Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein Ajumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam Zanzibar Katika Maulidi ya Kuzaliwa Mtume S.A.W Viwanja vya Maisara Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein akikabidhiwa CD ya Qasweeda ya Mwaka 1442 na Mdhamini wa Bodi ya Jumuiya ya Maulid Milade Nabii Association -Zanzibar Sheikh Sherali Champsi, wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Maulidi ya Kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliofanyika jana usiku 18/10/2020 na (kushoto kwa Rais) Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali na Rais Mstaaf wa Tanzania Alhajj Ali Hassan Mwinyi. 

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein jana aliwaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbali mbali katika Maulidi ya kuadhimisha Kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kitaifa yaliofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.

Sherehe hizo za kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambazo hufanyika kila mwaka Kitaifa hapa Zanzibar ni miongoni mwa kawaida na mila ya Waislamu wa Zanzibar ambazo hapa nchini zilianzishwa mapema mnamo mwaka 1926.

Alhaj Dk. Shein aliungana na Waislamu pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na viongozi wa Dini na wananchi akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhaj Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Alhaj Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mawaziri, Masheikh na viongozi wengine wa Serikali nao walihudhuria.

Nae, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan aliungana na viongozi wengine wanawake wa Kitaifa akiwemo Mama Mwanamwema Shein, Mama Asha Balozi, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma na wengineo.

Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi pamoja na waliohudhuria katika Maulid hayo akiwemo Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein ambaye ndio mlezi wa Maulid hayo huku akimpongeza kwa wazo lake la Maulid hayo kusomwa mapema ili kuepuka kuingiliana na uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika Sherehe  hizo, Waislamu walisisitizwa suala zima la kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na kutakiwa kufuata nyayo za Mtume Muhammad (S.A.W) ili wapate kuongoka hapa duniani na kesho akhera.

Akisoma khutba ya Maulid hayo, Sheikh Abdulaziz Saleh Juma kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana aliwataka  Waislamu kuwa kitu kimoja huku akiwasisitiza umuhimu wa kusaidiana na kuvumiliana kwa lengo la kupata rehema za Allah.

Sheikh Hassan  pia, alitumia fursa hiyo kumpongeza Alhaj Dk. Shein kwa kuiongoza Zanzibar kwa muda wa miaka kumi na kufanya mambo mengi mazuri aliyoyafanya na kusisitiza kuwa kwa vile hakuna cha kumlipa ni vyema akaombewa dua.

Akisisitiza umuhimu wa amani na utulivu hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 mwezi huu, Sheikh Abdulaziz Juma alieleza haja ya kudumisha amani na utulivu ili heri zaidi izidi kupatikana hapa nchini. “Uchaguzi sio vita wala kuhatarisha amani na utulivu bali uchaguzi ni sehemu ya demokrasia hivyo wananachi tunapaswa kuwa kitu kimoja”, alisema Sheikh Abdulaziz.

Sherehe hizo za Maulid ambazo husherehekewa duniani kote, zilianza kufunguliwa na Qur-an tukufu iliyosomwa na  Ustadhi Idd Ussi Haji kutoka Tazari Mkoa wa Kaskazi ni Unguja, ambapo tafsiri yake ilitolewa na Sheikh Abdullah Hamid kutoka Chuo cha Kislamu Mazizini Unguja.

Milango  ya Maulid Barzanji iliyoenda sambamba na Qasweeda ilisomwa na Maustadhi kutoka vyuo mbali mbali vya Qur-an kutoka Unguja na Pemba yakiwemo Maulid ya Hom kutoka Jumuiya ya Maulid ya Hom Mtendeni, Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo nayo yalikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo adhimu.

Katika sherehe hizo za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) Madrassa Noor El Islamiya ya Mji Mkongwe, Mjini Unguja walisoma Qiyaam Talaa, kilichotanguliwa na Mlango wa nne uliosomwa na Ustadhi Hassan Mdungi kutoka Tumbatu Jongowe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Qasweeda ya mwaka 1442 Al Hijra, ilisomwa na wanafunzi kutoka Madrassa Nassur Iman ya Mtoni Kijundu, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi  ambapo  Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maulid  Sheikh Sherali Chapsi alitumia fursa hiyo kama ilivyo kawaida kwa kila mwaka kumkabidhi Rais, Qasweeda hiyo maalum.

Maulid hayo yalimalizika kwa Mlango wa dua uliosomwa na Sheikh Abubaker Said Abubaker, kutoka Mji Mkongwe Unguja na hatimae kufungwa kwa fat-ha iliyosomwa na Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi chini ya mshereheshaji Sheikh Hamza Zubeir Rijal.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.