Habari za Punde

OFISI YA ARDHI TABORA YATATUA MGOGORO KATI YA BIBI NA KANISA LA EAGT ULIODUMU ZAIDI YA MIAKA 20

 

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tabora Jabir Singano akimkabidhi Hati ya Ardhi Bi. Tamasha Mhanuka mkazi wa mtaa wa Bakari katika Manispaa ya Tabora mkoani Tabora baada ya mgogoro baina yake na Kanisa la EAGT kutatuliwa na ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano (aliyevaa suti) akiwaonesha ramani familia ya Kakurukuru na kampuni ya Tumbaku ya Alliance One Tobacco eneo la Ipuli Manispaa ya Tabora baada ya kutatua mgogoro uliodumu kwa miaka 23. Aliyevaa miwani ni Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One Tobacco David Mayunga.
Bi Tamasha Mhanuka mkazi wa Mtaa wa Bakari Manispaa ya Tabora akiwa mbele ya nyumba yake baada ya kutatuliwa mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 20 baina yake na Kanisa la EAGT.
Bi Tamasha Mhanuka akisalimiana na timu ya ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora  baada ya timu hiyo iliyoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Jabir Singano kufika eneo la Bibi huyo kumkabidhi hati ya Ardhi kufuatia kutatuliwa mgogoro baina yake na Kanisa la EAGT.
Bi Tamasha Mhanuka mkazi wa Mtaa wa Bakari Manispaa ya Tabora mkoani Tabora akipata ufafanuzi kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano baada ya kukabidhiwa Hati ya Ardhi kufuatia kutatuliwa mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 20 baina yake na Kanisa la EAGT. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)

Na Munir Shemweta, WANMM TABORA

Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Tanga imetatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati ya Kanisa la EAGT na bibi Tamasha Mhanuka kwenye eneo la mtaa wa Bakari Manispaa ya Tabora mkoani Tabora na kumkabidhi Hati.

Bibi Tamasha kwa muda mrefu amekuwa na mgogoro na Kanisa la EAGT lililotaka   kulichukua eneo hilo na maeneo ya wakazi wengine watano kwa ajili ya kuendesha shughuli za kanisa. Hata hivyo, wamiliki wa maeneo hayo walishindwa kukubaliana na Kanisa kuhusiana na fidia ya kuwaondoa.

Timu ya Ofisi ya Ardhi mkoa wa Tabora ikioongozwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Jabir Singano juzi ilikwenda eneo la Bi Tamasha lililopo mtaa wa Bakari njia kuu ya kuelekea Kigoma katika Manispaa ya Tabora na kumkabidhi Hati ya Ardhi sambamba na kumuonesha mipaka ya eneo lake ili aweze kufanya maendelezo aliyoshindwa kufanya kutokana na mgogoro huo.

Mkuu wa idara ya ardhi Manispaa ya Tabora Deo Damian Msilu alisema, chimbuko la mgogoro huo baina ya Bi. Tamasha na Kanisa la EAGT lilisababishwa na eneo hilo kuwa katika mpango wa matumizi ya umma yaani taasisi za dini na kupewa kanisa la EAGT.

Kwa mujibu wa Msilu, kilichotakiwa kufanyika ni uthamini wa kumlipa bibi Tamasha pamoja na wakazi wengine watano aliyekataa kuchukua fidia jambo lililosababisha ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora kubadilisha mpango wa matumizi ya eneo hilo na kuwa makazi.

Kwa upande wake kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora Jabir Singano alisema, ofisi yake imekuwa ikishirika kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa huo na moja ya mgogoro uliofanyiwa kazi ni wa bibi Tamasha na kanisa la EAGT.

Singano alisema, suala la mgogoro huo awali lilishughulikiwa na halmashauri ya Manispaa ya Tabora lakini halikupata ufumbuzi jambo lililoifanya ofisi yake mara baada ya kuanza kazi kuamua kulifanyia kazi hasa ikizingatiwa moja ya kazi ya ofisi hiyo ni kuhakikisha wanyonge wanabaki katika miji.

‘’Eneo la huyu bibi zuri kama mnavyoona liko katika barabara kuu ya kuelekea Kigoma na ni barabara ya lami na stendi iko umbali wa takriban kilometa moja, tuliliita kanisa na kuzungumza nalo ingawa kuna baadhi ya vipande lilipa fidia lakini kwa kuwa eneo hili lilikuwa ni utoaji binafsi ilibidi waachwe.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora aliongeza kwa kusema kuwa, baada ya kufikia muafaka na pande zote mbili waliamua kupima viwanja vitano na kuwaandalia Ankara ya malipo wamiliki wake ili watakapokamilisha wapatiwe hati na kumshukuru Mungu kwa kufanikisha kutatua mgogoro huo alioueleza kuwa ulikuwa ukimfanya Bi. Tamasha kushindwa kufanya maendelezo ya eneo kutokana na kutojua mipaka.

Singano alisema, kwa wananchi wote wenye migogoro ya aina hiyo waifikishe ofisi ya ardhi mkoa wa Tabora ili kupatiwa ufumbuzi na kusisitiza kuwa ofisi hiyo iko kwa ajili ya kutetea haki  ya kila mtu na aliye na haki atapata haki yake na aliyepora haki ya mtu atairudisha.

Naye Bi. Tamasha Mhanuka aliishukuru ofisi ya Adhi mkoa wa Tabora hasa Kamisha Msaidizi wa Ardhi Jabir Singano pamoja na Afisa Mipango Miji Faraji Shemgha kwa kusaidia kutatua mgogoro huo na kufanikisha kupatiwa hati ya eneo lake.

Aidha, Bi. Tamasha aliiomba serikali na wananchi wenye uwezo kumsaidia kufanikisha ujenzi wa nyumba yake aliyoieleza kuwa haiku katika hali nzuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.