Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Shein Amuombea Kura Mgombea Urais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi Kwa Wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwahutubia Wananchi wa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika mkutano wa Kampeni ya Mgombea Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Mhe.Dk. Hussein Mwinyi, uliofanyika katika viwanja vya mpira Chwaka leo 10-10-2020. 

MAKAMO Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisisitiza haja ya kumpa kura nyingi Dk. Mwinyi ili aendelee kuyalinda na kuyadumisha Mapinduzi ya Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 pamoja na kuulinda Muungano uliopo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Chwaka, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini  Unguja katika Mkutano wa Kampeni za CCM ambapo pia, aliwahutubia wanaCCM pamoja na wananchi wote sambamba na kuwaombea kura na kuwakabidhi nakala za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 wagombea wote wa CCM wa Wilaya hiyo ya Kati.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa CCM akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha, Wake wa viongozi wakiongozwa na Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa chama hicho.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza kuwa Dk. Mwinyi ameusimia vyema Muungano wakati akiwa Waziri katika Ofisi ya Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa heshima yake ni kubwa na ameshiriki vizuri katika vikao vya Muungano na kusisitiza kuwa nafasi ya Urais anaiweza.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Dk. Hussein Mwinyi aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa muda wa vipindi vitatu, Mjumbe wa Kamati Kuu kwa vipindi viwili na amekua na mchango mkubwa kwenye chama “Wasiojua nawambia yeye ni mgongwe ndani ya CCM”, alisisitiza Dk. Shein.

Alisema kuwa kuhusu suala la amani, umoja na mshikamano yeye ni hodari sana hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hivyo, anamatumaini makubwa kuwa Dk. Mwinyi ataiongoza vyema Zanzibar.

Kwa upande wa nidhamu na heshima Rais Dk. Shein alisema kuwa Dk. Mwinyi anachukia rushwa na ubabaishaji kazini, ni msimamizi mzuri kwenye kazi kwani amefanya kazi nae na anajua jinsi alivyokuwa akifanyakazi, “Upole, uvumilivu na ustahamilivu ni sifa ya utawala bora”, alisisitiza Dk. Shein.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliwapongeza wanaCCM kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo na kueleza kuwa madhumuni makubwa ya kukusanyika katika mkutano ni kwenda kuwaombea kura viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo.

Alisema kuwa wagombea wote wa Wilaya hiyo pamoja na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM wana uwezo mkubwa na uzoefu wa kukiongoza chama hicho na kukipigania na wala si wanagenzi bali ni weledi kwa kila nafasi walizogombea.

Aliongeza kuwa viongozi hao wanauwezo mkubwa sana na uzoefu wao unawapa nafasi wanaCCM na wanachama wengine wawachague kwa kishindo na wako tayari kuwatumikia wananchi na wanaCCM katika Baraza la Wawakilishi, Bungeni na katika Halmashauri zao.

Kwa upande wa mgombea wa Urais, Rais Dk. Shein alisema kuwa mgombea huyo wa nafasi ya Urais wa Zanzibar ameanza kazi ya kuwatumikia wanaCCM kwa kuielezea Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar na amekuwa akielezea kwa ufasaha yaliyomo, yatakayofanyika na yaliyofanyika.

Aliongeza kuwa tayari ameshakutana na makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali, waendesha bodaboda, wafugaji, wavuvi, wakulima na wengineo na amekuwa akikutana nao na kuwaeleza ahadi za CCM katika kuongoza nchi.

“Dk. Mwinyi ni chaguo letu na CCM imemchagua kwani ana nguvu kubwa ya kisiasa na anaungwa mkono sana na Zanzibar na Tanzania kwa jumla tunasikia mengi juu ya sifa za Dk. Mwinyi”, alisema Dk. Shein.

Aliwataka wananchi na wanaCCM wa Chwaka na Wilaya hiyo ya kati kuendelea kuiunga mkono CCMi kwani hiyo ni ngome iliyokuwa tangu wakati wa ASP na leo ni ngome ya CCM kwani hata katika uchaguzi wa Januari 1961 Jimbo la Chwaka lilichukuliwa na ASP hivyo, Jimbo hilo ni ngome ya chama hicho.

Hivyo, Rais Dk. Shein aliwataka wanaChwaka waoneshe kwa vitendo kuwa wao wanahistoria kubwa katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotokana na ASP na TANU.

Sambamba na hayo, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alimuombea kura Dk. Magufuli pamoja na mgombea wake mwenza Samia Suluhu Hassan, Dk. Hussein Mwinyi, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani wote wa CCM.

Nae Dk. Hussein Mwinyi kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Shein kwa Utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 90.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba imefanya mengi ikiwemo ujenzi wa skuli za kisasa katika Wilaya hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa elimu ndio msingi wa maisha na kumpongeza Rais Dk. Shein kwa jitihada zake hizo.

Pia, alimpongza Rais Dk. Shein katika uongozi wake kwa kujengwa skuli za ghorofa 26 zenye zana zote za kujifunzia, madawari, na vifaa vyote muhimu.

Kwa upande wa sekta ya afya, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuanza kwa  mradi wa hospitali ya Binguni na kuahidi kuwa Awamu ya Nane ijayo itaulamilisha mradi huo.

Alisema kuwa Hospitali ya Binguni atahakikisha ujenzi wake unakamilika na wananchi wanapata huduma zote za afya.

Kwa upande wa mradi maji km. 7.6 kutoka Bambi hadi Uroa mradi uliowaondoshea wananchi adha ya kupata maji  huku akieleza kuwa kwa upande wa na miundombinu, Dk. Hussein alisema kuwa kazi iliyofanywa ni kubwa na kila mtu anaona kwani nchi yote imefunguka kwa barabara za lami.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, alisema kuwa kilimo cha mpunga ni kikubwa katika Wilaya hiyo, hivyo alisema kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kimeimarishwa kutoka  hekta 110 hadi hekta 892 mradi ambao unaendelea na utekelezaji wake.

Alisema kuwa licha ya mafanikio hayo pia, zipo changamoto ambazo Awamu ya Nane itazitatua na kuziondoa kabisa ikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi, maeneo ya kufanyia shughuli, pamoja na kuyatenga maeneo ya wafugaji na wakulima.

Aliongeza kuwa katika sekta ya ardhi, Awamu ya Nane itaangalia namna ya matumizi ya ardhi na kuahidi kuweka mipango mizuri ya ardhi.

Alisema kuwa baadhi ya matatizo yanasababishwa na wawekezaji na kusema kuwa Awamu ijayo inataka viuongozi watakaowajibika kwa wananchi na kuhakikisha kila kiongozi anawajibika na wanao lega lega hatua zitachukuliwa juu yao.

Dk. Hussein alisema kuwa kunatakiwa kuwepo na maeneo maalum ya uvuvi, na utalii, kwani lengo ni kuhakikisha rasimali za nchi haziharibiki.

Akieleza kuhusu uvuvi haramu katika maeneo tengefu alisema kuwa doria zitaendelea kufanyika kwani tatizo kubwa ni ukosefu wa vyombo vya kisasa jambo ambalo litawezeshwa ili uvuvi uwe na tija.

Alieleza kuwa tatizo la ajira kwa vijana litapatiwa ufumbuzi kwani Serikali ijayo inataka kujenga uchumi mpya wa kisasa ambao utatatua tatizo la ajira kwa vijana ambao uchumi wnyewe utakuwa ni uchumi wa buluu.

Kwa upande wa ajira alisema kuwa tayari ajira laki tatu zimetengwa kwa hivyo hana wasiwasi na kusema kuwa uchumi unaokuja ni uchumi wa kisasa wa utalii wa kisasa, uvuvi mkubwa ukiwemo wa bahari kuu, ufugaji wa samaki na usindikaji wa samaki katika viwanda sambamba na bandari maalum za uvuvi.

Akieleza kuhusu ukosefu wa soko la matunda na mboga, Dk. Hussein alisema kuwa  wajasiriamali wa aina zote Serikali ijayo itahakikisha wanasaidiwa kupitia mfuko maalum wa uwezeshaji ambao utakuzwa ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ili wafanye kazi kwa weledi, zana, masoko na mazingira ya kazi.

Hivyo, aliwataka wajasiriamali wa aina zote kuondoa hofu kwani mambo mazuri yanakuja. “Yajayo yanafurahisha na ni neema tupu kwa Wazanzibari”,alisema Dk. Hussein.

Alisema kuwa kwa upande wa viwanda kadhaa vitajengwa kwa ajili ya kuwapatia wajasiriamali soko zuri pamoja na ajira.

Kwa upande wa miundombinu, alisema kuwa barabara zilizobaki zitamalizwa lakini kazi kubwa itafanywa katika kuzijenga barabara za ndani.

Alieleza kuwa kwa upande wa malisho ya mifugo kutakuwa na mipango mizuri ya ardhi hasa ikizingatiwa kuwa nia na dhamira ya serikali ya Awamu ya Nane ni kuhakikisha tija inapatikana.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa soko atahakikisha Wilaya ya Kati inapata soko lake huku akieleza kuwa kwa upande wa changamoto ya Maji, Jumbi, Ungujaa, Charawe na Ukongoroni na kuahidi kuwa atahakikisha kwamba huduma hiyo inapatikana kwa wananchi wote kwani serikali ya awamu ya saba imefanya kazi.

Kwa upande wa kulinda misitu ambayo inakatwa alisema kuwa juhudi zitafanywa ili waweze kufanya kazi mbadala kwa kuwaoa mtaji, masoko na kuwapa kazi nyengine ili kuilinda misitu hiyo.

Sambamba na hayo, kwa upande wa uwezeshaji, Dk. Mwiyi alisema kuwa eneo hilo atalipa kipaumbele na kuwaondoa watu katika umasikini unaowakabili.

Kwa upande wa amani alisisitiza ni lazima kuilinda amani, na kusisitiza kuwa amani na utulivu iliyopo ni pamoja na kuwepo kwa Muungano uliopo na vikosi vya Muungano vimekwua vikifanya kazi kubwa ya kulinda Amani.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi alimpongeza Dk. Hussein Mwinyi kwa kuwafuata wananchi kuomba kura na kukiombea chama chake kwa kwenda mtaa kwa mtaa, kijiwe kwa kijiwe, makundi kwa makundi na mtu kwa mtu.

Alisema kuwa wanaCCM wataendelea kuhubiri amani, umoja na upendo huku akieleza kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao wanahubiri siasa za ubaguzi wazi wazi jambo ambalo halikubaliki na jamii.

Alisisitiza haja kwa wanaCCM kwenda kupiga kura siku ya Oktoba 28 mwaka huu bila ya kukosa ambapo pia, alitumia fursa hiyo kumkaribisha Balozi Ali Karume ambaye kwa upande wake alimuombea kura Dk. Hussein Mwinyi, Dk. Magufuli pamoja na viongozi wengine wote wa CCM.

Alisema kuwa CCM ina historia kubwa hapa Zanzibar na imefanya mambo mengi tokea uhuru wa Januari 12, 1964.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Ramadhan Abdalla Ali Kichupa alisema kuwa alisema kuwa wananchi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wataendeleza ushindi wa chama hicho kama ilivyo kawaida ya Mkoa huo.

Nao wagombea wa Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa Wilaya hiyo ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja walieleza kuwa mwaka huu wataendelea kuvunja rekodi katika Wilaya na Mkoa wao.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mahmoud alitumia fursa hiyo kueleza mafaniko makubwa yaliopatikana katika uongozi wa Rais Dk. Shein.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na burudani kutoka kwa wasanii mbali mbali kutoka Zanzibar na Dar es Salaam ambao waliunogesha na kuivutia hadhira iliyohudhuria katika mkutano huo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.