituo vitano vya kuuzia mafuta Pemba,  kituo cha kuuzia gesi Masingini pamoja na maeneo yanayokaa maji yakiwemo Bwawa la Mwantenga A na B na ziwa maboga.

 

Alisema kufuatia ukaguzi huo imebainika kuna baadhi ya majengo yamekosa mfumo sahihi wa kukabiliana na maafa ikiwemo milango ya dharura, alama na michoro inayoonesha maeneo salama na kukosa maeneo ya kukusanyika wakati wa dharura ama maafa.

 

Alisema Kamisheni imeanzisha namba ya dharura 190 kupitia mitandao ya Zantel, Tigo na Airtel ambapo wananchi wanapata fursa ya kupiga simu bure na kupatiwa huduma stahiki katika kukabiliana na maafa mbali mbali nchini.

 

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya siku ya Maafa duniani mwaka huu “Utawala bora kupunguza athari za maafa.”


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.